Kama ilivyo ada, tunaanza kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka zake na kibali chake cha kutukunanisha
siku hii ya leo.
Nawashukuru wote mliofika
hapa na nyote mnaonisikiliza kupitia luninga na redio. Nawashukuru pia wana-CCM
na Watanzania waliokusanyika katika mikoa mbalimbali ambao wataunganishwa nasi
moja moja wakati wa kipindi cha maswali na majibu.
Nimeonelea nitumie siku na
fursa hii kuwajulisha kwamba, baada ya tafakuri ya kina ya changamoto za sasa
nchi yetu na mahitaji ya uongozi wa aina mpya, nimeamua kuomba nafasi ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa ajili hiyo, keshokutwa,
nitasafiri kwenda Dodoma kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya wana-CCM ili niweze
kuteuliwa na Chama chetu kuwa mgombea kwa nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu
wa mwaka huu.
Nafanya hivyo nikitambua ukubwa
na utakatifu wa dhamana ninayoiomba.
Naiomba nafasi hii nikiwa
nimejiridhisha bila shaka yoyote kwamba ninao uwezo, ukomavu, uzalendo,
uadilifu, uzoefu, hekima, busara, maarifa na ubunifu wa kuishika nafasi ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naiomba nafasi hii nikielewa
kiu ya Watanzania ya kupata uongozi mpya, wa zama za sasa, unaotoa matumiani
mapya, yatakayozaa Tanzania mpya.
Naiomba nafasi hii nikiwa
naelewa misingi iliyoijenga nchi yetu – misingi ya haki, umoja, amani,
mshikamano na upendo miongoni mwa Watanzania – na haja ya kuilinda misingi hiyo.
Nchi yetu iko katika njia
panda. Katika miaka 10 ijayo, Tanzania inaweza kuchukua njia mojawapo kati ya
hizi mbili: inaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo na hali ya maisha ya
wananchi wote kuboreka.
Lakini vilevile, ipo hatari
ya taifa letu kupasuka kutokana na dalili za mpasuko wa kidini, mmomonyoko wa
maadili kwenye jamii, kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa dola, dalili za ufa
katika Muungano, umaskini na tofauti kubwa ya kipato baina ya wananchi.
Aina ya uongozi tutakaouchagua mwaka huu ndio
utaamua mustakabali wa nchi yetu. Baada ya miaka 50 ya uongozi wa kizazi
kilichopita, sasa ni wakati wa nchi yetu kuongozwa na viongozi wa aina mpya,
wenye mtazamo mpya, fikra mpya, maarifa mapya na majawabu mapya.
Ndugu zangu, Watanzania wenzangu,
Nimesimama hapa kuwahakikishia kwamba nimefanya tafakuri ya kina na za
muda mrefu kuhusu mwelekeo wa nchi yetu. Na niko tayari kutengeneza na kuongoza
timu madhubuti ya Watanzania wazalendo na waadilifu watakaounda Serikali itakayojenga
kesho njema.
Nimesimama hapa kuwakaribisha wana-CCM
wenzangu na Watanzania wote kwenye kampeni hii. Tunayo dhamira na uwezo wa
kushinda na kuongoza mabadiliko makubwa ambayo Watanzania wanayatarajia.
Kwa mambo niliyoyaona na
kujifunza kuanzia kufanya kazi na Rais Kikwete Ikulu, kwenye uongozi wa Chama,
Bungeni na Serikalini, nimepata matayarisho ya kutosha ya kuiongoza nchi yetu.
Naiomba nafasi hii nikiwa
naijua vyema sana nchi yetu, nikiwa nayajua kwa kina matatizo ya Watanzania
katika kila kona ya nchi yetu, na nikiwa nimejiridhisha kwamba ninao ubunifu na
maarifa ya kutosha ya kutafuta majawabu mapya kwa ajili ya kuinua hali za
maisha za Watanzania.
Siko mbele yenu kuwasimulia
kuhusu matatizo ya nchi yetu ambayo sote tunayajua. Niko mbele yenu kuelezea
namna tukavyotatua matatizo ya nchi yetu. Katika kuomba nafasi hii nimefikiria
na nitaelezea baadhi ya majawabu mapya ambayo yananitofuatisha mimi na wengine
wanaoomba nafasi hii.
Natambua kwamba nikiteuliwa
na Chama changu, nitakabidhiwa Ilani ya Uchaguzi itakayoelekeza mambo ya
kufanywa na Serikali ijayo. Nitainadi Ilani hiyo na kuitekeleza kwa nguvu zangu
zote.
Hata hivyo, kama wasemavyo
waswahili, ziada njema haigombi. Kuwepo kwa Ilani hakuzuii kuwa na mambo ya
ziada ya msingi kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Kwa msingi huo, nianze kwa
kusema kwamba Serikali nitakayounda itaendeshwa na falsafa ya uwezeshaji mpana
wa wananchi – kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Kwa miaka mingi sasa,
Watanzania wamepewa ahadi nyingi na viongozi wa siasa. Badala ya kuwaahidi wananchi
kwamba tutawafanyia kila kitu, Serikali nitakayoiunda itawajengea uwezo na
nguvu ya maamuzi kuhusu maisha yao. Serikali yangu itajikita katika kuwajengea
nguvu ya kiuchumi ya kuendesha maisha yao, na kuamua waishi wapi, wapeleke
watoto shule wapi, waanzishe biashara gani, wajenge nyumba za aina gani, wakatibiwe
wapi.
Tutawajengea uwezo wa kuwa na
sauti katika maamuzi ya Serikali yao. Tutaondokana na dhana ya wananchi kubaki
watazamaji tu katika masuala ya nchi yao.
Sitaunda Serikali ya waporaji
na wabinafsi. Nitaunda Serikali yenye utu na inayowasikiliza na kuwajali watu. Serikali
inayotimiza wajibu wake bila chembe ya uzembe wala ulegevu. Nitaunda Serikali
yenye Mawaziri wasiozidi 18 ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa
shaka kuhusu uwezo na uadilifu wake.
Serikali yetu itakuwa na
vipaumbele vikubwa vitano:
Kwanza ni kukuza kipato cha
watu. Msingi wa maendeleo ya nchi yetu sio mapato ya Serikali, bali ukubwa na
uhakika wa kipato cha Watanzania. Kama nilivyosema awali, nitataka Watanzania
tuwe na nguvu na uwezo wa kiuchumi wa kuendesha maisha yetu.
Kwahiyo, kwa wale wenye
shughuli za kufanya – iwe ni kilimo, uvuvi, ufugaji au biashara – tutaweka
mazingira ya kisera, kisheria na kikodi ili shughuli hizo zipanuke, zishamiri,
ziwe na faida kwao na ziwanufaishe katika maisha yao.
Falsafa yetu ni kwamba mtu
yoyote anayetoa jasho kutengeneza maisha yake na ya familia yake, ni lazima
anufaike na juhudi na jasho lake. Kwa wale wasio na shughuli za kipato,
tutafanya jitihada zote ili wawe na shughuli za kiuchumi za kufanya. Tutatengeneza
fursa za kiuchumi ili mtu yoyote kama hana shughuli ya kufanya basi awe ameamua
mwenyewe. Maendeleo ya nchi yatapatikana kwa nguvu ya uchumi ya wananchi, sio
kwa hisani ya wafadhili.
Kipaumbele cha pili kitakuwa
ni kupatikana kwa huduma bora za jamii na kiuchumi. Kazi kubwa imefanywa na
viongozi waliotangulia, lakini bado Watanzania wengi wanahitaji kupata huduma
ya uhakika ya maji, afya, elimu bora, barabara za uhakika, umeme, huduma za
fedha na mawasiliano. Tutabuni mbinu
mpya za kumaliza matatizo haya.
Kipaumbele cha tatu ni
utawala bora, wa haki na wa sheria. Msingi wa amani ya nchi yetu ni haki.
Wananchi wengi hawana uhakika wa kupata haki zao waendapo polisi au mahakamani.
Serikali yangu italibadilisha hili. Tutazijenga upya taasisi ya usimamizi wa
utawala na haki za watu, zikiwemo mahakama na jeshi la polisi.
Hatutakubali Mtanzania yoyote
aonewe na watu au mamlaka za umma. Lakini pia tutataka kila mtu afuate sheria
za nchi, hata ziwe ndogo kiasi gani.
Tutakabiliana na tatizo la
ubadhirifu wa mali ya umma kwa nguvu zote. Nampongeza Rais Kikwete kwa kufanya
jambo la kimapinduzi la kuelekeza Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) ziwekwe hadharani na kujadiliwa.
Serikali yangu itaenda mbele zaidi
na kuhakikisha kwamba ripoti ya CAG ikitolewa, viongozi ambao taasisi zao
zimekutwa na makosa wanakaa pembeni siku hiyo hiyo na hatua za kisheria, za kipolisi,
za kimahakama zinaanza siku inayofuatia.
Kipaumbele cha nne ni
usimamizi wa uchumi. Serikali yangu taimarisha uwezo wa taasisi za usimamizi wa
uchumi – ikiwemo Wizara ya Fedha, Tume ya Mipango, Benki Kuu na Mamlaka ya
Mapato. Nitazipa mamlaka na rasilimali-watu ili ziweze kudhibiti mfumuko wa
bei, kuporomoka kwa thamani ya shilingi, nakisi ya bajeti, kupungua kwa hifadhi
ya fedha za kigeni, kukua kwa deni la taifa na kusimamia uwekezaji wa kimkakati
wa sekta binafsi.
Kama ambavyo tuna Baraza la
Usalama wa Taifa sasa, nitaunda Baraza la Uchumi la Taifa litakalojumuisha
wataalam kutoka katika taasisi za umma za usimamizi wa uchumi, wagwiji wa
uchumi kwenye nchi yetu, pamoja na wawakilishi wa sekta binafsi.
Baraza hili litakuwa na
jukumu la kuhakikisha kwamba uchumi wetu unawekewa mikakati ya muda mrefu na wakati
wote hali ya uchumi wetu inaratibiwa kwa weledi na changamoto zinazojitokeza
zinarekebishwa haraka.
Kipaumbele cha tano ni amani,
umoja na usalama wa mali na maisha ya Watanzania. Amani na umoja wa nchi yetu
ni tunu na urithi tulioachiwa na waasisi wa nchi yetu. Marais wote waliopita
wamefanya kazi kubwa ya kuzilinda tunu hizi. Serikali yangu haitakubali urithi
huu upotee. Tutafanya jitihada zote ili kujenga maridhiano mapya na upendo
miongoni mwa makundi mbalimbali katika jamii yetu. Nitawahusisha viongozi wa
dini zote katika hili. Nitaanzisha Jukwaa la Rais na Baraza la Maaskofu
Tanzania (TEC), Jumuiya ya Wakristo Tanzania (CCT) na Baraza la Waislam
Tanzania (BAKWATA) litakalokutana kila miezi miwili kujadili na kupanga mikakati
ya kuendeleza amani, umoja, upendo na maadili ya jamii.
Pia tutachukua hatua mpya za
kuimarisha Muungano wetu na kuupatia uhalali mpya na wa ziada miongoni mwa
Watanzania.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Naomba sasa nifafanue
majawabu mapya ambayo Serikali yangu itayatekeleza kwa changamoto mahsusi:
Naomba nianze na suala la ajira. Kwasasa,
wapo zaidi ya Watanzania milioni 23 kwenye soko la ajira leo hii. Kila mwaka
wanaongezeka vijana zaidi ya laki tisa kwenye soko la ajira.
Hawa ni watu wengi sana. Viongozi wengi wa
siasa wameliita tatizo la ajira kuwa ni bomu. Lakini kulielezea tatizo sio
kulitatua.
Serikali yangu itafanya nini?
Watanzania wengi wanajishughulisha na
biashara ndogo na za kati. Karibu zote zinaajiri mtu mmoja au wawili na nyingi
zinasuasua. Watalaamu wanatuambia,
asilimia 20 tu ya biashara na kampuni ndogo nchini zikiongeza mfanyakazi mmoja
kwa mwaka, ajira 400,000 za kudumu zitazalishwa kwa mwaka. Je asilimia 80 za
biashara hizi zikiongeza watu wawili wawili tu kwa mwaka? Tutakuwa tumepunguza
sana kama sio kumaliza tatizo la ajira.
Kwahiyo, jawabu letu la kwanza litakuwa ni
maendeleo ya biashara ndogo na za kati. Zilizopo zifanye vizuri na kuongeza
waajiriwa na wale wanaotaka kuanzisha biashara, iwe rahisi kufanya hivyo.
Ziko namna kadhaa za kufanya hivi. Kwa mfano,
katika nchi yetu, Serikali bado ndio mnunuzi mkuu. KIla siku, Serikali yetu
inanunua bidhaa nyingi - kuanzia kuni, karatasi, matofali, mabati, vyakula na
huduma nyingine nyingi. Katika kuzijengea uwezo kampuni ndogo na za kati,
Serikali yangu itaweka Sheria ya kuwezesha asilimia 30 ya thamani ya manunuzi
ya umma kupewa makampuni madogo na ya kati yatakayokidhi vigezo rahisi
yanayomilikiwa na vijana na wanawake. Jambo hili litawezesha biashara nyingi
ndogo kujenga uwezo, kupanuka na kuajiri watu wengi zaidi.
Lakini, ili hili litokee, lazima tuwe na
taasisi madhubuti ambayo itashughulika na ustawi wa biashara na makampuni
madogo na ya kati.
Kwahiyo, nitaanzisha Mamlaka mahsusi ya
Maendeleo ya Biashara Ndogo na za Kati. Pamoja na mambo mengine, Mamlaka hii itapewa majukumu ya kuwezesha, kurahisisha
na kusimamia biashara ndogo kuanzishwa kwa urahisi, kuendeshwa bila bughudha,
na kupata fursa ya kukua.
Ndugu Wananchi,
Viwanda bado ni tegemeo kubwa la
ajira. Kwa viwanda vikubwa
vilivyopo sasa, tutaweka motisha ya kikodi kwa yoyote ambaye ataweza kuongeza
ajira mpya angalau 500 au zaidi za
kudumu kwa mwaka. Haipaswi kumgharimu kikodi mtu mwenye biashara kuongeza
wafanyakazi.
Kwa waajiri ambao ni biashara au kampuni mpya
ndogo na za kati, yaani SMEs, Serikali yangu itatoa motisha ya kupunguziwa kodi
hizi kwa kila kazi mpya tano au zaidi kwa mwaka. Ukweli hapa ni kwamba kunawiri kwa uchumi hakutokani na kodi
inayokusanywa na Serikali bali kunatokana na kipato na uwezo wa manunuzi
walionao wananchi na kipato cha wafanyabiashara kuweza kukuza biashara zao na
kutoa ajira nyingi zaidi.
Vilevile, katika
kukabiliana na tatizo hili la ajira, tutawezesha sekta binafsi kujenga
na kufufua viwanda vya nguo, katani na korosho nchini. Huko nyuma tulishawahi
kuwa na viwanda vingi vya aina hii, vikichangia asilimia 25 ya pato la Taifa na
kuajiri asilimia 25 ya wafanyakazi wote nchini. Kwa sasa, ni asilimia 30 tu ya
pamba yetu ndio inayotumika nchini. Pamba tunayo ya kutosha kukidhi mahitaji ya
viwanda vikubwa zaidi ya hamsini. Ndani ya miaka mitano ijayo tutahakikisha
tunajenga na kufufua viwanda 11 vya nguo vitakavyotoa ajira mpya zaidi 100,000 viwandani tu, huku asilimia zaidi ya 80 ya
wafanyakazi hawa wakiwa ni wanawake. Lengo ni sekta nzima ya pamba kuajiri
walau asilimia 10 ya nguvu kazi (kazi
milioni 2.5).
Katika kuwezesha hili, Serikali nitakayoiongoza
itachukua hatua za muda mfupi za kikodi na kiushuru ili kuwezesha viwanda hivi
kukabiliana na ushindani wa kanga, vitenge, mitumba na vitambaa kutoka nje ya
nchi.
Ndugu wananchi,
Shughuli za ujenzi wa nyumba na
miundombinu huongeza chachu katika uchumi na kuongeza ajira nyingi sana. Tuna
mahitaji makubwa ya nyumba na tuna mahitaji makubwa ya ajira. Nitahakikisha
tunatengeneza mazingira mazuri ya uanzishwaji na uimarishaji wa makampuni
madogo na ya kati yanayojihusisha na biashara katika sekta ya nyumba. Tutahakikisha
kwamba, ndani ya miaka kumi ya uongozi wangu, sekta ya ujenzi inachangia zaidi
ya asilimia 25 ya Pato la Taifa na kuajiri zaidi za watanzania milioni 5. Hii
itawezekana kwa kupunguza gharama za ujenzi. Na hili litawezekana kwa uwekezaji
kwenye viwanda vya vifaa ya ujenzi, kama vile viwanda vya nondo, mabati,
simenti, vigae na vioo.
Hii itaenda pamoja na ujenzi wa miundombinu
mikubwa, hasa ya usafirishaji. Tutaweka jitihada za makusudi kuongeza kasi na
ukubwa wa miradi ya miundombinu nchini ambayo itaajiri watanzania wengi zaidi
na kuingiza fedha nyingi zaidi kwenye mzunguko wa uchumi. Tutahakikisha kwamba
wakandarasi wa miradi hii ni makampuni ya ndani yatakayohifadhi na kuwekeza
fedha hizo hapa ndani. Lengo langu ni kuwezesha wakandarasi wa ndani kiufundi,
kiutawala na kifedha na kuwawezesha kupata walau
asilimia 80 ya miradi yote ya miundombinu inayojengwa kwa fedha za umma
ndani ya miaka kumi ijayo.
Shughuli
za sanaa na michezo zikisimamiwa vizuri zina uwezo wa kuajiri asilimia kubwa ya
watanzania. Mapema kabisa kwenye
serikali yetu tutarasimisha shughuli za sanaa ikiwemo sinema, muziki na
kazi zote za ubunifu. Tutatunga Sheria kali zaidi kulinda hakimiliki. Kupitia
Mfuko wa Sanaa wa Taifa tutakaouunda upya, tutatoa ruzuku na mikopo ya masharti
nafuu kwa wazalishaji, waendeshaji na wasanii wenyewe kwenye kuendeleza ubunifu
na kuzalisha, kutangaza na kuuza kazi mpya kwa njia za kisasa. Tukiweza kuongeza
maradufu uwekezaji kwenye tasnia ya sanaa na ubunifu hapa nchini, tutatengeneza
ajira mpya zaidi ya milioni mbili.
Sita, kwa vijana wasomi na wanataaluma ambao hawatakuwa
wamebahatika kupata ajira katika sekta rasmi, tutawawekea utaratibu wajiunge na
kuanzisha makampuni na biashara za kitaaluma – wahandisi, wanasheria, wasomi
katika fani za siasa na utawala, na wengineo – na tutawapa mikopo maalum ya
kufanya hivyo.
Kwa upande wa wamachinga, naelewa kwamba wanazunguka kutwa nzima
wakiuza bidhaa ambazo hawazimiliki na huishia kupata pesa ya kula tu au nauli
au hawapati kitu kabisa. Viongozi
nitakaowateua kuongoza Mamlaka mpya ya Biashara Ndogo na Za Kati katika mwaka
wao wa kwanza watapimwa kwa uwezo wao wa kuhakikisha wamachinga wana sehemu
salama na zenye wateja za kufanyia shughuli zao na hawaishii kuwa fremu tu
barabarani kwa mali za watu wengine.
Jambo jingine kubwa tutakalofanya ni kutoa shilingi milioni 50 kwa
kila kijiji hapa nchini katika miaka mitano kwa ajili ya wanavijiji kukopeshana
kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali. Mfuko huu utaendeshwa na Kamati
maalum zitakazoundwa na wanavijiji wenyewe na wao ndio watakaomua nani
akopeshwe na arudishe baada ya muda gani. Mzunguko wa shilingi milioni 50
kwenye shughuli za uzalishaji mali kijijini utatoa chachu ya maendeleo ya watu.
Fedha zinazohitajika hazifiki bilioni 700 katika miaka mitano. Kwa sasa
tunakusanya zaidi ya bilioni 800 kwa mwezi. Fedha hizi tutazipata na nitaelezea
ni. Utaratibu wa aina hii umebadilisha maisha ya wananchi wa vijijini huko
nchini Thailand.
Kilimo bado ndio nguzo ya ajira
kwa Watanzania wengi. Mambo mengi yamezungumzwa kuhusu mapinduzi ya kilimo kwa
miaka mingi. Kila zao linalolimwa nchini – iwe ni pamba, korosho, chai, kahawa,
tumbaku, mkonge, au mboga na matunda – lina changamoto zake mahsusi. Serikali
yangu itabadilisha namna ya kushughulikia maendeleo ya kilimo kwa kuweka
mkakati ya zao moja moja tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna mikakati ya jumla
ya kilimo. Tutabadilisha utaratibu wa
sasa wa upatikanaji wa pembejeo ambapo pesa nyingi zinapotea kwa watu wa kati
huku wakulima wakiwa hawapati pembejeo za kutosha, kwa wakati na kwa bei wanayoimudu.
Tutaweka mkazo kwenye kurekebisha mfumo wa ununuzi wa mazao ambao kwasasa
unamkandamiza mkulima. Tutaanzisha Soko Kuu la Kitaifa la Mazao, yaani
Commodities Exchange, litakalowezesha wakulima kuwa na nguvu ya kujua na kuamua
bei na wakati wa kuuza mazao yao.
Kwenye uvuvi na ufugaji, mipango
iliyopo inatosheleza. Tutakachokifanya na kuitekeleza kwa haraka na uhakika.
Kwa maeneo ya uvuvi, tutaanzisha mifuko ya kuwawezesha wavuvi kukopeshwa nyavu,
boti na mashine na majokofu ili waweze kwenda mbali majini na kuhifadhi samaki kwa
muda mrefu ili wapate soko zuri na bei nzuri. Hatutaacha wafugaji wakose
malisho ya mifugo yao. Kila mfugaji atamilikishwa eneo ya malisho na kupewa
hati. Hii itasaidia kumaliza migogoro kati yao na wakulima.
Ndugu wananchi,
Jambo jingine ambalo ningependa kuliongelea ni suala la elimu. Ni lazima
kukiri kwamba, pamoja na changamoto zilizopo, mafanikio makubwa yamepatikana
kwenye Serikali ya Rais Kikwete kwenye nyanja ya elimu, hasa kwenye udahili wa
wanafunzi kwa ngazi zote. Pamoja na mafanikio haya, changamoto za elimu zipo
lukuki na ndugu zangu Watanzania mnazijua. Sasa nini kifanyike kuboresha elimu?
Katika serikali yetu, tutatekeleza yafuatayo.
Kwanza, Serikali yangu itaondoa shaka
na kumaliza kabisa mjadala kuhusu dira ya elimu yetu. Tutaongozwa na dira ya
elimu inayochochea vijana kujiajiri, inayochochea udadisi, inayochochea
ubunifu, inayochochea uthubutu, nidhamu, weledi na uzalendo. Tutatengeneza
mitaala mipya na thabiti kabisa inayokidhi mahitaji ya mazingira na changamoto
za sasa na mahitaji ya uchumi wa kisasa, mahitaji ya jamii na mahitaji ya taifa
kwa ujumla. Hiyo ndio itakuwa mihimili ya elimu tutakayowafundisha watoto wetu
chini ya uongozi wangu.
Tutawafundisha watoto wetu kwa lugha zote mbili, ya Kiswahili na
Kiingereza kwasababu ni jambo linalowezekana.
Rais Kikwete amefanya kazi kubwa katika kukabiliana na tatizo la
uhaba wa walimu. Bado changamoto ipo kwenye walimu wa sayansi na hisabati. Tutaongeza
udahili kwenye vyuo vya ualimu vinavyofundisha masomo hayo ili kupata walimu
wengi zaidi.
Kama saikolojia ya mwalimu haijakaa
sawa kutokana na changamoto nyingi, tusahau kuhusu ubora wa elimu. Tunasema
ualimu ni wito lakini haipaswi kuwa adhabu. Tutazitatua changamoto za
walimu, ikiwemo mazingira yao ya kazi, motisha na hamasa yao ya kufundisha
ikiwemo mishahara yao, kupandishwa madaraja, mafunzo yao ya ziada ya
kujiendeleza.
Tutaweka vipimo vipya ya maendeleo ya elimu nchini kwa kupima uelewa na maarifa
ya wanafunzi kwa mambo wanayopaswa kuyajua katika ngazi husika ya elimu.
Hatutaishia tu kusheherekea ufaulu wa jumla katika mitihani ya mwisho. Pia, tutaweka
mfumo wa motisha ya malipo au kupandishwa vyeo kwa walimu wetu wa shule za
Serikali wanaofanya vizuri
Vilevile, hatutaingiza siasa kwenye
maendeleo ya elimu. Tutaweka uongozi thabiti na wa kizalendo kwenye sekta ya
elimu utakaokabiliana na changamoto za uendeshaji na utawala wa sekta ya
elimu, ikiwemo masuala ya ukaguzi, usimamizi wa walimu, uidhinishaji na
usambazaji vitabu kwenye mashule, upelekaji na matumizi ya fedha za uendeshaji
wa shule na mambo mengineyo.
Ili kuchukua vijana wengi wanaoishia darasa la saba na kidato cha
nne, tutajenga Chuo kikubwa cha ufundi kwenye kila Wilaya ya nchi yetu kwa
kushirikiana na sekta binafsi.
Kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Serikali yangu
itabadilisha utaratibu na kuweka utaratibu mpya, wa wazi na wa haki ili kila
anayestahili mkopo apate na apate kwa kiwango kinachotosheleza. Tutaanzisha
Mfuko Maalum, yaani National Education Endowment Fund, kwa ajili ya kugharamia
elimu ya juu kwa wenye mahitaji maalum. Serikali pia itaweka dhamana ya mikopo
wanafunzi katika taasisi binafsi zitakazokuwa tayari kukopesha wanafunzi. Zaidi
ya hapo, tutaanza utaratibu wa kuviwezesha vyuo na taasisi za elimu ya juu viwe
na mifuko kwa ajili ya kutoa mikopo na misaada kwa wanafunzi.
Jambo jingine kubwa ambalo ningependa kulizungumzia ni tatizo la
rushwa. Limezungumzwa na wengi. Lakini kulizungumzia
na kulipigia kelele suala la rushwa pekee hakulimalizi. Ziko namna mbili tutakazozitumia
kukabiliana na hili tatizo: njia ya kwanza ni kisheria, kimfumo na kitaasisi;
njia ya pili ni kijamii.
Kuhusu kimfumo, nitafanya mabadiliko makubwa mawili. Kwanza, ni kuiwezesha TAKUKURU kuwa
na mamlaka kisheria ya kuwashitaki watuhumiwa wa rushwa moja kwa moja
mahakamani. Pia, tuanzishe Mahakama Maalum ya Uhujumu Uchumi ambayo itahusika
na makosa ya rushwa; ubadhirifu wa mali ya umma; ukwepaji kodi; kuiba,
kunufaika au kutaka kuiba au kutaka kunufaika na mali ya umma; na makosa
mengine ya aina hii.
Mahakama ambayo
itakuwa na jopo maalum la majaji ambalo litafanya kazi mwaka mzima na
kusikiliza na kuhukumu kesi hizi haraka. Kesi za uhujumu uchumi ziendeshwe wazi
na mfululizo na adhabu ziwe kali sana, kwa mfano ya kifungo cha maisha. Pia tutaanzisha
Kurugenzi ya Uchunguzi na Mashtaka ya Uhujumu Uchumi. Tutaiwezesha Mahakama hii
na Kurugenzi hii bila ukomo wa kirasilimali kuifanya kazi hii vizuri.
Kuhusu kijamii, kwa
kushirikiana na viongozi wa dini na wengine wa kijamii, nitaanzisha na
kuwezesha mjadala mpana kwenye jamii yetu kuhusu maadili ya jamii. Jamii yetu ijengwe kwenye misingi
ya kuchukia rushwa, ulaghai na njia za mkato za kupata mali. Inapofika mahala
jamii inasheherekea mali ambazo hazina maelezo, inapofika mahali ambapo jamii
inawatukuza wachache ambao wametumia ujanja kufanikiwa, inapofika mahala ambapo
jamii inakuita mjinga unapostaafu ukiwa hujilimbikizia mali, hapo lipo tatizo
ndani ya jamii. Lazima kujenga jamii tofauti, ambayo wala rushwa wanajiona kama
wanatembea uchi, jamii ambayo inatoa adhabu za kijamii, yaani social sanctions,
ikiwemo kutengwa, ambazo ni kali kuliko adhabu za kisheria. Mwalimu Nyerere
alijaribu kujenga jamii ya aina hii: jamii ambayo kiongozi wa umma hapaswi
kungoja mahakama itamke kwamba ni mla rushwa. Tunapaswa kuendelea kujenga jamii
ya aina hii. Viongozi wa dini wana nafasi kubwa. Maadili na malezi na makuzi
kwenye familia pia yana nafasi yake.
Ndugu zangu Watanzania, bila kudhibiti rushwa na wizi hatuwezi kupata
maendeleo. Kwa hiyo, kwa kiongozi yoyote, kama anataka kuacha rekodi nzuri ya
maendeleo, kuitokomeza rushwa ni jambo la kufa na kupona.
Katika uchaguzi
huu, tunayo fursa ya kuanza safari ya kumaliza tatizo hili. Rekodi ya uadilifu
sio sifa pekee ya uongozi. Lakini pia sio jambo la kupuuzwa hata kidogo. Namna
viongozi wanavyotafuta uongozi ndio namna watakavyotawala. Tunayo fursa ya
kuchagua viongozi ambao hawatapata kigugumizi kupambana na rushwa. Tunayo fursa
ya kuchagua viongozi ambao hawatakuwa na madeni ya kulipa. Sina shaka kabisa
kwamba mimi ni kiongozi wa aina hiyo.
Ndugu wananchi,
Napenda pia
kuzungumzia suala la ardhi. Hili pia ni
muhimu kwasababu mbili: kwanza, ardhi, kwa maana ya
umiliki na matumizi yake, ndio msingi wa yote; na pili, zimeanza kuonekana
dalili ya watu wachache kuhodhi ardhi kubwa na kuanza kuirudisha nchi yetu
kwenye zama za ukabaila. Hakuna
maendeleo ya kilimo kama hakuna uhakika wa matumizi bora ya ardhi na kama
hakuna uhakika wa mfumo wa umiliki wa ardhi.
Lazima sasa kuondoa migogoro ya ardhi isiyoisha kati ya wakulima, wafugaji, wawekezaji na Serikali na kuipa ardhi
thamani halisi inayostahili. Kama tunavyobainisha
kisheria na kulinda hifadhi za misitu na mbuga za wanyama lazima maeneo ya
kilimo na mifugo na makazi ya watu nayo yawe hivyo. Lazima wakulima wamiliki
ardhi yao kisheria. Lazima kutenga maeneo maalumu ya wafugaji yanayomilikiwa na
wafugaji kisheria na bila kusahau korido mahususi za kupitisha mifugo kutoka
upande mmoja wa nchi mpaka mwingine.
Serikali
yetu itatumia teknolojia mpya ya satellite katika kupima na kupanga matumizi ya
ardhi nchini. Tutajenga kituo cha kupokea picha za satellite ambacho
kitawezesha kila kipande cha ardhi katika nchi yetu kupimwa, na hati ya
umiliki, yenye picha na mipaka isiyo na shaka, kutolewa na matumizi ya ardhi
hiyo kujulikana. Kituo hiki hakigharimu fedha ambazo tunazishindwa.
Kuhusu huduma ya afya,
Watanzania wengi, hasa wa vijijini, bado wana changamoto kubwa kuipata. Kazi
nzuri imefanywa na Serikali ya Rais Kikwete kusogeza huduma hii karibu na
wananchi na kuiboresha. Kazi hiyo tutaiendeleza. Tutaitazama huduma ya afya
kimfumo zaidi na kurekebisha uendeshaji wake.
Lakini kubwa tutakalofanya ni
kuhakikisha kwamba kila Mtanzania ana bima ya afya na anapata matibabu bila
kujali uwezo wa kipato chake. Moja ya namna ya kufanya hili ni kutengeneza
Sheria mpya ya kuiunganisha mifuko yote ya Bima na kurahisisha ukusanyaji na
matumizi ya pesa kwenye vituo vya afya ya msingi. Nchi nyingine za Afrika
wamefanya hivi na kufanikiwa. Na sisi hatuwezi kushindwa. Tutaondoa ukiritimba na urasimu wa Bohari ya
Madawa ya Taifa katika kusambaza madawa katika vituo vya huduma vya Serikali.
Kwa
wananchi wa Tanzania, ukiwauliza leo ni huduma ipi ya jamii bado ni kero kubwa.
