Ninayo furaha kubwa kukamilisha zoezi la kupata wadhamini katika mikoa 28 kati ya 31 ya nchi yetu. Kila nilikopita walijitokeza wadhamini wengi kunidhamini kuliko idadi iliyohitajika. Nawashukuru wote waliojitokeza kunidhamini. Nawashukuru pia viongozi wa CCM, ikiwemo Makatibu wa Wilaya na Mikoa, kwa ushirikiano mkubwa walionipa na weledi mkubwa waliounyesha. Nakishukuru Chama changu kwa kuweka utaratibu mzuri na wa wazi ambapo wagombea wote tulipewa haki na hadhi sawa katika zoezi hili. Kasoro za hapa na pale zilizojitokeza ni ndogo sana na zinarekebishika.
Nimesafiri sehemu kubwa ya nchi yetu, sehemu nyingi kwa basi, na kukutana na wanachama na viongozi wa CCM pamoja na wananchi. Kila nilikopita yalijitokeza makundi makubwa ya wana-CCM na wananchi kunilaki, kunidhamini na kunisikiliza. Nimeguswa sana na wingi na hamasa kubwa ya watu. Nimepata fursa ya kusikiliza maoni, mawazo na fikra zao. Kwa kifupi, nimeshuhudia yafuatayo:
1. CCM bado ni Chama imara na hakuna shaka kabisa kwamba kitashinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. CCM itashinda kwa nguvu ya wananchi na wanachama na viongozi wa CCM kuanzia kwenye ngazi za mashina, kwa utekelezaji wa Ilani yake na ahadi za viongozi wake, kwa Ilani nzuri itakayowasilishwa kwa wananchi, kwa usafi na umahiri wa wagombea itakaowasimamisha, na kwa kazi nzuri ya kuimarisha Chama iliyofanywa na Sekretarieti ya CCM chini ya Katibu Mkuu Ndugu Kinana na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
2. Wananchi wengi, hasa vijana. wanaangalia CCM itamteua mgombea wa aina gani. Wengi wanataka aina mpya ya uongozi, uongozi unaoangalia mbele zaidi, uongozi unaoakisi matarajio yao.
3. Wana-CCM, kama walivyo wananchi wote, wanachukizwa na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na wanachukizwa na Chama chao kuhusishwa na masuala hayo. Masuala ya uwajibikaji na maadili na miiko ya viongozi yatakuwa sehemu kubwa ya mjadala na ajenda kwenye Uchaguzi Mkuu.
4. Wana-CCM wanataka wagombea wa CCM kwa nafasi za ngazi zote ambao wana mvuto kwa watu na ambao itakuwa rahisi kuwanadi bila kuwatolea maelezo au utetezi kwanza. Wana-CCM wanatambua kwamba Chama chao kinayo hazina kubwa ya viongozi wa aina hiyo.
5. Wana-CCM wanataka Chama chao kiendelee kuwa na umoja na mshikamano. Wanachukizwa na vitendo vya kushambuliana, kushutumiana, kuhujumiana, kuchafuana na uadui baina ya wana-CCM. Wanataka wagombea ambao sio sehemu ya mambo haya, ambao hawana uadui na wana-CCM wenzao. Bahati nzuri viongozi wa aina hiyo wapo ndani ya CCM.
6. Watanzania wanataka CCM iendelee wajibu wake wa msingi wa kuwasemea wanyonge, kukemea dhulma na maovu kwenye jamii, na kukabiliana na hali duni ya maisha ya Watanzania.
Katika mazungumzo yangu na wadhamini wangu na wana-CCM kwa ujumla, ujumbe wangu ulijumuisha yafuatayo:
1. Mwaka 1995, Mwenyekiti wa Kwanza wa CCM, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM wa kumteua mgombea Urais wa CCM, alisema kwamba “Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM”. Miaka 20 baadaye, kauli ile ya Mwalimu bado iko sahihi. Katika uchaguzi wa mwaka huu, CCM inayo nafasi ya kuwapa Watanzania aina ya mgombea ambaye anaashiria na anaakisi mabadiliko ambayo Watanzania wanayataka.
2. Rais na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Ndugu Benjamin William Mkapa, mwaka 2005, wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM wa kumteua mgombea Urais wa CCM, alisema ni muhimu CCM ikatazama aina ya wapiga kura waliopo, ambao wengi ni vijana, na kuwapatia mgombea anayeendana nao. Miaka 10 baadaye, kauli hiyo ya Mzee Mkapa bado iko sahihi.
3. Nina imani kwamba mchakato wa kumpata mgombea wetu wa Urais utazingatia busara hizi za Wenyeviti wetu waliotangulia, busara zilizofanya Chama chetu kupata wagombea sahihi mwaka 1995 na 2005. Nina imani kubwa na viongozi wakuu wa Chama chetu katika kutuongoza kupata mgombea anayeakisi hadhi, heshima na dhamana ya Chama chetu.
4. Rais na Mwenyekiti Mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, alipata kusema “kila zama na kitabu chake”. Umri sio sifa ya uongozi lakini uongozi unaenda kwa rika au kizazi. Kila kizazi kina wakati wake. Kila zama zina changamoto na mahitaji yake. Na kila kizazi kina wajibu mahsusi wa kukabiliana na changamoto za wakati wake. Vizazi vilivyopita vya viongozi wetu vimeiongoza nchi yetu vizuri na mafanikio yako dhahiri. Baada ya miaka zaidi ya 50 ya uhuru, sasa ni wakati wa kizazi kingine kitakachokuja na fikra mpya, mtazamo mpya na majawabu mapya kwa changamoto za sasa. Ni vema utamaduni tulio nao wa kizazi kimoja cha viongozi kukabidhi madaraka kwa kizazi kinachofuatia ukaendelea.
