Wednesday, January 14, 2015

Maswali 40 kwa January Makamba


Maswali 40 ya Padre Karugendo

1  Kabla hatujaanza, na kabla sijasahau, nimekuwa na hamu kubwa ya kusikia kauli yako mwenyewe kuhusu hili suala la Urais. Mjadala wa Urais, hasa ndani ya Chama chenu, umekuwa mkali sana. Majina mengi yametajwa, ikiwemo lako. Je, ni kweli unaingia? Nimekusikia ukisema umefikia uamuzi wa kugombea kwa asilimia 90. Hiyo asilimia 10 bado tu?

2  Naamini watu wengi watapenda kujua January Makamba ni nani haswa. Hebu tuelezee kwa kifupi historia yako; ulizaliwa wapi, umekulia wapi, umepitia wapi, umefikaje hapa ulipo leo? Jina la baba yako limekubeba?

3  Je umeshapata watoto? Kama ni ndiyo ni wangapi? Je, mtazamo wako kuhusu familia na malezi ya watoto ni upi? Watu wanasema maji hufuata mkondo, je, ungependa watoto wako wawe wanasiasa kama wewe?

4  Umesema kwamba ulisomea Chuo Kikuu cha Kikatoliki Marekani. Kama ujuavyo, mimi ni Padre. Napenda kusikia kidogo kuhusu suala hili. Ulijifunza nini pale.

5  Umenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari ukisema kwamba sasa ni wakati wa viongozi vijana kujitokeza na kuchukua nafasi kubwa za uongozi kama Urais wa nchi. Kwa nini mjadala huu ni muhimu wakati huu na vitu gani vipya vya kuibadilisha Tanzania vinavyoweza kufanywa na vijana na si wazee? Kwanini vijana waaminiwe kwenye nafasi kubwa wakati hawana uzoefu wa kuongoza?

6  Je, umekomaa vya kutosha kushika nafasi ya Urais? Umefanya nini kwenye wizara yako, kiasi kwamba watu waweze kuamini kwamba unastahili nafasi ya juu zaidi ya hiyo uliyo nayo kwa sasa? Ulipochaguliwa kuwa Mbunge ulianzisha Shirika la Maendeleo Bumbuli. Nini kilikusukuma? Shirika linafanya nini na limewasaidia vipi watu wa Bumbuli. Je, kama jimbo bado lina changamoto unastahili kuomba nafasi ya juu?

7  Ni changamoto gani kubwa zinawakabili vijana wa Tanzania? Wanasiasa wengi wamekuwa wakisema watamaliza tatizo la ajira nchini. Kuna mawazo gani mapya kutoka kwa viongozi wa kizazi kipya ya kumaliza tatizo hili?

8  Kuna wazo kwamba nchi tukiigawa katika majimbo ya kiutawala, itapiga hatua za kimaendeleo kwa haraka. Kuna siku nilikusikia ukipinga wazo hili na ukasema kwamba badala ya majimbo ya kiutawala tuigawe nchi kwenye majimbo ya kiuchumi. Je, unaweza kufafanua fikra hizi?

9  Baada ya kuingia Bungeni, ulipewa nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati nyeti ya Nishati na Madini. Kwanza, tuambie uliwezaje kupata Uenyekiti wa Kamati nyeti katika wiki chache tu baada ya kuingia Bungeni. Tuelezee baadhi ya changamoto kwenye nafasi hii, lakini pia mlichukua hatua gani kulisaidia taifa kwenye sekta hizi nyeti? Ilikuwaje Kamati hii ikavunjwa mara tu baada ya wewe kuachia Uenyekiti? Nini kifanyike kumaliza tatizo la mgao wa umeme na bei kubwa za umeme?

10  Umeeleza kwamba ulikuwa sehemu ya kampeni ya Urais ya CCM mwaka 2005 na kwamba ulipata nafasi ya kuzunguka na Mheshimiwa Kikwete akiwa mgombea wa Urais wa CCM kwenye uchaguzi huo. Ulikuwa unafanya shughuli gani na ulijifunza nini katika shughuli ile?

11  Kwa miaka mitano na zaidi, ulipata nafasi ya pekee ya kuwa karibu na Rais wakati wote. Kutokana na nafasi hiyo ni mambo gani ya msingi uliyojifunza na yakakujenga kuwa kama ulivyo leo hii? Kwa nini uliamua kuacha kazi nzuri ya Ikulu na kwenda kugombea ubunge? Je, ilikuwa rahisi Rais kukuachia?

12  Hivi karibuni wananchi wengi hasa wa kipato cha chini na cha kati wamekuwa wakilalamika kwamba maisha yamekuwa makali, na gharama za maisha zimekuwa zikipanda kila kukicha. Maarifa gani yanahitajika ili kuweza kupunguza ukali wa maisha kwa Watanzania?

13  Watanzania wengi wanajishughulisha na kilimo, ufugaji na uvuvi lakini wamekuwa hawanufaiki na shughuli hizi licha ya mipango mingi tangu wakati wa uhuru hadi sasa. Je, kizazi kipya cha uongozi wa nchi kinapaswa kuwa na maarifa gani mapya kuhusu mapinduzi ya kilimo na maendeleo ya uvuvi na ufugaji?

14  Tanzania imekuwa ikisifika kwamba uchumi wake unakua kwa kasi kwa miaka kadhaa sasa. Lakini wananchi wengi bado hawajaona hayo manufaa. Nini kifanyike wananchi nao waone na wanufaike na uchumi kukua? Unauelezeaje uchumi wetu kwa ujumla?

15  Mwaka jana nilisoma kwenye vyombo vya habari kwamba ulipata tuzo ya taasisi ya National Democratic Institute ya Marekani, unaweza kutueleza ni tuzo ya nini na kwa nini uliipata? Pili, tulisoma kwamba uliteuliwa na taasisi ya World Economic Forum kuwa mmoja wa viongozi vijana mashuhuri duniani (Young Global Leaders). Pia tena majuzi tukasoma kwamba jarida mashuhuri duniani la Forbes limekutaja kuwa mmoja wa watu kumi wenye ushawishi Afrika kwa mwaka 2014. Ni kwanini unadhani wanakupa hizi tuzo? Na je, tuzo hizi zina maana gani kwa wapiga kura wako?

16  Kama kiongozi kijana uliyepata kufanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ikulu, unazungumziaje nafasi ya Tanzania katika siasa za kimataifa?

17  Tunaona jinsi nchi jirani zetu wanavyopata changamoto za usalama. Je, sisi tufanyaje kuepukana nazo?

18  Kiwango cha elimu katika taifa letu kimeporomoka, ni kwa nini na unafikiri ni kitu gani kifanyike kuinua hali ya elimu katika taifa letu?

19  Walimu ni sehemu kubwa ya watumishi wa umma. Je, wewe unayajua matatizo yao? Una fikra na mawazo gani ya kuyashughulikia? Vipi kuhusu wahadhiri wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu?

20  Kumekuwa na malalamiko kuhusu utendaji Serikalini, hasa juu ya urasimu; kwamba maamuzi hayafanyiki kwa wakati, lakini pia hakuna uwajibikaji. Je, nini kifanyike kurekebisha hali hii?

21  Mfumo mpya wa Matokeo Makubwa Sasa, BRN, ni mwanzo mzuri lakini lazima uende sambamba na uwezo wa kufanya maamuzi na kuchukua hatua za uwajibikaji pale matokeo makubwa yanapokuwa hayajapatikana.Wananchi wanalalamikia sana ufisadi. Mikakati ya sasa inaelekea haijafanikiwa kiasi cha kuridhisha wananchi. Je, wewe una mbinu zozote mpya za kupambana na tatizo hili? Je, unaongeleaje ufisadi wa Richmond, EPA na IPTL?

22  Kumekuwa na hii dhana ya kufanya maamuzi magumu kama sifa ya uongozi. Je, unalisemeaje hili? Je, wewe umeshawahi kufanya maamuzi yoyote magumu kwenye uongozi wako?

23  Hapa tupo Dar es Salaam. Inaelekea karibu kila mtu anataka kuhamia na kuishi Dar es Salaam. Una maoni gani kuhusu nafasi ya Jiji la Dar es Salaam katika maendeleo ya nchi yetu? Nini changamoto za jiji hili na nini kifanyike kuzirekebisha?

24  Mwaka 2012 ulipeleka Bungeni Muswada Binafsi wa Sheria ya Kudhibiti shughuli za Upangishaji Nyumba. Tuelezee maudhui yake, nini kilikusukuma na muswada huo umefikia wapi?

25  Inaelekea siku hizi kila mwanasiasa anajikita katika kundi la vijana na kuzungumzia masuala yanayowavutia vijana. Hakuna makundi mengine ya kuyasemea? Ni makundi gani na mahitaji yao ni yapi na ufumbuzi wa changamoto zao ni upi?

26  Umekuwa mmoja ya viongozi ambao wanaliongelea sana suala la mabadiliko ya kasi ya kuongezeka kwa idadi ya watu nchini na taifa kuwa changa kiumri. Unaweza kutuelezea kwa upana nini maana ya mabadiliko haya kwenye mustakabali wa taifa letu la leo na la kesho?

27  Miaka ya hivi karibuni imejitokeza dalili kwamba mahusiano ya watanzania wenye dini tofauti si mazuri na kuna dalili kwamba hali hii inaweza kuleta kutoelewana siku za usoni. Wewe unalisemeaje suala hili? Nini nafasi ya imani ya kiroho katika kumwongoza Kiongozi wa nchi?

28  Wewe kama kiongozi kijana, umewasaidiaje hawa vijana wenzenu wa Bongo Movies na vijana wa muziki wa kizazi kipya maana yake kila siku wanalalamika. Pia inaelekea tumetelekeza maendeleo ya sanaa kwa ujumla. Tufanyeje?

29  Tanzania imekuwa ikijulikana kama kichwa cha mwendawazimu kwenye medani ya michezo ya kimataifa. Ni muda mrefu sasa tumeshindwa kupata medali zozote kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola au Olimpiki. Mara ya mwisho kwa Taifa Stars kushiriki fainali za kombe la Mataifa ya Afrika ilikuwa ni miaka 36 iliyopita. Una fikra gani mpya katika kulirekebisha hili na kuwafanya Watanzania kujisikia fahari kutokana na mafanikio ya wanamichezo wake?

30  Watu wengi wamekuwa wanalalamikia bandari na reli. Wengine wanasema kwamba kwa takribani miaka kumi sasa bandari na reli ziko vilevile, hakuna upanuzi wala ujenzi mpya. Una maoni gani kuhusu miundombinu ya usafirishaji? Nini kipya kinaweza kufanyika? 

31  Nimetembea sana vijijini na nimeona kuwa vijiji vingi havina huduma yoyote ya afya. Hata kule ambapo zipo watumishi hawatoshi, vifaa hakuna, hakuna umeme, na wakati wote hakuna dawa. Ukienda hospitali, iwe ndogo au kubwa, una hatari ya kupata ugonjwa kuliko nyumbani. Haya matatizo wewe unayaonaje? Kwa kweli watu hawamudu gharama za matibabu na wanakufa bila sababu za msingi. Nini kifanyike? 

32  Umesema kwamba Rais Kikwete amejitahidi kuboresha huduma. Unadhani ni huduma gani ya jamii bado ni kero kwa Watanzania na unadhani kuna maarifa gani mapya ya kuitatua?

33  Ukiwa kama kiongozi kijana wa CCM, uliyepata fursa ya kuwa kiongozi wa juu wa Chama chenu, huoni kama Chama chenu kimepoteza mwelekeo na kinapata ushindani mkubwa sasa? Kuna sababu za Chama chenu kuendelea kuaminiwa na Watanzania? Ukichaguliwa Rais, pia unakuwa Mwenyekiti wa CCM, je kijana anaweza kukiongoza Chama kikongwe kama CCM?

34  Hapa Tanzania karibu kila mtu, hata ambao ni watumishi wa Serikali na hata wananchi wa vijijini ni wajasiriamali. Lakini ujasiriamali unakwamishwa na ukosefu wa mikopo. Benki ziko nyingi lakini hazikopeshi watu maskini ambao hawana dhamana. Taasisi za ukopeshaji, microfinance, zimejaa lakini riba ni kubwa na watu wanashindwa. Kulikuwa na Mabilioni ya JK lakini hayakufika mbali. Kuna jambo gani kubwa na jipya la kumaliza tatizo hili?

35  Nini nafasi ya uhuru wa vyombo vya habari katika kuchochea maendeleo ya taifa letu. Unaongeleaje suala la kuwa na vyombo vya habari vingi ambavyo vinaandika habari za uchochezi?  

36  Baada ya uvumbuzi wa gesi nchini, kumekuwa na mjadala kuhusu Watanzania kunufaika na rasilimali za taifa hili. Una maoni gani kuhusu huu mjadala? Nini kifanyike ili watu wa hali ya chini wanufaike? Kama kiongozi umeshiriki vipi kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali zao?

37  Wakati wa Bajeti, kila tunapozungumzia kutotekelezwa kwa miradi ya maendeleo, kutolipwa kwa wazabuni, kutolipwa kwa walimu na askari, tunasikia sana msemo wa “kasungura kadogo”. Je, kutokana na hali hii, kuna matumaini ya kupata maendeleo kama kila wakati Serikali inasema haina fedha ya kutekeleza majukumu yake ya msingi? Je, kuna maarifa gani mapya, ambayo wewe kama kiongozi wa kizazi kipya, ambayo unayo kuhusu namna ya kupata fedha za maendeleo?

38  Mwaka jana niliona picha yako kwenye gazeti ukiwa Butiama na Mama Maria Nyerere mkiomba pembeni ya kaburi la Mwalimu Nyerere. Ulifikaje huko? Mama Maria alikupa usia gani? Unazungumziaje nafasi ya Mwalimu Nyerere kwenye siasa za sasa za nchi yetu?

39  Je, kati ya marais wanne waliowahi kuliongoza taifa letu, unafikiri ni rais gani ameacha historia kubwa kama Rais aliyefanya mambo makubwa kuliko wote katika taifa letu?

40  Kuna mambo yoyote unayodhani hatukuyazungumzia ambayo unadhani yana umuhimu katika ustawi wa nchi yetu?