Jibu litakuwa ni huduma ya maji. Watanzania wanaopata huduma hii hawafiki
asilimia 60. Maeneo ya vijijini hali ni mbaya zaidi. Ni jambo la kawaida kwa
kina mama vijijini kutumia siku nzima na kwenda umbali mrefu kupata nusu ndoo
kwa familia nzima. Tatizo kubwa ni uwekezaji mdogo katika sekta ya maji. Ili
kukabiliana na tatizo hili, tutaanzisha Mfuko wa Maji Vijijini pamoja na Wakala
wa Maji Vijijini. Tumeona jinsi Mfuko wa Barabara na Wakala wa Barabara wa
Taifa unavyofanya kazi nzuri kwenye ujenzi wa barabara. Tumeona jinsi ambavyo
Mfuko wa Umeme Vijijini na Wakala wa Umeme Vijijini ulivyofanya kazi nzuri
kusambaza umeme vijijini. Tumeweza kufanya kazi nzuri ya barabara na umeme kwa
kutumia fedha zetu wenyewe.
Utaratibu
mpya na msukumo mpya wa kupeleka maji vijijini utasaidia. Chanzo cha fedha kwa
Mfuko wa Maji kinaweza kuwa tozo maalum ndogo kwenye matumizi ya maji mijini na
maji ya kunywa kwenye chupa. Nina uhakika
kabisa kuwa ndani ya miaka kumi tunaweza kusogeza maji safi, salama na ya
uhakika karibu kabisa na kaya zote nchini kote.
Nataka sasa niongelee kuhusu
miundombinu. Suala hili lazima tulipe umuhimu wa kipekee. Uchumi wa nchi unaendeshwa na miundombinu ya
usafirishaji. Rais Kikwete amefanya kazi kubwa, hasa kwenye miundombinu ya
barabara. Na naamini kwamba kabla hajamaliza muda wake ataweka jiwe la msingi
la ujenzi wa reli ya kati. Kazi hii nzuri tutaiendeleza lakini tutaifanya kwa
kazi zaidi na maarifa mapya. Barabara ambazo hazijaisha tutazimalizia na
tutaanza nyingine mpya. Tutahusisha sekta binafsi katika ujenzi wa reli za
kutoka Mtwara hadi Mchuchuma hadi Mbamba Bay. Pia tutafufua reli ya Tanga hadi Arusha
na kuisogeza hadi Musoma. Bandari ya Mtwara itakuwa bandari kubwa ya uchumi wa
gesi na chuma kutoka Liganga na makaa ya m awe kutoka Mchuchuma. Nimebahatika
kufika kwenye bandari za Kemondo Bay, Mwanza, Nansio na Musoma kwenye Ziwa
Victoria; bandari za Kigoma na Kasanga kwenye Ziwa Tanganyika; na bandari za
Itungi, Manda, Liuli na Mbamba Bay kwenye Ziwa Nyasa. Hizo zote ni bandari za
uchumi na zinahitaji matengenezo mapya makubwa. Kazi hii tutaifanya. Bandari ya
Mwambani ambayo imeahidiwa kwa miaka mingi nayo tutaanza kuijenga kwa
kushirikisha sekta binafsi.
Ndugu wananchi,
Nimezungumzia mambo mengi na
mabadiliko makubwa ambayo tutayatekeleza. Ni dhahiri kwamba baadhi ya haya
mambo yatahitaji rasilimali-fedha za Serikali kuyafanya. Kwa hakika hatuwezi
kufanya mambo yote haya bila uwezo wa Serikali kuongezeka na uchumi kupanuka.
Kiongozi makini hawezi
kuzungumzia mambo yote haya bila kuzungumzia rasilimali za kuyatekeleza. Tofauti
na wenzangu, nataka niwahakikishie
kwamba ninazo fikra za namna ya kupata fedha za kufanya yote niliyoyazungumzia.
Kwanza, tutaihusisha sekta
binafsi kwa kina zaidi kutekeleza ile miradi ambayo ni ya kimaendeleo lakini
pia ni ya kibiashara ambapo Serikali haina ulazima kutumia fedha zake.
Kwa upande wa uwezo wa
Serikali, nimefanya utafiti wa kina kupitia taarifa za Serikali, ripoti za Bunge
na sekta binafsi kuhusu kuongeza uwezo wa Serikali kutimiza majukumu niliyoyaainisha.
Serikali nitakayounda itafanya yafuatayo: (napenda kwa wale wenye calculator kwenye
simu zao tupige hesabu kwa pamoja hapa)
Kwanza, bila kusita wala
kuchelewa, nitapunguza misamaha ya kodi na kufikia kiwango cha asilimia 1 ya
Pato la Taifa. Hatua hii itaiwezesha Serikali kupata zaidi ya shilingi bilioni
780 kwa mwaka.
Ili kuwaingiza walipa kodi
wengi wapya, hasa kutoka sekta isiyo rasmi, Serikali yangu itapunguza kiwango
cha mapato kwa mwaka kwa walipa kodi wadogo wanaolipa kodi kwa mtindo wa
ukadiriaji. Hakuna mfanyabiashara atakayetozwa kodi kabla hajatengeneza faida.
Lakini pia tutaweka adhabu kubwa kwa wataoshindwa kulipa kodi. Tutakamilisha
vitambulisho vya taifa na anuani za makazi ili kuweza kuwatambua watu wote
wanaofanya biashara na kuwatoza kodi. Hatua hizi itawezesha Serikali kupata
fedha za ziada zaidi ya shilingi bilioni 860 kwa mwaka.
Tutaongeza ufanisi wa Mamlaka
ya Kodi Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa za Kamati ya Spika Kuhusu Mapato na
Matumizi Serikalini, TRA ikiongeza ufanisi kwa asilimia 10 tu, Serikali itapata
mapato ya ziada ya shilingi bilioni 620 kwa mwaka. Kazi hiyo tutaifanya kwani
sio ngumu. Na fedha hizo tutazipata.
Tutakapokamilisha mradi
mkubwa wa kufua chuma wa Liganga, ifikapo mwaka 2020, Serikali itapata mapato
ya shilingi bilioni 960. Tutakapokamilisha mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma,
Serikali itaweza kupata zaidi ya shilingi bilioni 800.
Tutahakikisha kwamba ardhi
yote inapimwa na kila mwenye ardhi anayo hati na anatozwa kodi stahiki. Hatua
hii itaiwezesha Serikali kupata zaidi ya shilingi bilioni 520.
Tukiwekeza kiasi kidogo cha
fedha kwenye sekta ya nyuki na kudhibiti uvunaji na biashara haramu ya
rasilimali za misitu, tutaweza kupata fedha za ziada zaidi ya shilingi bilioni
130.
Meli nyingi za kigeni zinavua
samaki katika eneo letu bila kutozwa mrahaba, wala kukaguliwa, wala kutozwa
faini. Tutarekebisha Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu na kuimarisha Mamlaka ya
Uvuvi wa Bahari Kuu ili kuwezesha haya kufanyika. Hatua hii itaipatia Serikali
mapato ya ziada ya zaidi ya shilingi bilioni 350.
