Tuesday, June 9, 2015

Hotuba ya January Makamba ya kutangaza kuomba nafasi ya Urais wa Tanzania, Juni 7, 2015.

Kama ilivyo ada, tunaanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka zake na kibali chake cha kutukunanisha siku hii ya leo.

Nawashukuru wote mliofika hapa na nyote mnaonisikiliza kupitia luninga na redio. Nawashukuru pia wana-CCM na Watanzania waliokusanyika katika mikoa mbalimbali ambao wataunganishwa nasi moja moja wakati wa kipindi cha maswali na majibu.

Nimeonelea nitumie siku na fursa hii kuwajulisha kwamba, baada ya tafakuri ya kina ya changamoto za sasa nchi yetu na mahitaji ya uongozi wa aina mpya, nimeamua kuomba nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa ajili hiyo, keshokutwa, nitasafiri kwenda Dodoma kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya wana-CCM ili niweze kuteuliwa na Chama chetu kuwa mgombea kwa nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Nafanya hivyo nikitambua ukubwa na utakatifu wa dhamana ninayoiomba.

Naiomba nafasi hii nikiwa nimejiridhisha bila shaka yoyote kwamba ninao uwezo, ukomavu, uzalendo, uadilifu, uzoefu, hekima, busara, maarifa na ubunifu wa kuishika nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naiomba nafasi hii nikielewa kiu ya Watanzania ya kupata uongozi mpya, wa zama za sasa, unaotoa matumiani mapya, yatakayozaa Tanzania mpya.

Naiomba nafasi hii nikiwa naelewa misingi iliyoijenga nchi yetu – misingi ya haki, umoja, amani, mshikamano na upendo miongoni mwa Watanzania – na haja ya kuilinda misingi hiyo.

Nchi yetu iko katika njia panda. Katika miaka 10 ijayo, Tanzania inaweza kuchukua njia mojawapo kati ya hizi mbili: inaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo na hali ya maisha ya wananchi wote kuboreka.

Lakini vilevile, ipo hatari ya taifa letu kupasuka kutokana na dalili za mpasuko wa kidini, mmomonyoko wa maadili kwenye jamii, kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa dola, dalili za ufa katika Muungano, umaskini na tofauti kubwa ya kipato baina ya wananchi.

Aina ya uongozi tutakaouchagua mwaka huu ndio utaamua mustakabali wa nchi yetu. Baada ya miaka 50 ya uongozi wa kizazi kilichopita, sasa ni wakati wa nchi yetu kuongozwa na viongozi wa aina mpya, wenye mtazamo mpya, fikra mpya, maarifa mapya na majawabu mapya.  

Ndugu zangu, Watanzania wenzangu,

Nimesimama hapa kuwahakikishia kwamba nimefanya tafakuri ya kina na za muda mrefu kuhusu mwelekeo wa nchi yetu. Na niko tayari kutengeneza na kuongoza timu madhubuti ya Watanzania wazalendo na waadilifu watakaounda Serikali itakayojenga kesho njema.

Nimesimama hapa kuwakaribisha wana-CCM wenzangu na Watanzania wote kwenye kampeni hii. Tunayo dhamira na uwezo wa kushinda na kuongoza mabadiliko makubwa ambayo Watanzania wanayatarajia.

Kwa mambo niliyoyaona na kujifunza kuanzia kufanya kazi na Rais Kikwete Ikulu, kwenye uongozi wa Chama, Bungeni na Serikalini, nimepata matayarisho ya kutosha ya kuiongoza nchi yetu.

Naiomba nafasi hii nikiwa naijua vyema sana nchi yetu, nikiwa nayajua kwa kina matatizo ya Watanzania katika kila kona ya nchi yetu, na nikiwa nimejiridhisha kwamba ninao ubunifu na maarifa ya kutosha ya kutafuta majawabu mapya kwa ajili ya kuinua hali za maisha za Watanzania.

Siko mbele yenu kuwasimulia kuhusu matatizo ya nchi yetu ambayo sote tunayajua. Niko mbele yenu kuelezea namna tukavyotatua matatizo ya nchi yetu. Katika kuomba nafasi hii nimefikiria na nitaelezea baadhi ya majawabu mapya ambayo yananitofuatisha mimi na wengine wanaoomba nafasi hii.  

Natambua kwamba nikiteuliwa na Chama changu, nitakabidhiwa Ilani ya Uchaguzi itakayoelekeza mambo ya kufanywa na Serikali ijayo. Nitainadi Ilani hiyo na kuitekeleza kwa nguvu zangu zote.

Hata hivyo, kama wasemavyo waswahili, ziada njema haigombi. Kuwepo kwa Ilani hakuzuii kuwa na mambo ya ziada ya msingi kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.  

Kwa msingi huo, nianze kwa kusema kwamba Serikali nitakayounda itaendeshwa na falsafa ya uwezeshaji mpana wa wananchi – kiuchumi, kisiasa na kijamii. 

Kwa miaka mingi sasa, Watanzania wamepewa ahadi nyingi na viongozi wa siasa. Badala ya kuwaahidi wananchi kwamba tutawafanyia kila kitu, Serikali nitakayoiunda itawajengea uwezo na nguvu ya maamuzi kuhusu maisha yao. Serikali yangu itajikita katika kuwajengea nguvu ya kiuchumi ya kuendesha maisha yao, na kuamua waishi wapi, wapeleke watoto shule wapi, waanzishe biashara gani, wajenge nyumba za aina gani, wakatibiwe wapi.

Tutawajengea uwezo wa kuwa na sauti katika maamuzi ya Serikali yao. Tutaondokana na dhana ya wananchi kubaki watazamaji tu katika masuala ya nchi yao.  

Sitaunda Serikali ya waporaji na wabinafsi. Nitaunda Serikali yenye utu na inayowasikiliza na kuwajali watu. Serikali inayotimiza wajibu wake bila chembe ya uzembe wala ulegevu. Nitaunda Serikali yenye Mawaziri wasiozidi 18 ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa shaka kuhusu uwezo na uadilifu wake.

Serikali yetu itakuwa na vipaumbele vikubwa vitano:

Kwanza ni kukuza kipato cha watu. Msingi wa maendeleo ya nchi yetu sio mapato ya Serikali, bali ukubwa na uhakika wa kipato cha Watanzania. Kama nilivyosema awali, nitataka Watanzania tuwe na nguvu na uwezo wa kiuchumi wa kuendesha maisha yetu.

Kwahiyo, kwa wale wenye shughuli za kufanya – iwe ni kilimo, uvuvi, ufugaji au biashara – tutaweka mazingira ya kisera, kisheria na kikodi ili shughuli hizo zipanuke, zishamiri, ziwe na faida kwao na ziwanufaishe katika maisha yao.