5. Katika kuomba nafasi hii, ni vyema kutosahau kwamba bado tunaye Rais ambaye amefanya kazi nzuri na anaendelea kufanya kazi nzuri. Tusizungumze kana kwamba hakuna kilichofanyika. Yoyote atakayepata heshima ya kuliongoza taifa letu ataanzia alipoishia.
6. Nafasi hii ni ya hadhi, heshima na dhamana kubwa. Ni muhimu kujitafakari kwa kina kabla ya kuiomba. Lakini pia ni muhimu kuiomba kwa staha, unyenyekevu na hekima na kwa namna inayoendana na hadhi, heshima na dhamana ya nafasi yenyewe. Anayeiomba nafasi hii kwa namna tofauti ni hii, haistahili nafasi hii.
7. Binafsi, nimejitafakari kwa kina. Nimejiandaa na nimeandaliwa vizuri kiuongozi na kimaadili kwenye Chama chetu, Serikali, Bungeni na kwenye utumishi wangu ndani ya Ikulu. Nafasi hii naiweza, tena naiweza vizuri. Nafahamu ukubwa wa dhamana hii. Nafahamu misingi iliyoijenga nchi yetu na nafahamu urithi wa taifa hili na wajibu wa kuilinda misingi hiyo na urithi huo. Siombi nafasi hii kwa kujaribisha au kwa kujiandaa kwa wakati ujao. Wakati ni sasa na niko tayari. Nafahamu nini kipya kinahitajika kufanywa kwenye ajira, elimu, afya, maji, uvuvi, kilimo, ufugaji, migogoro ya ardhi, umeme, uwezeshaji wa biashara ndogo, barabara, reli, kodi, mikopo ya wanafunzi, masuala ya haki na uhuru wa watu, uwekezaji, usalama wa watu na mali zao, muungano na umoja, upendo na mshikamano wa Watanzania, matumizi ya rasilimali za nchi na masuala ya maadili na uwajibikaji.
8. Katika mchakato huu, sijatenda na wala sitatenda kitendo hata chenye chembechembe ya kujenga kundi au kukidhoofisha Chama chetu. Kundi langu ni CCM, kabla, wakati na baada ya mchakato huu.
9. Natambua pia kwamba mgombea atakayeteuliwa na Chama chetu, pia atakuja kupata heshima ya kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Chama. Kwahiyo ni muhimu awe anakijua Chama vizuri. Binafsi, nimelelewa na kukulia ndani ya CCM. Nimekuwa chipukizi wa CCM, nimekuwa kiongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya; nimekuwa kwenye Sekretarieti ya Chama Taifa kama Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje, ambapo ofisi yangu ya kazi ilikuwa ni Makao Makuu ya CCM, nimekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, na ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Nimekuwa Mlezi wa Chama wa Mkoa wa Kigoma na sasa Mlezi wa Shirikisho la Wana-CCM katika vyuo vikuu. Sijakichangamkia Chama kwasababu naomba madaraka. Nakifahamu vizuri Chama chetu. Nafahamu umuhimu wa Chama kujiimarisha kiuchumi. Nafahamu umuhimu wa watendaji na watumishi wa Chama na Jumuiya wa ngazi zote kupata vitendea kazi stahiki na kuangaliwa maslahi yao. Nafahamu umuhimu wa kazi zinazofanywa na viongozi wa Chama wa ngazi zote na haja ya kazi hizo kutambuliwa na kuwezeshwa. Sitakuwa mwanafunzi katika kukiongoza Chama chetu.
10. Katika siku chache zijazo, mchakato huu utafikia ukingoni. Baada ya hapo, Chama chetu kitapata mgombea mmoja tu atakayepeperusha bendera ya Chama chetu kwenye Uchaguzi Mkuu. Ni muhimu sisi tuliionyesha nia ya kuomba nafasi hii kuelewa kuwa umoja wetu ndio ushindi wetu. Kama nilivyokwishasema, nina imani kubwa na uongozi wa Chama chetu, nina imani kubwa na vikao na kanuni zitakazotumika kuchuja wagombea. Nina imani haki itatendeka na tutamaliza mchakato huu tukiwa wamoja. Nina imani kwamba vikao vitafanya maamuzi kwa msingi wa kujiamini na sio kwa msingi wa shaka ya kusambaratika. CCM ni taasisi kubwa. Kama Chama, katika historia yetu, tumepita kwenye michakato mingi migumu kuliko hata huu, tumefanya maamuzi mengi makubwa na bado tumeendelea kubaki wamoja na imara. Nina imani kwamba katika hili pia tutavuka salama.
11. Nawapongeza wanachama wenzangu walioonyesha ujasiri na kiu ya kutaka kuliongoza taifa letu. Nafarijika kwamba ndani ya CCM kuna hazina kubwa ya viongozi. Sina kinyongo na nawaheshimu baadhi ya viongozi waliokwishaamua kuwaunga mkono wagombea wengine. Nina imani kwamba kadri mchakato huu utakavyoendelea kwenye vikao vya Chama, nitapata heshima ya wao kuja kuniunga mkono. Niko tayari kufanya kazi na wagombea waliojitokeza na wale waliowaunga mkono, kazi ya kuendelea kukijenga na kukiimarisha Chama chetu na kutatua changamoto za Watanzania.