Mwaka 2011, nikiwa kwenye ziara ya Kichama Mkoani Mwanza kama Mjumbe wa Sekretarieti ya CCM, vijana wanaondesha Bodaboda Mwanza walinifuata kuomba msaada ili wamiliki pikipiki zao wenyewe na waondokane na kuajiriwa. Niliporudi Dar nilifanya mazungumzo na makampuni mbalimbali yanayouza pikipiki ili watengeneze utaratibu wa kuwakopesha. Nikiwa alike kwa gharama zangu viongozi wa Bodaboda kutoka Mwanza na kuwatambulisha kwenye makampuni hayo.
Baada ya taratibu mbalimbali kukamilika, kampuni moja ilianza kukopesha pikipiki kwa vijana hawa mwaka 2012. Hadi sasa zimekopeshwa pikipiki 224. Na zimeshatengwa nyingine 1,745 tayari kwa kukopeshwa. Tulifanya hivi bila kutangaza hadi pale Mwenyekiti wa Bodaboda Mwanza alipokumbusha huu mchakato kwenye mkutano wa hadhara.
Tarehe 1 Novemba nilipata barua ya Chama cha Waendesha Bodaboda Mwanza wakiniomba nishiriki nao kwenye sherehe ya kufunga mwaka. Wanasema walinialika pia kama sehemu ya kutoa shukrani kwa msaada wa kukopeshwa pikipiki. Nikawajibu kwamba binafsi sina interest na sherehe au matukio labda pale ambapo yana tija kwao. Nikawaambia kwamba miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ajali nyingi sana za pikipiki na kusababisha vifo na ulemavu kwa vijana wengi. Nikawaambia kwamba wenye pikipiki wanaweka Bima kwenye pikipiki zao, zikipata ajali wanalipwa lakini waendeshaji na abiria wakikatwa miguu na mikono ndio basi tena hata matibabu shida. Nikawaambia kwamba nitakubali kushiriki shughuli yao Mwanza iwapo tu watakubali tuwaanzishie utaratibu wa Bima. Bahati nzuri walikubali. Nikatafuta makampuni mawili ya Bima tukashauriana kuwe na package ya Bodaboda - Safari Njema na Bodaboda. Kwasababu vijana hawa wana kipato kidogo, utaratibu tulioweka unaruhusu kukata Bima hadi ya wiki moja kwa shilingi kuanzia 3,000 hadi 5,000 ambapo akipata ajali anaweza kufidiwa hadi shilingi milioni 10 pamoja na matibabu - lakini pia rambirambi na gharama za msiba pale atakapokuwa amefariki. Nilizindua program hii pale Nyamagana na vijana 100 walipata Bima papo hapo. Nafarijika kwamba vijana wale waliandaa vizuri shughuli ile na kulikuwa na pikipiki zaidi ya 1,200 uwanjani. Nafarijika kwa commitment yao ya kuacha shughuli kutwa nzima na kuchangishana mafuta yao. Nafarijika kwamba hatukufanya sherehe tu, tulifanya zaidi ya sherehe.
Hata hivyo kazi kubwa ipo kwenye kuzuia hizi ajali. Niliomba Mkuu wa Polisi wa Mkoa awepo pia ili kusisitiza haja ya kufuata sheria za Usalama Barabara. Mwaka 2011 walifariki watu 695 kwa ajali za bodaboda, mwaka 2012 walifariki 930. Tena hizi ni zile tu ajali zilizoripotiwa. Hili ni janga. Niliwaambia kwamba bodaboda ni ajira lakini Usalama kwanza, nao wakaamua kutengeneza fulana za ujumbe huo wakininukuu. Naamini ni ujumbe sahihi.
1 comment:
Nakupongeza kwa hatua nzuri hasa ya kufanikisha mpango wa bima kwa waendesha bodaboda.
Lakini msingi mkubwa wa tatizo la ajali za bodaboda uko katika ukosefu wa usimamizi makini katika utoaji wa leseni. Ulanguzi wa leseni unapelekea kuwa na madereva wasiofahamu sheria na utaratibu uendeshaji salama. Hiki ndicho kiini cha tatizo. Na utatuzi wake ni mgumu kuliko hiyo hatua uliyochukua.
Kuna haja ya kudhibiti chanzo na siyo matokeo. Bima ishughulikie matokeo ya ajali zisizozuilika ambazo ni asilimia chache sana.
Post a Comment