Thursday, July 2, 2015

MAELEZO YA NDUGU JANUARY MAKAMBA WAKATI WA KURUDISHA FOMU YA KUOMBA KUTEULIWA NA CCM KWA NAFASI YA URAIS, 2 JULAI 2015Ninayo furaha kubwa kukamilisha zoezi la kupata wadhamini katika mikoa
28 kati ya 31 ya nchi yetu. Kila nilikopita walijitokeza wadhamini
wengi kunidhamini kuliko idadi iliyohitajika. Nawashukuru wote
waliojitokeza kunidhamini. Nawashukuru pia viongozi wa CCM, ikiwemo
Makatibu wa Wilaya na Mikoa, kwa ushirikiano mkubwa walionipa na
weledi mkubwa waliounyesha. Nakishukuru Chama changu kwa kuweka
utaratibu mzuri na wa wazi ambapo wagombea wote tulipewa haki na hadhi
sawa katika zoezi hili. Kasoro za hapa na pale zilizojitokeza ni ndogo
sana na zinarekebishika.

Nimesafiri sehemu kubwa ya nchi yetu, sehemu nyingi kwa basi, na
kukutana na wanachama na viongozi wa CCM pamoja na wananchi. Kila
nilikopita yalijitokeza makundi makubwa ya wana-CCM na wananchi
kunilaki, kunidhamini na kunisikiliza. Nimeguswa sana na wingi na
hamasa kubwa ya watu. Nimepata fursa ya kusikiliza maoni, mawazo na
fikra zao. Kwa kifupi, nimeshuhudia yafuatayo:

1.      CCM bado ni Chama imara na hakuna shaka kabisa kwamba kitashinda
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. CCM itashinda kwa nguvu ya wananchi na
wanachama na viongozi wa CCM kuanzia kwenye ngazi za mashina, kwa
utekelezaji wa Ilani yake na ahadi za viongozi wake, kwa Ilani nzuri
itakayowasilishwa kwa wananchi, kwa usafi na umahiri wa wagombea
itakaowasimamisha, na kwa kazi nzuri ya kuimarisha Chama iliyofanywa
na Sekretarieti ya CCM chini ya Katibu Mkuu Ndugu Kinana na Kamati Kuu
na Halmashauri Kuu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

2.      Wananchi wengi, hasa vijana. wanaangalia CCM itamteua mgombea wa
aina gani. Wengi wanataka aina mpya ya uongozi, uongozi unaoangalia
mbele zaidi, uongozi unaoakisi matarajio yao.

3.      Wana-CCM, kama walivyo wananchi wote, wanachukizwa na rushwa na
matumizi mabaya ya madaraka na wanachukizwa na Chama chao kuhusishwa
na masuala hayo. Masuala ya uwajibikaji na maadili na miiko ya
viongozi yatakuwa sehemu kubwa ya mjadala na ajenda kwenye Uchaguzi
Mkuu.

4.      Wana-CCM wanataka wagombea wa CCM kwa nafasi za ngazi zote ambao
wana mvuto kwa watu na ambao itakuwa rahisi kuwanadi bila kuwatolea
maelezo au utetezi kwanza. Wana-CCM wanatambua kwamba Chama chao
kinayo hazina kubwa ya viongozi wa aina hiyo.

5.      Wana-CCM wanataka Chama chao kiendelee kuwa na umoja na mshikamano.
Wanachukizwa na vitendo vya kushambuliana, kushutumiana, kuhujumiana,
kuchafuana na uadui baina ya wana-CCM. Wanataka wagombea ambao sio
sehemu ya mambo haya, ambao hawana uadui na wana-CCM wenzao. Bahati
nzuri viongozi wa aina hiyo wapo ndani ya CCM.

6.      Watanzania wanataka CCM iendelee wajibu wake wa msingi wa kuwasemea
wanyonge, kukemea dhulma na maovu kwenye jamii, na kukabiliana na hali
duni ya maisha ya Watanzania.

Katika mazungumzo yangu na wadhamini wangu na wana-CCM kwa ujumla,
ujumbe wangu ulijumuisha yafuatayo:

1.      Mwaka 1995, Mwenyekiti wa Kwanza wa CCM, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM wa kumteua mgombea
Urais wa CCM, alisema kwamba “Watanzania wanataka mabadiliko.
Wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM”. Miaka 20 baadaye,
kauli ile ya Mwalimu bado iko sahihi. Katika uchaguzi wa mwaka huu,
CCM inayo nafasi ya kuwapa Watanzania aina ya mgombea ambaye
anaashiria na anaakisi mabadiliko ambayo Watanzania wanayataka.

2.      Rais na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Ndugu Benjamin William Mkapa,
mwaka 2005, wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM wa kumteua mgombea
Urais wa CCM, alisema ni muhimu CCM ikatazama aina ya wapiga kura
waliopo, ambao wengi ni vijana, na kuwapatia mgombea anayeendana nao.
Miaka 10 baadaye, kauli hiyo ya Mzee Mkapa bado iko sahihi.

3.      Nina imani kwamba mchakato wa kumpata mgombea wetu wa Urais
utazingatia busara hizi za Wenyeviti wetu waliotangulia, busara
zilizofanya Chama chetu kupata wagombea sahihi mwaka 1995 na 2005.
Nina imani kubwa na viongozi wakuu wa Chama chetu katika kutuongoza
kupata mgombea anayeakisi hadhi, heshima na dhamana ya Chama chetu.

4.       Rais na Mwenyekiti Mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, alipata kusema
“kila zama na kitabu chake”. Umri sio sifa ya uongozi lakini uongozi
unaenda kwa rika au kizazi. Kila kizazi kina wakati wake. Kila zama
zina changamoto na mahitaji yake. Na kila kizazi kina wajibu mahsusi
wa kukabiliana na changamoto za wakati wake. Vizazi vilivyopita vya
viongozi wetu vimeiongoza nchi yetu vizuri na mafanikio yako dhahiri.
Baada ya miaka zaidi ya 50 ya uhuru, sasa ni wakati wa kizazi kingine
kitakachokuja na fikra mpya, mtazamo mpya na majawabu mapya kwa
changamoto za sasa.  Ni vema utamaduni tulio nao wa kizazi kimoja cha
viongozi kukabidhi madaraka kwa kizazi kinachofuatia ukaendelea.

5.      Katika kuomba nafasi hii, ni vyema kutosahau kwamba bado tunaye
Rais ambaye amefanya kazi nzuri na anaendelea kufanya kazi nzuri.
Tusizungumze kana kwamba hakuna kilichofanyika. Yoyote atakayepata
heshima ya kuliongoza taifa letu ataanzia alipoishia.

6.      Nafasi hii ni ya hadhi, heshima na dhamana kubwa. Ni muhimu
kujitafakari kwa kina kabla ya kuiomba. Lakini pia ni muhimu kuiomba
kwa staha, unyenyekevu na hekima na kwa namna inayoendana na hadhi,
heshima na dhamana ya nafasi yenyewe. Anayeiomba nafasi hii kwa namna
tofauti ni hii, haistahili nafasi hii.

7.      Binafsi, nimejitafakari kwa kina. Nimejiandaa na nimeandaliwa
vizuri kiuongozi na kimaadili kwenye Chama chetu, Serikali, Bungeni na
kwenye utumishi wangu ndani ya Ikulu. Nafasi hii naiweza, tena naiweza
vizuri. Nafahamu ukubwa wa dhamana hii. Nafahamu misingi iliyoijenga
nchi yetu na nafahamu urithi wa taifa hili na wajibu wa kuilinda
misingi hiyo na urithi huo. Siombi nafasi hii kwa kujaribisha au kwa
kujiandaa kwa wakati ujao. Wakati ni sasa na niko tayari. Nafahamu
nini kipya kinahitajika kufanywa kwenye ajira, elimu, afya, maji,
uvuvi, kilimo, ufugaji, migogoro ya ardhi, umeme, uwezeshaji wa
biashara ndogo, barabara, reli, kodi, mikopo ya wanafunzi, masuala ya
haki na uhuru wa watu, uwekezaji, usalama wa watu na mali zao,
muungano na umoja, upendo na mshikamano wa Watanzania, matumizi ya
rasilimali za nchi na masuala ya maadili na uwajibikaji.

8.      Katika mchakato huu, sijatenda na wala sitatenda kitendo hata
chenye chembechembe ya kujenga kundi au kukidhoofisha Chama chetu.
Kundi langu ni CCM, kabla, wakati na baada ya mchakato huu.

9.      Natambua pia kwamba mgombea atakayeteuliwa na Chama chetu, pia
atakuja kupata heshima ya kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Chama.
Kwahiyo ni muhimu awe anakijua Chama vizuri. Binafsi, nimelelewa na
kukulia ndani ya CCM. Nimekuwa chipukizi wa CCM, nimekuwa kiongozi wa
Umoja wa Vijana wa CCM, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya; nimekuwa
kwenye Sekretarieti ya Chama Taifa kama Katibu wa Siasa na Mambo ya
Nje, ambapo ofisi yangu ya kazi ilikuwa ni Makao Makuu ya CCM,
nimekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, na ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa. Nimekuwa Mlezi wa Chama wa Mkoa wa Kigoma na sasa Mlezi wa
Shirikisho la Wana-CCM katika vyuo vikuu. Sijakichangamkia Chama
kwasababu naomba madaraka. Nakifahamu vizuri Chama chetu. Nafahamu
umuhimu wa Chama kujiimarisha kiuchumi. Nafahamu umuhimu wa watendaji
na watumishi wa Chama na Jumuiya wa ngazi zote kupata vitendea kazi
stahiki na kuangaliwa maslahi yao. Nafahamu umuhimu wa kazi
zinazofanywa na viongozi wa Chama wa ngazi zote na haja ya kazi hizo
kutambuliwa na kuwezeshwa. Sitakuwa mwanafunzi katika kukiongoza Chama
chetu.

10.     Katika siku chache zijazo, mchakato huu utafikia ukingoni.  Baada
ya hapo, Chama chetu kitapata mgombea mmoja tu atakayepeperusha
bendera ya Chama chetu kwenye Uchaguzi Mkuu. Ni muhimu sisi
tuliionyesha nia ya kuomba nafasi hii kuelewa kuwa umoja wetu ndio
ushindi wetu. Kama nilivyokwishasema, nina imani kubwa na uongozi wa
Chama chetu, nina imani kubwa na vikao na kanuni zitakazotumika
kuchuja wagombea. Nina imani haki itatendeka na tutamaliza mchakato
huu tukiwa wamoja. Nina imani kwamba vikao vitafanya maamuzi kwa
msingi wa kujiamini na sio kwa msingi wa shaka ya kusambaratika. CCM
ni taasisi kubwa. Kama Chama, katika historia yetu, tumepita kwenye
michakato mingi migumu kuliko hata huu, tumefanya maamuzi mengi
makubwa na bado tumeendelea kubaki wamoja na imara. Nina imani kwamba
katika hili pia tutavuka salama.

11.     Nawapongeza wanachama wenzangu walioonyesha ujasiri na kiu ya
kutaka kuliongoza taifa letu. Nafarijika kwamba ndani ya CCM kuna
hazina kubwa ya viongozi. Sina kinyongo na nawaheshimu baadhi ya
viongozi waliokwishaamua kuwaunga mkono wagombea wengine. Nina imani
kwamba kadri mchakato huu utakavyoendelea kwenye vikao vya Chama,
nitapata heshima ya wao kuja kuniunga mkono. Niko tayari kufanya kazi
na wagombea waliojitokeza na wale waliowaunga mkono, kazi ya kuendelea
kukijenga na kukiimarisha Chama chetu na kutatua changamoto za
Watanzania.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIANo comments: