Monday, December 9, 2013

Kwanini Tunasherehekea Uhuru Wetu? January Makamba atoa Sababu 10.


Kwa bahati mbaya sana siku za karibuni kumetokea mtindo wa hovyo kwa baadhi ya Watanzania, ambao kwa makusudi au kwa kutokufahamu, wamekuwa wakitoa maneno ya dhihaka dhidi ya Uhuru wetu, hasa hasa katika siku kama ya leo ya Disemba 9.

Kwa mfano, wanabeza na kuuliza ipo wapi leo hii hiyo Tanganyika ya kuisherehekea? Wanauliza kwa dhihaka Miaka 52 baada ya Uhuru hakuna umeme, hakuna dawa mahospitalini, watoto wanakaa chini mashuleni n.k, kana kwamba hakuna chochote kilichofanyika au kilicho cha kujivunia. Ni kweli kabisa kuhusu yote hayo yanayotajwa sentensi ya juu kwavile changamoto bado zipo nyingi sana katika nchi yetu. Lakini wanaosema hayo pengine wanasahau kwamba kazi ya kujenga nchi yetu bado haijaisha, ndiyo kwanza imeanza.

Nimefanya tafsiri ya hotuba aliyotoa Ndugu January Makamba (MB) kwa Watanzania wanaoishi majimbo ya DMV Marekani juzi Jumamosi katika hafla ya kuadhimisha siku ya Uhuru. Sehemu kubwa hapa nimemkariri neno kwa neno. Kwa mtizamo wangu, Ndugu Makamba alifanikiwa kupangua hoja moja baada ya nyingine dhidi ya wale wanaodhihaki siku ya leo na akaeleza sababu 10 za msingi kwanini tunasherehekea Uhuru wetu.

Alianza kwa kufafanua kwamba leo hatuadhimishi Miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania, bali tunaadhimisha Miaka 52 ya Uhuru wa “Tanzania Bara”. Alitukumbusha kwamba Taifa letu ni Muungano wa nchi mbili. Ibara ya 2 (1) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inayotumika sasa inasema kwamba “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.” Tungeweza kusema leo tunasherehekea Miaka 52 ya Uhuru wa “Tanganyika”, lakini leo Tanganyika haipo tena na nafasi yake kikatiba leo hii inashikiliwa na Tanzania Bara.

January alisema kwamba Miaka 52 ni mingi sana kwa binadamu, lakini kwa Taifa ni miaka michache sana. Nchi ya Marekani, kwa mfano, imekuwa huru kwa Miaka zaidi ya 200. Safari yao katika kujenga nchi yao imekuwa ndefu na yenye mitihani mingi lakini bado wao wenyewe wanasema kazi ya kuijenga nchi yao kuwa bora zaidi haijakamilika (“the work of building a more perfect Union is not complete”). Kwahiyo kiumri utaona kwamba sisi ndio kwanza tumeanza safari ya kuijenga nchi yetu.

Hizi ndizo sababu 10 alizotoa Ndugu Makamba akijibu swali:

Kwanini tunasherehekea Uhuru wetu?

1)    Uhuru wetu bado upo, haujapotea. Japo leo hii Tanganyika haipo tena, bado tuna haki ya kusherehekea siku tulipopata Uhuru kwavile mpaka leo Uhuru huo tunao. Tuna mamlaka kamili na tunajitawala wenyewe tofauti na iliyokuwa awali. Katiba ya Tanzania niliyoitaja katika kifungu chake cha 151(1) kinafafanua kuhusu “Tanzania Bara” kuwa ni “eneo lote la Jamhuri ya Muungano ambalo zamani ilikuwa eneo la Jamhuri ya Tanganyika.” Kwa maana nyingine, japo jina la Tanganyika halitumiki tena, eneo lake bado lipo, watu wake bado wapo, mamlaka yake na Uhuru wake umezingatiwa na unatambulika ndani ya Katiba ya sasa. Kutokuwapo kwa Tanganyika ni kwa jina tu!

2)    Tunasherehekea kwavile kuwapo kwa Tanzania Bara kunapelekea kuwapo kwa NCHI ya Tanzania (kama jinsi Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo mwakani tutasherehekea Miaka 50, vile vile yanapelekea kuwapo kwa nchi ya Tanzania).