Falsafa yetu ni kwamba mtu yoyote anayetoa jasho kutengeneza maisha yake na ya familia yake, ni lazima anufaike na juhudi na jasho lake. Kwa wale wasio na shughuli za kipato, tutafanya jitihada zote ili wawe na shughuli za kiuchumi za kufanya. Tutatengeneza fursa za kiuchumi ili mtu yoyote kama hana shughuli ya kufanya basi awe ameamua mwenyewe. Maendeleo ya nchi yatapatikana kwa nguvu ya uchumi ya wananchi, sio kwa hisani ya wafadhili.

Kipaumbele cha pili kitakuwa ni kupatikana kwa huduma bora za jamii na kiuchumi. Kazi kubwa imefanywa na viongozi waliotangulia, lakini bado Watanzania wengi wanahitaji kupata huduma ya uhakika ya maji, afya, elimu bora, barabara za uhakika, umeme, huduma za fedha na mawasiliano.  Tutabuni mbinu mpya za kumaliza matatizo haya.

Kipaumbele cha tatu ni utawala bora, wa haki na wa sheria. Msingi wa amani ya nchi yetu ni haki. Wananchi wengi hawana uhakika wa kupata haki zao waendapo polisi au mahakamani. Serikali yangu italibadilisha hili. Tutazijenga upya taasisi ya usimamizi wa utawala na haki za watu, zikiwemo mahakama na jeshi la polisi. 

Hatutakubali Mtanzania yoyote aonewe na watu au mamlaka za umma. Lakini pia tutataka kila mtu afuate sheria za nchi, hata ziwe ndogo kiasi gani.

Tutakabiliana na tatizo la ubadhirifu wa mali ya umma kwa nguvu zote. Nampongeza Rais Kikwete kwa kufanya jambo la kimapinduzi la kuelekeza Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ziwekwe hadharani na kujadiliwa.

Serikali yangu itaenda mbele zaidi na kuhakikisha kwamba ripoti ya CAG ikitolewa, viongozi ambao taasisi zao zimekutwa na makosa wanakaa pembeni siku hiyo hiyo na hatua za kisheria, za kipolisi, za kimahakama zinaanza siku inayofuatia.

Kipaumbele cha nne ni usimamizi wa uchumi. Serikali yangu taimarisha uwezo wa taasisi za usimamizi wa uchumi – ikiwemo Wizara ya Fedha, Tume ya Mipango, Benki Kuu na Mamlaka ya Mapato. Nitazipa mamlaka na rasilimali-watu ili ziweze kudhibiti mfumuko wa bei, kuporomoka kwa thamani ya shilingi, nakisi ya bajeti, kupungua kwa hifadhi ya fedha za kigeni, kukua kwa deni la taifa na kusimamia uwekezaji wa kimkakati wa sekta binafsi.

Kama ambavyo tuna Baraza la Usalama wa Taifa sasa, nitaunda Baraza la Uchumi la Taifa litakalojumuisha wataalam kutoka katika taasisi za umma za usimamizi wa uchumi, wagwiji wa uchumi kwenye nchi yetu, pamoja na wawakilishi wa sekta binafsi.

Baraza hili litakuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba uchumi wetu unawekewa mikakati ya muda mrefu na wakati wote hali ya uchumi wetu inaratibiwa kwa weledi na changamoto zinazojitokeza zinarekebishwa haraka. 

Kipaumbele cha tano ni amani, umoja na usalama wa mali na maisha ya Watanzania. Amani na umoja wa nchi yetu ni tunu na urithi tulioachiwa na waasisi wa nchi yetu. Marais wote waliopita wamefanya kazi kubwa ya kuzilinda tunu hizi. Serikali yangu haitakubali urithi huu upotee. Tutafanya jitihada zote ili kujenga maridhiano mapya na upendo miongoni mwa makundi mbalimbali katika jamii yetu. Nitawahusisha viongozi wa dini zote katika hili. Nitaanzisha Jukwaa la Rais na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Jumuiya ya Wakristo Tanzania (CCT) na Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) litakalokutana kila miezi miwili kujadili na kupanga mikakati ya kuendeleza amani, umoja, upendo na maadili ya jamii.

Pia tutachukua hatua mpya za kuimarisha Muungano wetu na kuupatia uhalali mpya na wa ziada miongoni mwa Watanzania.

Ndugu Watanzania wenzangu,

Naomba sasa nifafanue majawabu mapya ambayo Serikali yangu itayatekeleza kwa changamoto mahsusi:

Naomba nianze na suala la ajira. Kwasasa, wapo zaidi ya Watanzania milioni 23 kwenye soko la ajira leo hii. Kila mwaka wanaongezeka vijana zaidi ya laki tisa kwenye soko la ajira.

Hawa ni watu wengi sana. Viongozi wengi wa siasa wameliita tatizo la ajira kuwa ni bomu. Lakini kulielezea tatizo sio kulitatua.

Serikali yangu itafanya nini?

Watanzania wengi wanajishughulisha na biashara ndogo na za kati. Karibu zote zinaajiri mtu mmoja au wawili na nyingi zinasuasua.  Watalaamu wanatuambia, asilimia 20 tu ya biashara na kampuni ndogo nchini zikiongeza mfanyakazi mmoja kwa mwaka, ajira 400,000 za kudumu zitazalishwa kwa mwaka. Je asilimia 80 za biashara hizi zikiongeza watu wawili wawili tu kwa mwaka? Tutakuwa tumepunguza sana kama sio kumaliza tatizo la ajira.

Kwahiyo, jawabu letu la kwanza litakuwa ni maendeleo ya biashara ndogo na za kati. Zilizopo zifanye vizuri na kuongeza waajiriwa na wale wanaotaka kuanzisha biashara, iwe rahisi kufanya hivyo.  

Ziko namna kadhaa za kufanya hivi. Kwa mfano, katika nchi yetu, Serikali bado ndio mnunuzi mkuu. KIla siku, Serikali yetu inanunua bidhaa nyingi - kuanzia kuni, karatasi, matofali, mabati, vyakula na huduma nyingine nyingi. Katika kuzijengea uwezo kampuni ndogo na za kati, Serikali yangu itaweka Sheria ya kuwezesha asilimia 30 ya thamani ya manunuzi ya umma kupewa makampuni madogo na ya kati yatakayokidhi vigezo rahisi yanayomilikiwa na vijana na wanawake. Jambo hili litawezesha biashara nyingi ndogo kujenga uwezo, kupanuka na kuajiri watu wengi zaidi.

Lakini, ili hili litokee, lazima tuwe na taasisi madhubuti ambayo itashughulika na ustawi wa biashara na makampuni madogo na ya kati.

Kwahiyo, nitaanzisha Mamlaka mahsusi ya Maendeleo ya Biashara Ndogo na za Kati. Pamoja na mambo mengine, Mamlaka  hii itapewa majukumu ya kuwezesha, kurahisisha na kusimamia biashara ndogo kuanzishwa kwa urahisi, kuendeshwa bila bughudha, na kupata fursa ya kukua.

Ndugu Wananchi,

Viwanda bado ni tegemeo kubwa la ajira. Kwa viwanda vikubwa vilivyopo sasa, tutaweka motisha ya kikodi kwa yoyote ambaye ataweza kuongeza ajira mpya angalau 500 au zaidi za kudumu kwa mwaka. Haipaswi kumgharimu kikodi mtu mwenye biashara kuongeza wafanyakazi.

Kwa waajiri ambao ni biashara au kampuni mpya ndogo na za kati, yaani SMEs, Serikali yangu itatoa motisha ya kupunguziwa kodi hizi kwa kila kazi mpya tano au zaidi kwa mwaka. Ukweli hapa ni kwamba kunawiri kwa uchumi hakutokani na kodi inayokusanywa na Serikali bali kunatokana na kipato na uwezo wa manunuzi walionao wananchi na kipato cha wafanyabiashara kuweza kukuza biashara zao na kutoa ajira nyingi zaidi.
Vilevile, katika kukabiliana na tatizo hili la ajira, tutawezesha sekta binafsi kujenga na kufufua viwanda vya nguo, katani na korosho nchini. Huko nyuma tulishawahi kuwa na viwanda vingi vya aina hii, vikichangia asilimia 25 ya pato la Taifa na kuajiri asilimia 25 ya wafanyakazi wote nchini. Kwa sasa, ni asilimia 30 tu ya pamba yetu ndio inayotumika nchini. Pamba tunayo ya kutosha kukidhi mahitaji ya viwanda vikubwa zaidi ya hamsini. Ndani ya miaka mitano ijayo tutahakikisha tunajenga na kufufua viwanda 11 vya nguo vitakavyotoa ajira mpya zaidi 100,000 viwandani tu, huku asilimia zaidi ya 80 ya wafanyakazi hawa wakiwa ni wanawake. Lengo ni sekta nzima ya pamba kuajiri walau asilimia 10 ya nguvu kazi (kazi milioni 2.5).

Katika kuwezesha hili, Serikali nitakayoiongoza itachukua hatua za muda mfupi za kikodi na kiushuru ili kuwezesha viwanda hivi kukabiliana na ushindani wa kanga, vitenge, mitumba na vitambaa kutoka nje ya nchi. 

Ndugu wananchi,

Shughuli za ujenzi wa nyumba na miundombinu huongeza chachu katika uchumi na kuongeza ajira nyingi sana. Tuna mahitaji makubwa ya nyumba na tuna mahitaji makubwa ya ajira. Nitahakikisha tunatengeneza mazingira mazuri ya uanzishwaji na uimarishaji wa makampuni madogo na ya kati yanayojihusisha na biashara katika sekta ya nyumba. Tutahakikisha kwamba, ndani ya miaka kumi ya uongozi wangu, sekta ya ujenzi inachangia zaidi ya asilimia 25 ya Pato la Taifa na kuajiri zaidi za watanzania milioni 5. Hii itawezekana kwa kupunguza gharama za ujenzi. Na hili litawezekana kwa uwekezaji kwenye viwanda vya vifaa ya ujenzi, kama vile viwanda vya nondo, mabati, simenti, vigae na vioo.

Hii itaenda pamoja na ujenzi wa miundombinu mikubwa, hasa ya usafirishaji. Tutaweka jitihada za makusudi kuongeza kasi na ukubwa wa miradi ya miundombinu nchini ambayo itaajiri watanzania wengi zaidi na kuingiza fedha nyingi zaidi kwenye mzunguko wa uchumi. Tutahakikisha kwamba wakandarasi wa miradi hii ni makampuni ya ndani yatakayohifadhi na kuwekeza fedha hizo hapa ndani. Lengo langu ni kuwezesha wakandarasi wa ndani kiufundi, kiutawala na kifedha na kuwawezesha kupata walau asilimia 80 ya miradi yote ya miundombinu inayojengwa kwa fedha za umma ndani ya miaka kumi ijayo.

Shughuli za sanaa na michezo zikisimamiwa vizuri zina uwezo wa kuajiri asilimia kubwa ya watanzania. Mapema kabisa kwenye serikali yetu tutarasimisha shughuli za sanaa ikiwemo sinema, muziki na kazi zote za ubunifu. Tutatunga Sheria kali zaidi kulinda hakimiliki. Kupitia Mfuko wa Sanaa wa Taifa tutakaouunda upya, tutatoa ruzuku na mikopo ya masharti nafuu kwa wazalishaji, waendeshaji na wasanii wenyewe kwenye kuendeleza ubunifu na kuzalisha, kutangaza na kuuza kazi mpya kwa njia za kisasa. Tukiweza kuongeza maradufu uwekezaji kwenye tasnia ya sanaa na ubunifu hapa nchini, tutatengeneza ajira mpya zaidi ya milioni mbili.
Sita, kwa vijana wasomi na wanataaluma ambao hawatakuwa wamebahatika kupata ajira katika sekta rasmi, tutawawekea utaratibu wajiunge na kuanzisha makampuni na biashara za kitaaluma – wahandisi, wanasheria, wasomi katika fani za siasa na utawala, na wengineo – na tutawapa mikopo maalum ya kufanya hivyo.
Kwa upande wa wamachinga, naelewa kwamba wanazunguka kutwa nzima wakiuza bidhaa ambazo hawazimiliki na huishia kupata pesa ya kula tu au nauli au hawapati kitu kabisa.  Viongozi nitakaowateua kuongoza Mamlaka mpya ya Biashara Ndogo na Za Kati katika mwaka wao wa kwanza watapimwa kwa uwezo wao wa kuhakikisha wamachinga wana sehemu salama na zenye wateja za kufanyia shughuli zao na hawaishii kuwa fremu tu barabarani kwa mali za watu wengine.
Jambo jingine kubwa tutakalofanya ni kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji hapa nchini katika miaka mitano kwa ajili ya wanavijiji kukopeshana kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali. Mfuko huu utaendeshwa na Kamati maalum zitakazoundwa na wanavijiji wenyewe na wao ndio watakaomua nani akopeshwe na arudishe baada ya muda gani. Mzunguko wa shilingi milioni 50 kwenye shughuli za uzalishaji mali kijijini utatoa chachu ya maendeleo ya watu. Fedha zinazohitajika hazifiki bilioni 700 katika miaka mitano. Kwa sasa tunakusanya zaidi ya bilioni 800 kwa mwezi. Fedha hizi tutazipata na nitaelezea ni. Utaratibu wa aina hii umebadilisha maisha ya wananchi wa vijijini huko nchini Thailand.
Kilimo bado ndio nguzo ya ajira kwa Watanzania wengi. Mambo mengi yamezungumzwa kuhusu mapinduzi ya kilimo kwa miaka mingi. Kila zao linalolimwa nchini – iwe ni pamba, korosho, chai, kahawa, tumbaku, mkonge, au mboga na matunda – lina changamoto zake mahsusi. Serikali yangu itabadilisha namna ya kushughulikia maendeleo ya kilimo kwa kuweka mkakati ya zao moja moja tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna mikakati ya jumla ya kilimo.  Tutabadilisha utaratibu wa sasa wa upatikanaji wa pembejeo ambapo pesa nyingi zinapotea kwa watu wa kati huku wakulima wakiwa hawapati pembejeo za kutosha, kwa wakati na kwa bei wanayoimudu. Tutaweka mkazo kwenye kurekebisha mfumo wa ununuzi wa mazao ambao kwasasa unamkandamiza mkulima. Tutaanzisha Soko Kuu la Kitaifa la Mazao, yaani Commodities Exchange, litakalowezesha wakulima kuwa na nguvu ya kujua na kuamua bei na wakati wa kuuza mazao yao.
Kwenye uvuvi na ufugaji, mipango iliyopo inatosheleza. Tutakachokifanya na kuitekeleza kwa haraka na uhakika. Kwa maeneo ya uvuvi, tutaanzisha mifuko ya kuwawezesha wavuvi kukopeshwa nyavu, boti na mashine na majokofu ili waweze kwenda mbali majini na kuhifadhi samaki kwa muda mrefu ili wapate soko zuri na bei nzuri. Hatutaacha wafugaji wakose malisho ya mifugo yao. Kila mfugaji atamilikishwa eneo ya malisho na kupewa hati. Hii itasaidia kumaliza migogoro kati yao na wakulima.
Ndugu wananchi,
Jambo jingine ambalo ningependa kuliongelea ni suala la elimu. Ni lazima kukiri kwamba, pamoja na changamoto zilizopo, mafanikio makubwa yamepatikana kwenye Serikali ya Rais Kikwete kwenye nyanja ya elimu, hasa kwenye udahili wa wanafunzi kwa ngazi zote. Pamoja na mafanikio haya, changamoto za elimu zipo lukuki na ndugu zangu Watanzania mnazijua. Sasa nini kifanyike kuboresha elimu? Katika serikali yetu, tutatekeleza yafuatayo.
Kwanza, Serikali yangu itaondoa shaka na kumaliza kabisa mjadala kuhusu dira ya elimu yetu. Tutaongozwa na dira ya elimu inayochochea vijana kujiajiri, inayochochea udadisi, inayochochea ubunifu, inayochochea uthubutu, nidhamu, weledi na uzalendo. Tutatengeneza mitaala mipya na thabiti kabisa inayokidhi mahitaji ya mazingira na changamoto za sasa na mahitaji ya uchumi wa kisasa, mahitaji ya jamii na mahitaji ya taifa kwa ujumla. Hiyo ndio itakuwa mihimili ya elimu tutakayowafundisha watoto wetu chini ya uongozi wangu.
Tutawafundisha watoto wetu kwa lugha zote mbili, ya Kiswahili na Kiingereza kwasababu ni jambo linalowezekana.
Rais Kikwete amefanya kazi kubwa katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu. Bado changamoto ipo kwenye walimu wa sayansi na hisabati. Tutaongeza udahili kwenye vyuo vya ualimu vinavyofundisha masomo hayo ili kupata walimu wengi zaidi.

Kama saikolojia ya mwalimu haijakaa sawa kutokana na changamoto nyingi, tusahau kuhusu ubora wa elimu. Tunasema ualimu ni wito lakini haipaswi kuwa adhabu. Tutazitatua changamoto za walimu, ikiwemo mazingira yao ya kazi, motisha na hamasa yao ya kufundisha ikiwemo mishahara yao, kupandishwa madaraja, mafunzo yao ya ziada ya kujiendeleza.

Tutaweka vipimo vipya ya maendeleo ya elimu nchini kwa kupima uelewa na maarifa ya wanafunzi kwa mambo wanayopaswa kuyajua katika ngazi husika ya elimu. Hatutaishia tu kusheherekea ufaulu wa jumla katika mitihani ya mwisho. Pia, tutaweka mfumo wa motisha ya malipo au kupandishwa vyeo kwa walimu wetu wa shule za Serikali wanaofanya vizuri

Vilevile, hatutaingiza siasa kwenye maendeleo ya elimu. Tutaweka uongozi thabiti na wa kizalendo kwenye sekta ya elimu utakaokabiliana na changamoto za uendeshaji na utawala wa sekta ya elimu, ikiwemo masuala ya ukaguzi, usimamizi wa walimu, uidhinishaji na usambazaji vitabu kwenye mashule, upelekaji na matumizi ya fedha za uendeshaji wa shule na mambo mengineyo.
Ili kuchukua vijana wengi wanaoishia darasa la saba na kidato cha nne, tutajenga Chuo kikubwa cha ufundi kwenye kila Wilaya ya nchi yetu kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Serikali yangu itabadilisha utaratibu na kuweka utaratibu mpya, wa wazi na wa haki ili kila anayestahili mkopo apate na apate kwa kiwango kinachotosheleza. Tutaanzisha Mfuko Maalum, yaani National Education Endowment Fund, kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu kwa wenye mahitaji maalum. Serikali pia itaweka dhamana ya mikopo wanafunzi katika taasisi binafsi zitakazokuwa tayari kukopesha wanafunzi. Zaidi ya hapo, tutaanza utaratibu wa kuviwezesha vyuo na taasisi za elimu ya juu viwe na mifuko kwa ajili ya kutoa mikopo na misaada kwa wanafunzi.
Jambo jingine kubwa ambalo ningependa kulizungumzia ni tatizo la rushwa. Limezungumzwa na wengi. Lakini kulizungumzia na kulipigia kelele suala la rushwa pekee hakulimalizi. Ziko namna mbili tutakazozitumia kukabiliana na hili tatizo: njia ya kwanza ni kisheria, kimfumo na kitaasisi; njia ya pili ni kijamii.

Kuhusu kimfumo, nitafanya mabadiliko makubwa mawili. Kwanza, ni kuiwezesha TAKUKURU kuwa na mamlaka kisheria ya kuwashitaki watuhumiwa wa rushwa moja kwa moja mahakamani. Pia, tuanzishe Mahakama Maalum ya Uhujumu Uchumi ambayo itahusika na makosa ya rushwa; ubadhirifu wa mali ya umma; ukwepaji kodi; kuiba, kunufaika au kutaka kuiba au kutaka kunufaika na mali ya umma; na makosa mengine ya aina hii.

Mahakama ambayo itakuwa na jopo maalum la majaji ambalo litafanya kazi mwaka mzima na kusikiliza na kuhukumu kesi hizi haraka. Kesi za uhujumu uchumi ziendeshwe wazi na mfululizo na adhabu ziwe kali sana, kwa mfano ya kifungo cha maisha. Pia tutaanzisha Kurugenzi ya Uchunguzi na Mashtaka ya Uhujumu Uchumi. Tutaiwezesha Mahakama hii na Kurugenzi hii bila ukomo wa kirasilimali kuifanya kazi hii vizuri.

Kuhusu kijamii, kwa kushirikiana na viongozi wa dini na wengine wa kijamii, nitaanzisha na kuwezesha mjadala mpana kwenye jamii yetu kuhusu maadili ya jamii. Jamii yetu ijengwe kwenye misingi ya kuchukia rushwa, ulaghai na njia za mkato za kupata mali. Inapofika mahala jamii inasheherekea mali ambazo hazina maelezo, inapofika mahali ambapo jamii inawatukuza wachache ambao wametumia ujanja kufanikiwa, inapofika mahala ambapo jamii inakuita mjinga unapostaafu ukiwa hujilimbikizia mali, hapo lipo tatizo ndani ya jamii. Lazima kujenga jamii tofauti, ambayo wala rushwa wanajiona kama wanatembea uchi, jamii ambayo inatoa adhabu za kijamii, yaani social sanctions, ikiwemo kutengwa, ambazo ni kali kuliko adhabu za kisheria. Mwalimu Nyerere alijaribu kujenga jamii ya aina hii: jamii ambayo kiongozi wa umma hapaswi kungoja mahakama itamke kwamba ni mla rushwa. Tunapaswa kuendelea kujenga jamii ya aina hii. Viongozi wa dini wana nafasi kubwa. Maadili na malezi na makuzi kwenye familia pia yana nafasi yake.

Ndugu zangu Watanzania, bila kudhibiti rushwa na wizi hatuwezi kupata maendeleo. Kwa hiyo, kwa kiongozi yoyote, kama anataka kuacha rekodi nzuri ya maendeleo, kuitokomeza rushwa ni jambo la kufa na kupona.

Katika uchaguzi huu, tunayo fursa ya kuanza safari ya kumaliza tatizo hili. Rekodi ya uadilifu sio sifa pekee ya uongozi. Lakini pia sio jambo la kupuuzwa hata kidogo. Namna viongozi wanavyotafuta uongozi ndio namna watakavyotawala. Tunayo fursa ya kuchagua viongozi ambao hawatapata kigugumizi kupambana na rushwa. Tunayo fursa ya kuchagua viongozi ambao hawatakuwa na madeni ya kulipa. Sina shaka kabisa kwamba mimi ni kiongozi wa aina hiyo.

Ndugu wananchi,

Napenda pia kuzungumzia suala la ardhi.  Hili pia ni muhimu kwasababu mbili: kwanza, ardhi, kwa maana ya umiliki na matumizi yake, ndio msingi wa yote; na pili, zimeanza kuonekana dalili ya watu wachache kuhodhi ardhi kubwa na kuanza kuirudisha nchi yetu kwenye zama za ukabaila.  Hakuna maendeleo ya kilimo kama hakuna uhakika wa matumizi bora ya ardhi na kama hakuna uhakika wa mfumo wa umiliki wa ardhi.

Lazima sasa kuondoa migogoro ya ardhi isiyoisha kati ya wakulima, wafugaji, wawekezaji na Serikali na kuipa ardhi thamani halisi inayostahili. Kama tunavyobainisha kisheria na kulinda hifadhi za misitu na mbuga za wanyama lazima maeneo ya kilimo na mifugo na makazi ya watu nayo yawe hivyo. Lazima wakulima wamiliki ardhi yao kisheria. Lazima kutenga maeneo maalumu ya wafugaji yanayomilikiwa na wafugaji kisheria na bila kusahau korido mahususi za kupitisha mifugo kutoka upande mmoja wa nchi mpaka mwingine.

Serikali yetu itatumia teknolojia mpya ya satellite katika kupima na kupanga matumizi ya ardhi nchini. Tutajenga kituo cha kupokea picha za satellite ambacho kitawezesha kila kipande cha ardhi katika nchi yetu kupimwa, na hati ya umiliki, yenye picha na mipaka isiyo na shaka, kutolewa na matumizi ya ardhi hiyo kujulikana. Kituo hiki hakigharimu fedha ambazo tunazishindwa.

Kuhusu huduma ya afya, Watanzania wengi, hasa wa vijijini, bado wana changamoto kubwa kuipata. Kazi nzuri imefanywa na Serikali ya Rais Kikwete kusogeza huduma hii karibu na wananchi na kuiboresha. Kazi hiyo tutaiendeleza. Tutaitazama huduma ya afya kimfumo zaidi na kurekebisha uendeshaji wake.

Lakini kubwa tutakalofanya ni kuhakikisha kwamba kila Mtanzania ana bima ya afya na anapata matibabu bila kujali uwezo wa kipato chake. Moja ya namna ya kufanya hili ni kutengeneza Sheria mpya ya kuiunganisha mifuko yote ya Bima na kurahisisha ukusanyaji na matumizi ya pesa kwenye vituo vya afya ya msingi. Nchi nyingine za Afrika wamefanya hivi na kufanikiwa. Na sisi hatuwezi kushindwa.  Tutaondoa ukiritimba na urasimu wa Bohari ya Madawa ya Taifa katika kusambaza madawa katika vituo vya huduma vya Serikali.

Kwa wananchi wa Tanzania, ukiwauliza leo ni huduma ipi ya jamii bado ni kero kubwa. Jibu litakuwa ni huduma ya maji. Watanzania wanaopata huduma hii hawafiki asilimia 60. Maeneo ya vijijini hali ni mbaya zaidi. Ni jambo la kawaida kwa kina mama vijijini kutumia siku nzima na kwenda umbali mrefu kupata nusu ndoo kwa familia nzima. Tatizo kubwa ni uwekezaji mdogo katika sekta ya maji. Ili kukabiliana na tatizo hili, tutaanzisha Mfuko wa Maji Vijijini pamoja na Wakala wa Maji Vijijini. Tumeona jinsi Mfuko wa Barabara na Wakala wa Barabara wa Taifa unavyofanya kazi nzuri kwenye ujenzi wa barabara. Tumeona jinsi ambavyo Mfuko wa Umeme Vijijini na Wakala wa Umeme Vijijini ulivyofanya kazi nzuri kusambaza umeme vijijini. Tumeweza kufanya kazi nzuri ya barabara na umeme kwa kutumia fedha zetu wenyewe.

Utaratibu mpya na msukumo mpya wa kupeleka maji vijijini utasaidia. Chanzo cha fedha kwa Mfuko wa Maji kinaweza kuwa tozo maalum ndogo kwenye matumizi ya maji mijini na maji ya kunywa kwenye chupa. Nina uhakika kabisa kuwa ndani ya miaka kumi tunaweza kusogeza maji safi, salama na ya uhakika karibu kabisa na kaya zote nchini kote.

Nataka sasa niongelee kuhusu miundombinu. Suala hili lazima tulipe umuhimu wa kipekee. Uchumi wa  nchi unaendeshwa na miundombinu ya usafirishaji. Rais Kikwete amefanya kazi kubwa, hasa kwenye miundombinu ya barabara. Na naamini kwamba kabla hajamaliza muda wake ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kati. Kazi hii nzuri tutaiendeleza lakini tutaifanya kwa kazi zaidi na maarifa mapya. Barabara ambazo hazijaisha tutazimalizia na tutaanza nyingine mpya. Tutahusisha sekta binafsi katika ujenzi wa reli za kutoka Mtwara hadi Mchuchuma hadi Mbamba Bay. Pia tutafufua reli ya Tanga hadi Arusha na kuisogeza hadi Musoma. Bandari ya Mtwara itakuwa bandari kubwa ya uchumi wa gesi na chuma kutoka Liganga na makaa ya m awe kutoka Mchuchuma. Nimebahatika kufika kwenye bandari za Kemondo Bay, Mwanza, Nansio na Musoma kwenye Ziwa Victoria; bandari za Kigoma na Kasanga kwenye Ziwa Tanganyika; na bandari za Itungi, Manda, Liuli na Mbamba Bay kwenye Ziwa Nyasa. Hizo zote ni bandari za uchumi na zinahitaji matengenezo mapya makubwa. Kazi hii tutaifanya. Bandari ya Mwambani ambayo imeahidiwa kwa miaka mingi nayo tutaanza kuijenga kwa kushirikisha sekta binafsi.

Ndugu wananchi,

Nimezungumzia mambo mengi na mabadiliko makubwa ambayo tutayatekeleza. Ni dhahiri kwamba baadhi ya haya mambo yatahitaji rasilimali-fedha za Serikali kuyafanya. Kwa hakika hatuwezi kufanya mambo yote haya bila uwezo wa Serikali kuongezeka na uchumi kupanuka.

Kiongozi makini hawezi kuzungumzia mambo yote haya bila kuzungumzia rasilimali za kuyatekeleza. Tofauti na wenzangu, nataka  niwahakikishie kwamba ninazo fikra za namna ya kupata fedha za kufanya yote niliyoyazungumzia.

Kwanza, tutaihusisha sekta binafsi kwa kina zaidi kutekeleza ile miradi ambayo ni ya kimaendeleo lakini pia ni ya kibiashara ambapo Serikali haina ulazima kutumia fedha zake.

Kwa upande wa uwezo wa Serikali, nimefanya utafiti wa kina kupitia taarifa za Serikali, ripoti za Bunge na sekta binafsi kuhusu kuongeza uwezo wa Serikali kutimiza majukumu niliyoyaainisha. Serikali nitakayounda itafanya yafuatayo: (napenda kwa wale wenye calculator kwenye simu zao tupige hesabu kwa pamoja hapa)

Kwanza, bila kusita wala kuchelewa, nitapunguza misamaha ya kodi na kufikia kiwango cha asilimia 1 ya Pato la Taifa. Hatua hii itaiwezesha Serikali kupata zaidi ya shilingi bilioni 780 kwa mwaka.

Ili kuwaingiza walipa kodi wengi wapya, hasa kutoka sekta isiyo rasmi, Serikali yangu itapunguza kiwango cha mapato kwa mwaka kwa walipa kodi wadogo wanaolipa kodi kwa mtindo wa ukadiriaji. Hakuna mfanyabiashara atakayetozwa kodi kabla hajatengeneza faida. Lakini pia tutaweka adhabu kubwa kwa wataoshindwa kulipa kodi. Tutakamilisha vitambulisho vya taifa na anuani za makazi ili kuweza kuwatambua watu wote wanaofanya biashara na kuwatoza kodi. Hatua hizi itawezesha Serikali kupata fedha za ziada zaidi ya shilingi bilioni 860 kwa mwaka.

Tutaongeza ufanisi wa Mamlaka ya Kodi Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa za Kamati ya Spika Kuhusu Mapato na Matumizi Serikalini, TRA ikiongeza ufanisi kwa asilimia 10 tu, Serikali itapata mapato ya ziada ya shilingi bilioni 620 kwa mwaka. Kazi hiyo tutaifanya kwani sio ngumu. Na fedha hizo tutazipata.

Tutakapokamilisha mradi mkubwa wa kufua chuma wa Liganga, ifikapo mwaka 2020, Serikali itapata mapato ya shilingi bilioni 960. Tutakapokamilisha mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma, Serikali itaweza kupata zaidi ya shilingi bilioni 800.

Tutahakikisha kwamba ardhi yote inapimwa na kila mwenye ardhi anayo hati na anatozwa kodi stahiki. Hatua hii itaiwezesha Serikali kupata zaidi ya shilingi bilioni 520. 

Tukiwekeza kiasi kidogo cha fedha kwenye sekta ya nyuki na kudhibiti uvunaji na biashara haramu ya rasilimali za misitu, tutaweza kupata fedha za ziada zaidi ya shilingi bilioni 130.

Meli nyingi za kigeni zinavua samaki katika eneo letu bila kutozwa mrahaba, wala kukaguliwa, wala kutozwa faini. Tutarekebisha Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu na kuimarisha Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ili kuwezesha haya kufanyika. Hatua hii itaipatia Serikali mapato ya ziada ya zaidi ya shilingi bilioni 350.

Tutadhibiti biashara ya madini ya vito na kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya kazi kwa pamoja na urahisi na Mamlaka ya Ukaguzi wa Madini ili kuhakiki taarifa za mapato ya madini. Hatua hii itaiongezea Serikali mapato ya ziada ya zaidi ya shilingi bilioni 520.

Tutadhibiti uvujaji wa mapato yanayokusanywa katika ngazi za Halmashauri. Hatua hii itaweza kutupatia kipato cha zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka.

Sekta ya utalii kwa sasa inatuingizia shilingi karibu trilioni 3 kwa mwaka. Kwa mujibu wa taarifa ya kina ya Benki ya Dunia, ndani ya miaka kumi, sekta hii inaweza kuingiza shilingi trilioni 30 kwa mwaka. Ili tuzipate fedha hizo tunapaswa kufanya mambo manne yaliyo ndani ya uwezo wetu. Kwanza, kufungua, kuwekeza na kutangaza ukanda wa utalii wa kusini mwa Tanzania; pili, kuongeza aina na idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania na kuainisha vivutio vipya na mbadala na kuvitangaza. Tatu, kudhibiti mfumo wa kukusanya mapato ya utalii, ambayo mengi yanapotelea kwa wajanja wachache nchi au yanalipwa nje ya nchi kwa makampuni ya kitalii ya nje. Mambo haya tunayaweza, na tutayafanya ili tufikie lengo la mapato ya shilingi trilioni 30 kwa mwaka ili tuweze kufanya kazi kubwa tulizozianisha.

Pia, serikali ina mali na hisa kwenye biashara mbalimbali ambazo thamani yake ni zaidi ya shilingi trilioni 10. Tutaweka utaratibu mzuri zaidi kwa kufanya mabadiliko makubwa kwenye ofisi ya Msajili wa Hazina ili tunufaike na mali na hisa hizi. Pia, ndani ya miaka mitano, kwa hatua mbalimbali, tutayaingiza makampuni makuu manne ya Serikali kwenye masoko ya hisa – Shirika la Nyumba la Taifa, Shirika la Petroli Tanzania, Shirika la Reli la Taifa, Kampuni ya Simu ya Taifa na Shirika la Bandari Tanzania. Hatua hii itawezesha Watanzania kumiliki sehemu muhimu ya uchumi wa nchi lakini pia kupatikana mapato.

Ndugu Watanzania wenzangu,

Naweza kuendelea kuelezea ni kwa namna gani Serikali nitakayoiongoza itaweza kuongeza uwezo wake wa kutimiza majukumu niliyoyaainisha. Hapa bado sijagusia hatua za kubana matumizi ya Serikali ambazo pia fikra zake tunazo.

Tofauti na baadhi ya wenzangu waliotangulia kuzungumza, sijazungumzia mapato ya gesi kwa makusudi kwasababu ukweli ni kwamba Rais wa awamu ijayo, hata akiwa madarakani kwa miaka kumi, bado nchi yetu itakuwa haijaanza kupata fedha kutokana na gesi. Hata hivyo, ni muhimu kuendelea na maandalizi ya nchi yetu kunufaika na uchumi wa gesi.  

Na pia, tofauti na wenzangu, sijazungumzia kukopa au misaada ya wahisani kwa ajili ya maendeleo yetu. Ukweli ni kwamba tunao uwezo wa kufanya mambo yetu kwa kujitegemea huku tukidhibiti  deni letu la taifa. Ninachoweza kusema tu ni kwamba mambo haya nimeyafikiria kwa kina. Katika kutafakari ni kwa namna gani tutabadilisha hali za maisha ya watu wetu, sikukurupuka.

Inawezekana mambo niliyoyazungumza kwamba tutayafanya yakaonekana kuwa ni mengi na ni mzigo. Lakini waswahili wanasema tembo hashindwi na mkonga wake. Kama nilivyoonyesha, tunao uwezo kabisa wa kuyafanya. Katika nchi yetu yenye mahitaji mengi, hatuna anasa ya kuchagua kipi kiwe kwanza. Tunao wajibu kama viongozi wa ubunifu wa kufanya mambo yote ya msingi kwa wakati mmoja. Tunazo rasilimali na uwezo wa kuendeleza elimu na kilimo kwa wakati mmoja, tuna uwezo wa kumaliza matatizo ya madawati nchini, matatizo ya madawa katika hospitali zetu, matatizo ya mikopo kwa wanafunzi, matatizo ya maji, matatizo ya mishahara ya marupurupu ya wafanyakazi na mambo mengi ambayo Watanzania wanayatarajia kutoka katika Serikali yao.

Haya yote yatawezakana iwapo tutafumua na kusuka upya mfumo wa utumishi na utendaji wa Serikali ili kukomesha urasimu uliokithiri Serikalini, ili kurudisha nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma, ili kuongeza uwezekano na uharaka wa uwajibishaji wa watumishi wa umma wanaokiuka maadili ya kazi zao lakini pia ili kurudisha ari, morali na fahari na heshima kwa watumishi wa umma.

Lakini napenda nirudie, pamoja na yote haya, tiba ya uhakika ni kuutengeneza uchumi wetu ukue kwa namna ambayo inawajumuisha Watanzania wa hali zote.  Tiba ya uhakika ni kwa Watanzania kuumiliki uchumi wao na kuwa na nguvu ya kiuchumi ya kujiamulia hatma ya maisha yao. Serikali nitakayoiongoza italisimamia hili. Tiba kubwa ni nidhamu ya kazi na uwajibikaji wa kila mmoja wetu.

Nasimama mbele yenu nikiwa na bahati kubwa ya kupata malezi ya siasa na uongozi kwa viongozi waliotangulia wa nchi yetu. Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa aliyefahamu uwezo wangu na kunisaidia kupata elimu yangu ya Chuo Kuu na kuniwezesha kupata kazi Wizara ya Mambo ya Nje. Na, Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyeniona nikiwa naye Wizara ya Mambo ya Nje na kuniteua niwe Msaidizi wake kwenye kampeni za Urais mwaka 2005, ambapo nilizunguka naye nchi nzima tukizungumzia kero za Watanzania, na baadaye kuniteua kuwa Msaidizi wake Ikulu, ambapo nilipata fursa ya kuona na kujua nchi inaendeshwa vipi, kushiriki katika mikutano yake yote na viongozi wengine duniani na kuona diplomasia ya kimataifa inaendeshwa vipi, na kushiriki katika vikao vya Baraza la Mawaziri na kujua maamuzi makubwa ya nchi yanafanywa vipi.

Namshukuru pia Rais Kikwete kwa kunipa fursa ya kuwa kiongozi katika Chama chetu. Kwa kuwa Mjumbe wa Sektretarieti ya Chama, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, nimeshiriki kwenye uendeshaji wa shughuli za kila siku za Chama chetu na nimekijua vizuri Chama.  Nimejua uimara na udhaifu wake. Na nimeyajua yanayopaswa kufanywa ili kiendelee kuaminiwa na Watanzania.

Nawashukuru wananchi wa Bumbuli kwa kuniamini niwe Mbunge wao. Nawashukuru wa kunifanya nionekane na kuendelea kunipenda. Bado nina deni kubwa kwao kwa imani hiyo.
Napenda nifikie mwisho kwa kusema kwamba ninayo dhamira, uwezo, maarifa na ubunifu wa kuiongoza nchi yetu kukabiliana na changamoto mpya, za kizazi cha sasa, changamoto zinazohitaji maarifa mapya.

Naishukuru sana familia yangu, ikiwemo wazazi na ndugu na jamaa. Lakini zaidi mke wangu, ambaye tumekuwa wote sasa kwa miaka zaidi ya kumi, na watoto wetu wawili kwa upendo na uvumilivu.

Lakini kazi ya kuijenga nchi sio kazi ya mtu mmoja.  Kiongozi yoyote anayesema yeye ndio Masia na amekuja kama mkombozi wa taifa, atakuwa anawalaghai. Mafanikio yangu katika nafasi hii ninayoiomba na katika kutimiza majukumu yangu yanategemea ushiriki na ushirikiano wenu. Nachukua nafasi hii kuwaalika katika harakati hizi. Sigombei nafasi hii kupambana na mtu. Nagombea kupambana na changamoto za watu. Nikifanikiwa, nitasikiliza mawazo mazuri kutoka kwa kila mtu, hata ambao sio wana-CCM. Nitakuwa kiongozi wa watu wote – bila kujali dini zao, makabila yao, rangi zao, vyama vyao au kanda wanazotoka. Nitaongoza kwa namna ambayo Watanzania watajisikia fahari kuongozwa nami.

Sijawa kwenye siasa kwa miaka 30 au 40 kama baadhi ya wagombea, ambao wamepata fursa nyingi na madaraka makubwa ya kutekeleza yale wanayoyaahidi leo. Lakini nimekuwepo kwenye uongozi kiasi cha kutosha cha kujua matatizo yako wapi, nini cha kufanya, na namna ya kufanya, kama ambavyo nimeelezea kwa kirefu mchana huu.  Mkinipa nafasi hamtakuwa mnatumaini tu, bali mtakuwa mnaonyesha dhamira ya kutaka hakika ya mabadiliko makubwa.

Nafarijika kwamba kwenye Chama chetu wamejitokeza wagombea wengi. Hili ni jambo jema sana kwani kunaonesha ukomavu wa kidemokrasia. Lakini ni muhimu sote tukaelewa kwamba kugombea sio kugombana. Binafsi ndivyo ninavyoelewa na ndio maana sikutumia muda wenu kumshambulia mtu kwasababu jambo hili halisaidii Watanzania. Nina imani kubwa kwamba, kwa ukomavu wa Chama chetu, tutabaki wamoja na imara mara baada ya mchakato huu.  Chama chetu kina dhamana kubwa na kina historia adhimu barani Afrika. Dunia nzima inatazama mchakato huu wa ndani ya Chama chetu. Matumaini ya marafiki zetu na matumaini ya wanachama wetu ni kwamba tutachagua mgombea wetu kwa msingi wa kujiamini na sio kwa msingi wa woga wa kusambaratika.

Mkinichagua mimi kupeperusha bendera ya chama, nitatumia nguvu zangu zote na utajiri mkubwa wa hekima ndani ya chama chetu kuvunja makundi yote yaliyojitokeza kipindi hiki cha uchaguzi na kuwaunganisha wana-CCM wote.  Mwenyekiti wetu, Makamu Wenyeviti na Katibu Mkuu na Sekretarieti yake wamefanya kazi nzuri ya kukiimarisha Chama chetu na kukijengea uwezo. Nitakapokuwa kiongozi wa Chama chetu nitaanzia walipoishia. Nimekuwa chipukizi wa Chama hiki. Nimekuwa kiongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama hiki. Na nimefikia hadi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama chetu. Nafahamu changamoto za watendaji wa Chama na Jumuiya mikoani na wilayani. Wanafanya kazi kubwa. Nitawatazama. Nafahamu Wenyeviti wetu wa Mikoa na Wilaya, wana mahitaji mahsusi ya kufanya kazi zao za uongozi wa Chama chetu na usimamizi wa Ilani yetu katika ngazi zao. Nayajua hayo mahitaji. Naelewa majukumu mapya ya Wajumbe wa NEC yanahitaji uwezeshaji. Tutayazungumza na kuyafanya. Nafahamu Makatibu wa Siasa na Uenezi na Makatibu wa Uchumi na Fedha wa Mikoa na Wilaya wanafanya kazi kubwa na wanastahili kutambuliwa. Chama chetu kitakuwa salama chini ya uongozi wangu.

Tutaendelea na kazi nzuri inayofanywa sasa na viongozi wetu ya kukiimarisha Chama chetu ili kiendelee kuwa tumaini la Watanzania.

Nimalizie kwa kurudia kwamba sigombei nafasi hii kupambana na mtu bali kupambana na matatizo ya watu.  Nataka kushirikiana nanyi wote tuijenge Tanzania Mpya. Nataka uongozi wangu uwe mwanzo wa Tanzania Mpya, ya miaka 50 ijayo. Tunataka tujenge taifa la Watanzania ambao kila mmoja ana fursa, uwezo na nguvu ya kiuchumi ya kupata mahitaji yake na kuendesha maisha yake. Tunataka kujenga taifa ambalo wananchi hawabebi mzigo wa maisha unawaelemea. Tunataka kujenga taifa la watu wenye sauti na kauli juu ya Serikali yao.  Haya mambo sio ndoto. Yanawezekana kabisa.

Viongozi huwekwa na Mungu. Ninapoomba uongozi huu, namuomba Mungu anipe fursa ya kuwaongoza watu wake kupitia ridhaa yao. Kama mgombea, namuomba Mungu anipe uwezo, hekima na busara ya kupokea matakwa yake katika mchakato huu. Na kama kiongozi, namuomba anipe hekima ya kuwaongoza watu wake na kushughulikia mashauri yao kwa haki na ukweli.   

Na kubwa zaidi, namuomba Mungu aendelee kuibariki nchi yetu na watu wake.


Asanteni sana kwa kunisikiliza. 

January Makamba.

Juni 7, 2015.


1 comment:

Anonymous said...

He is very smart my future president of this republic