Tutadhibiti biashara ya
madini ya vito na kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya kazi kwa pamoja
na urahisi na Mamlaka ya Ukaguzi wa Madini ili kuhakiki taarifa za mapato ya
madini. Hatua hii itaiongezea Serikali mapato ya ziada ya zaidi ya shilingi
bilioni 520.
Tutadhibiti uvujaji wa mapato
yanayokusanywa katika ngazi za Halmashauri. Hatua hii itaweza kutupatia kipato
cha zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka.
Sekta ya utalii kwa sasa inatuingizia
shilingi karibu trilioni 3 kwa mwaka. Kwa mujibu wa taarifa ya kina ya Benki ya
Dunia, ndani ya miaka kumi, sekta hii inaweza kuingiza shilingi trilioni 30 kwa
mwaka. Ili tuzipate fedha hizo tunapaswa kufanya mambo manne yaliyo ndani ya
uwezo wetu. Kwanza, kufungua, kuwekeza na kutangaza ukanda wa utalii wa kusini
mwa Tanzania; pili, kuongeza aina na idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania na
kuainisha vivutio vipya na mbadala na kuvitangaza. Tatu, kudhibiti mfumo wa
kukusanya mapato ya utalii, ambayo mengi yanapotelea kwa wajanja wachache nchi
au yanalipwa nje ya nchi kwa makampuni ya kitalii ya nje. Mambo haya
tunayaweza, na tutayafanya ili tufikie lengo la mapato ya shilingi trilioni 30
kwa mwaka ili tuweze kufanya kazi kubwa tulizozianisha.
Pia, serikali ina mali na
hisa kwenye biashara mbalimbali ambazo thamani yake ni zaidi ya shilingi
trilioni 10. Tutaweka utaratibu mzuri zaidi kwa kufanya mabadiliko makubwa
kwenye ofisi ya Msajili wa Hazina ili tunufaike na mali na hisa hizi. Pia, ndani
ya miaka mitano, kwa hatua mbalimbali, tutayaingiza makampuni makuu manne ya
Serikali kwenye masoko ya hisa – Shirika la Nyumba la Taifa, Shirika la Petroli
Tanzania, Shirika la Reli la Taifa, Kampuni ya Simu ya Taifa na Shirika la
Bandari Tanzania. Hatua hii itawezesha Watanzania kumiliki sehemu muhimu ya
uchumi wa nchi lakini pia kupatikana mapato.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Naweza kuendelea kuelezea ni
kwa namna gani Serikali nitakayoiongoza itaweza kuongeza uwezo wake wa kutimiza
majukumu niliyoyaainisha. Hapa bado sijagusia hatua za kubana matumizi ya
Serikali ambazo pia fikra zake tunazo.
Tofauti na baadhi ya wenzangu
waliotangulia kuzungumza, sijazungumzia mapato ya gesi kwa makusudi kwasababu
ukweli ni kwamba Rais wa awamu ijayo, hata akiwa madarakani kwa miaka kumi,
bado nchi yetu itakuwa haijaanza kupata fedha kutokana na gesi. Hata hivyo, ni
muhimu kuendelea na maandalizi ya nchi yetu kunufaika na uchumi wa gesi.
Na pia, tofauti na wenzangu,
sijazungumzia kukopa au misaada ya wahisani kwa ajili ya maendeleo yetu. Ukweli
ni kwamba tunao uwezo wa kufanya mambo yetu kwa kujitegemea huku
tukidhibiti deni letu la taifa. Ninachoweza
kusema tu ni kwamba mambo haya nimeyafikiria kwa kina. Katika kutafakari ni kwa
namna gani tutabadilisha hali za maisha ya watu wetu, sikukurupuka.
Inawezekana mambo
niliyoyazungumza kwamba tutayafanya yakaonekana kuwa ni mengi na ni mzigo.
Lakini waswahili wanasema tembo hashindwi na mkonga wake. Kama nilivyoonyesha,
tunao uwezo kabisa wa kuyafanya. Katika nchi yetu yenye mahitaji mengi, hatuna
anasa ya kuchagua kipi kiwe kwanza. Tunao wajibu kama viongozi wa ubunifu wa
kufanya mambo yote ya msingi kwa wakati mmoja. Tunazo rasilimali na uwezo wa
kuendeleza elimu na kilimo kwa wakati mmoja, tuna uwezo wa kumaliza matatizo ya
madawati nchini, matatizo ya madawa katika hospitali zetu, matatizo ya mikopo
kwa wanafunzi, matatizo ya maji, matatizo ya mishahara ya marupurupu ya
wafanyakazi na mambo mengi ambayo Watanzania wanayatarajia kutoka katika
Serikali yao.
Haya
yote yatawezakana iwapo tutafumua na kusuka upya mfumo wa utumishi na utendaji
wa Serikali ili kukomesha urasimu uliokithiri Serikalini, ili kurudisha nidhamu
ya kazi kwa watumishi wa umma, ili kuongeza uwezekano na uharaka wa
uwajibishaji wa watumishi wa umma wanaokiuka maadili ya kazi zao lakini pia ili
kurudisha ari, morali na fahari na heshima kwa watumishi wa umma.
Lakini napenda nirudie,
pamoja na yote haya, tiba ya uhakika ni kuutengeneza uchumi wetu ukue kwa namna
ambayo inawajumuisha Watanzania wa hali zote. Tiba ya uhakika ni kwa Watanzania kuumiliki
uchumi wao na kuwa na nguvu ya kiuchumi ya kujiamulia hatma ya maisha yao.
Serikali nitakayoiongoza italisimamia hili. Tiba kubwa ni nidhamu ya kazi na
uwajibikaji wa kila mmoja wetu.
Nasimama mbele yenu nikiwa na
bahati kubwa ya kupata malezi ya siasa na uongozi kwa viongozi waliotangulia wa
nchi yetu. Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa aliyefahamu uwezo wangu na
kunisaidia kupata elimu yangu ya Chuo Kuu na kuniwezesha kupata kazi Wizara ya
Mambo ya Nje. Na, Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyeniona nikiwa naye Wizara ya
Mambo ya Nje na kuniteua niwe Msaidizi wake kwenye kampeni za Urais mwaka 2005,
ambapo nilizunguka naye nchi nzima tukizungumzia kero za Watanzania, na baadaye
kuniteua kuwa Msaidizi wake Ikulu, ambapo nilipata fursa ya kuona na kujua nchi
inaendeshwa vipi, kushiriki katika mikutano yake yote na viongozi wengine
duniani na kuona diplomasia ya kimataifa inaendeshwa vipi, na kushiriki katika
vikao vya Baraza la Mawaziri na kujua maamuzi makubwa ya nchi yanafanywa vipi.
Namshukuru pia Rais Kikwete
kwa kunipa fursa ya kuwa kiongozi katika Chama chetu. Kwa kuwa Mjumbe wa
Sektretarieti ya Chama, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama na Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM, nimeshiriki kwenye uendeshaji wa shughuli za kila siku za
Chama chetu na nimekijua vizuri Chama.
Nimejua uimara na udhaifu wake. Na nimeyajua yanayopaswa kufanywa ili
kiendelee kuaminiwa na Watanzania.
Nawashukuru wananchi wa
Bumbuli kwa kuniamini niwe Mbunge wao. Nawashukuru wa kunifanya nionekane na
kuendelea kunipenda. Bado nina deni kubwa kwao kwa imani hiyo.
Napenda nifikie mwisho kwa
kusema kwamba ninayo dhamira, uwezo, maarifa na ubunifu wa kuiongoza nchi yetu
kukabiliana na changamoto mpya, za kizazi cha sasa, changamoto zinazohitaji
maarifa mapya.
Naishukuru sana familia
yangu, ikiwemo wazazi na ndugu na jamaa. Lakini zaidi mke wangu, ambaye
tumekuwa wote sasa kwa miaka zaidi ya kumi, na watoto wetu wawili kwa upendo na
uvumilivu.
Lakini kazi ya kuijenga nchi
sio kazi ya mtu mmoja. Kiongozi yoyote
anayesema yeye ndio Masia na amekuja kama mkombozi wa taifa, atakuwa
anawalaghai. Mafanikio yangu katika nafasi hii ninayoiomba na katika kutimiza
majukumu yangu yanategemea ushiriki na ushirikiano wenu. Nachukua nafasi hii
kuwaalika katika harakati hizi. Sigombei nafasi hii kupambana na mtu. Nagombea
kupambana na changamoto za watu. Nikifanikiwa, nitasikiliza mawazo mazuri
kutoka kwa kila mtu, hata ambao sio wana-CCM. Nitakuwa kiongozi wa watu wote –
bila kujali dini zao, makabila yao, rangi zao, vyama vyao au kanda wanazotoka.
Nitaongoza kwa namna ambayo Watanzania watajisikia fahari kuongozwa nami.
Sijawa kwenye siasa kwa miaka
30 au 40 kama baadhi ya wagombea, ambao wamepata fursa nyingi na madaraka
makubwa ya kutekeleza yale wanayoyaahidi leo. Lakini nimekuwepo kwenye uongozi
kiasi cha kutosha cha kujua matatizo yako wapi, nini cha kufanya, na namna ya
kufanya, kama ambavyo nimeelezea kwa kirefu mchana huu. Mkinipa nafasi hamtakuwa mnatumaini tu, bali mtakuwa
mnaonyesha dhamira ya kutaka hakika ya mabadiliko makubwa.
Nafarijika kwamba kwenye
Chama chetu wamejitokeza wagombea wengi. Hili ni jambo jema sana kwani
kunaonesha ukomavu wa kidemokrasia. Lakini ni muhimu sote tukaelewa kwamba
kugombea sio kugombana. Binafsi ndivyo ninavyoelewa na ndio maana sikutumia
muda wenu kumshambulia mtu kwasababu jambo hili halisaidii Watanzania. Nina
imani kubwa kwamba, kwa ukomavu wa Chama chetu, tutabaki wamoja na imara mara
baada ya mchakato huu. Chama chetu kina
dhamana kubwa na kina historia adhimu barani Afrika. Dunia nzima inatazama
mchakato huu wa ndani ya Chama chetu. Matumaini ya marafiki zetu na matumaini
ya wanachama wetu ni kwamba tutachagua mgombea wetu kwa msingi wa kujiamini na
sio kwa msingi wa woga wa kusambaratika.
Mkinichagua mimi kupeperusha
bendera ya chama, nitatumia nguvu zangu zote na utajiri mkubwa wa hekima ndani
ya chama chetu kuvunja makundi yote yaliyojitokeza kipindi hiki cha uchaguzi na
kuwaunganisha wana-CCM wote. Mwenyekiti
wetu, Makamu Wenyeviti na Katibu Mkuu na Sekretarieti yake wamefanya kazi nzuri
ya kukiimarisha Chama chetu na kukijengea uwezo. Nitakapokuwa kiongozi wa Chama
chetu nitaanzia walipoishia. Nimekuwa chipukizi wa Chama hiki. Nimekuwa
kiongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama hiki. Na nimefikia hadi kuwa Mjumbe wa
Kamati Kuu wa Chama chetu. Nafahamu changamoto za watendaji wa Chama na Jumuiya
mikoani na wilayani. Wanafanya kazi kubwa. Nitawatazama. Nafahamu Wenyeviti
wetu wa Mikoa na Wilaya, wana mahitaji mahsusi ya kufanya kazi zao za uongozi
wa Chama chetu na usimamizi wa Ilani yetu katika ngazi zao. Nayajua hayo
mahitaji. Naelewa majukumu mapya ya Wajumbe wa NEC yanahitaji uwezeshaji.
Tutayazungumza na kuyafanya. Nafahamu Makatibu wa Siasa na Uenezi na Makatibu
wa Uchumi na Fedha wa Mikoa na Wilaya wanafanya kazi kubwa na wanastahili
kutambuliwa. Chama chetu kitakuwa salama chini ya uongozi wangu.
Tutaendelea na kazi nzuri
inayofanywa sasa na viongozi wetu ya kukiimarisha Chama chetu ili kiendelee
kuwa tumaini la Watanzania.
Nimalizie kwa kurudia kwamba
sigombei nafasi hii kupambana na mtu bali kupambana na matatizo ya watu. Nataka kushirikiana nanyi wote tuijenge
Tanzania Mpya. Nataka uongozi wangu uwe mwanzo wa Tanzania Mpya, ya miaka 50
ijayo. Tunataka tujenge taifa la Watanzania ambao kila mmoja ana fursa, uwezo
na nguvu ya kiuchumi ya kupata mahitaji yake na kuendesha maisha yake. Tunataka
kujenga taifa ambalo wananchi hawabebi mzigo wa maisha unawaelemea. Tunataka
kujenga taifa la watu wenye sauti na kauli juu ya Serikali yao. Haya mambo sio ndoto. Yanawezekana kabisa.
Viongozi huwekwa na Mungu. Ninapoomba
uongozi huu, namuomba Mungu anipe fursa ya kuwaongoza watu wake kupitia ridhaa
yao. Kama mgombea, namuomba Mungu anipe uwezo, hekima na busara ya kupokea
matakwa yake katika mchakato huu. Na kama kiongozi, namuomba anipe hekima ya kuwaongoza
watu wake na kushughulikia mashauri yao kwa haki na ukweli.
Na kubwa zaidi, namuomba
Mungu aendelee kuibariki nchi yetu na watu wake.
Asanteni sana kwa
kunisikiliza.
January Makamba.
Juni 7, 2015.