3)    Tunasherehekea Uhuru kama sehemu ya kuutambua UTAIFA wetu wa Tanzania.  Uhuru wetu ndio unaotambulisha Taifa letu. Wakati wa kupata Uhuru ndipo tulipopata mamlaka kamili, bendera, nembo, mipaka na pia tulitambulika na wenzetu duniani kwamba sisi ni Taifa.

4)    Tunasherehekea Uhuru wetu kama njia ya kukumbushana kuhusu haja ya kuendelea kuulinda Uhuru wetu.

5)    Tunasherehekea Uhuru wetu kama njia ya kukumbushana kuhusu haja ya kuendelea kuulinda Muungano wetu, kwa vile bila ya Uhuru (na Mapinduzi Zanzibar) tusingekuwa na Muungano.

6)    Tunasherehekea Uhuru wetu kwavile tuna haja pia ya kuwaenzi wale waliopigania Uhuru wetu kwa vile walifanya kazi kubwa, wengi walifungwa, wengi walipoteza mali zao na maisha yao ili sisi tuwe Huru.

7)    Tunasherehekea Uhuru wetu ili kukumbushana kwamba kazi ya kuijenga nchi yetu bado haijaisha. January alisema kwamba viongozi waliopigania Uhuru wetu walianza pia kazi ya kujenga Taifa letu kwa kutuunganisha katika makabila, katika dini n.k. Zikafanyika jitihadi nyingi na za makusudi za kuijenga nchi yetu ili iwe nchi moja ya watu wanaopendana, wanaoheshimiana, wanaoaminiana, wanaoshirikiana, wanaofanya kazi kwa pamoja katika kujenga Taifa. Hiyo kazi ya kujenga nchi yetu bado haijaisha kwa vile bado kuna changamoto nyingi sana za maendeleo. Vile vile, kuna changamoto mpya ambazo zimejitokeza zinazohatarisha Umoja wa Taifa letu. Hizi ni zile nyufa alizotaja Mwalimu Nyerere kama vile udini, ukabila, rushwa n.k. Kwahiyo Uhuru wetu upo hatarini sana kama hatutajidhatiti kwa dhati kuhakikisha kwamba bado tunaendelea na kazi ya ujenzi wa Taifa letu.

8)    Kuthaminiwa Utu wetu. January alikumbusha kwamba hii ndiyo ilikuwa sababu kubwa ya msingi kwanini wazee wetu walipigania kupata Uhuru. Walitaka kuondokana na kudhalilishwa, kutawaliwa, kutumwa, kunyanyaswa, kunyonywa na kuwa chini ya mtu mwingine kutoka sehemu nyingine. Mtu huyo anakuja anakalia nchi yako halafu anakufanya wewe kuwa ni mtu wa daraja la chini, kisha anakuamulia uishi vipi, anakuamulia lugha gani utumie, anaamua watoto wako wasome nini n.k. Wakasema hapana, kila mtu anahaki ya kuwa Huru na kuthaminiwa Utu wake, kujikomboa kwenye udhalimu na kujitoa kwenye udhalilishaji.

9)    Lengo la kupigania Uhuru lilikuwa ili tupate uwezo wa Kujiamulia mambo yetu yenyewe ili kutengeneze nchi ambayo tunaitaka sisi wenyewe. Lakini January aliweka bayana kwamba Malengo ya Uhuru bado hatujayafikia yote. Na ndiyo kazi ambayo sote tunapaswa kuifanya ili malengo hayo tuyafikie. Kila awamu ya uongozi wa nchi yetu baada ya Uhuru imetusogeza hatua moja au kadhaa kufikia Malengo ya Uhuru. Kikubwa ni kwamba bado tunayo kazi ya kujenga uwezo wa kiuchumi na uwezo wa kiutawala ili kuondoa umaskini wa watu wetu ili tuweze kufikia Malengo ya Uhuru wetu.

10)  Pamoja na changamoto zilizopo, ambazo alisema Serikali ya sasa chini ya Rais Kikwete inazitambua na inaendelea kuzifanyia kazi, nchi yetu bado ni nchi nzuri ya kuishi duniani. Hili pia ni jambo jema la kuherehekea wakati wa maadhimisho ya Uhuru. Watanzania bado kwa kiasi kikubwa ni wamoja, wanapendana na wanaheshimiana.

January alimaliza kwa kusema, “Nchi yetu bado inaweza kuwa nzuri sana kuliko ilivyo sasa. Sisi wenyewe tunaweza kuiharibu au kuijenga nchi yetu”.


No comments: