Wednesday, November 12, 2014

Maoni ya Ndugu January Makamba (MB) Kuhusu Utafiti wa Taasisi ya Twaweza Kuelekea 2015

Maoni ya Ndugu January Makamba (MB) Kuhusu Utafiti wa Taasisi ya Twaweza Kuelekea 2015 

Hatimaye nimepata fursa ya kusoma matokeo ya utafiti uliofanywa na Twaweza.  Tumeyapokea na binafsi nawapongeza Twaweza kwa kazi nzuri wanayofanya ya kupata hisia za wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nchini. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza tangu matoleo haya yaanze,  nimepata simu na ujumbe mwingi ikiwemo kutoka kwa magwiji wa sayansi ya ukusanyaji maoni wakiniuliza maswali mengi kuhusu misingi ya sayansi ya kupata maoni, kwa mfano dhana ya kuwapa watu simu za mikononi na chaja za sola ili watoe maoni na dhana ya kuwa na sampuli hiyo hiyo ya watu 2,000 kutoka Tanzania Bara pekee kila mara maoni yanapokusanywa. Binafsi sio mtaalam wa sayansi ya ukusanyaji maoni kwahiyo sina uhakika kama utaratibu uliotumika unabatilisha matokeo haya. Pamoja na hayo, utafiti huu unatupa mambo kadhaa muhimu ya kutafakari na hakuna sababu ya kutumia muda mrefu kujadili mbinu za ukusanyaji maoni. Binafsi, ninayo maoni yafuatayo kuhusu kura hii ya maoni.

Mosi, kuhusu suala la mgombea wa urais wa CCM, ukweli ni kwamba anateuliwa kwa misingi na taratibu za ndani ya Chama na kutokana na sifa 13 zilizowekwa na Chama. Mwaka 1995, Mwalimu Nyerere aliongoza kuenguliwa kwa wagombea wawili katika ngazi ya Kamati Kuu ambao licha ya umaarufu wao katika kura za maoni, walipungukiwa na sifa za kushika nafasi hiyo na tukapata mgombea ambaye hakuna aliyekuwa anamfikiria. Kwahiyo, kura hii ya maoni haina uhusiano na uamuzi wa uteuzi wa mgombea wa CCM. Bahati nzuri, katika maelezo yao ya utafiti, Twaweza hili wamelieleza.  

Pili, tunaona pia katika kura hii ya maoni kwamba bado Watanzania wengi hawajaamua nani awe kiongozi wao. Ingetegemewa kwamba viongozi ambao wamo kwenye siasa kwa miaka 40 sasa na wanaoshikilia au waliowahi kushikilia nyadhifa za juu, na wengine hata kuwahi kuomba nafasi ya Urais miaka ya nyuma, wangefanya vizuri zaidi katika kura hii ya maoni kwasababu Watanzania wanawajua zaidi na wamekuwa wanawasikia kwa miaka mingi. Lakini tunaona hakuna aliyekubalika kwa zaidi ya asilimia 15. Hii inaonyesha kwamba licha ya kuwafahamu kwa kina viongozi hawa, licha ya ukweli kwamba baadhi yao wamekuwa kwenye kampeni kwa miaka 10 sasa, Watanzania wengi hawaamini kwamba wana sifa na uwezo wa kuwaongoza. Lakini pia inaonyesha kwamba Watanzania wanahitaji  aina mpya ya uongozi wa nchi wenye mwelekeo, fikra na mawazo mapya ndio maana wengi bado hawajafanya uamuzi.

Mimi naamini kwamba viongozi wa kizazi cha sasa, kwa kadri utaratibu utakavyoruhusu kupata fursa ya kuelezea dira na mwelekeo mpya kwa nchi yetu, kwa kadri watakavyopewa fursa na vyombo vya habari, kama ambavyo viongozi wa muda mrefu wanapata, basi Watanzania watafanya uamuzi sahihi.  

Tatu, utafiti huu unatupa fursa ya kujua nini hasa vipaumbele vya Watanzania. Wananchi wengi wameonyesha kwamba wanahitaji huduma bora za afya, elimu na maji. Wananchi wengi wameonyesha kukerwa na rushwa na hali ya umaskini. Wananchi wengi wana tatizo la ajira.  Wananchi wengi wanataka nchi yetu iendelee kuwa ya amani na utulivu na usalama na yenye watu wanaopendana na kuheshimiana. Kwa viongozi wanaowania fursa ya kuwaongoza Watanzania, haya ndio mambo ya msingi ya kuyazingatia na kueleza mikakati ya kukabiliana nayo badala ya kuonyeshana ufahari wa nani ana nafasi nzuri zaidi ya kushinda.

Nne, nafarijika kwamba Chama cha Mapinduzi bado kinaendelea kuaminiwa na Watanzania wengi licha ya muungano wa vyama vya upinzani. Kazi nzuri iliyofanywa na Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahman Kinana,  na Sekretarieti yake inaonyesha matunda. Wanastahili pongezi na kutiwa moyo ili waendelee na kazi hiyo.

January Makamba


No comments: