Monday, July 5, 2010

Time Has Arrived!TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nimewaiteni kwa mambo mawili. Kwanza, kuzindua kitabu nilichokiandika. Pili, kuzungumzia uvumi na minong’no kwamba natarajia kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Bumbuli.

Nianze na jambo la pili. Baada ya kutafakari kwa kina, na kuzungumza na wana-Bumbuli wenzangu, nimeamua niombe fursa ya kuwa sauti yao, kuwawakilisha na kuwasemea Bungeni, kuwatumikia na kushirikiana nao kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Jimboni kwetu.

Nimesukumwa na mambo gani?

1. Kwa muda mrefu, nimekuwa na hamu kubwa sana ya kushiriki mijadala ya msingi inayohusu mustakabali wa nchi yetu, nimekuwa na hamu ya kutoa mawazo yangu binafsi na kuyaweka hadharani, kuyaboresha kupitia mijadala na utafiti, na kuyatumia kubadilisha hali za maisha ya watu wa kwetu. Nimeonelea kwamba nafasi ya Ubunge itanipa fursa hii.

2. Naamini kwamba, baada ya kufanya kazi kwa karibu na Rais Kikwete, naweza kuchukua mfano wake kuitumia siasa vizuri zaidi kuitumikia nchi yangu kwa namna pana zaidi. Naamini naweza kushirikiana na vijana wenzangu, wa CCM na wasio wa CCM, kuifanya siasa iwavutie vijana wengi zaidi na ionekane kama ni sehemu ya utumishi wa umma.

3. Asilimia 72 ya Watanzania wana umri wa chini ya miaka 29. Mwaka huu, vijana waliozaliwa mwaka 1992 watapiga kura. Letu ni taifa la vijana. Inabidi ifike mahali vijana sasa wajitokeze kwenye nafasi za uongozi ili sura ya uongozi wa nchi ifanane na hali halisi ya nchi. Tutakapojitokeza wachache na tukafanikiwa, hata vijana wadogo zetu nao watakuwa na hamu ya kufuatilia siasa na tutakuwa hatujawapoteza katika kujihusisha masuala ya nchi na wengine wengi nao watajitokeza kwasababu wataona inawezekana. Hata hivyo ujana peke yake sio sifa ya uongozi.

4. Naamini uzoefu wangu kama Msaidizi wa Rais, kwa kuzunguka na Rais nchi nzima mara mbili, wakati anaomba kura na baada ya kuchaguliwa, ambapo nimelazimika kusoma ripoti za maendeleo za Wilaya karibu zote, ambapo, kama Msaidizi wa Rais, nimehudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, pamoja na mikutano mingine mingi ya kimataifa na ndani ya nchi, utanisaidia sana kuwa Mbunge mzuri. Naingia kwenye siasa nikiwa nimejifunza mengi kuhusu Serikali na jinsi inavyofanya kazi, nikiwa nimejifunza jinsi baadhi ya maeneo nchini yalivyopiga hatua za maendeleo na mbinu gani wametumia na wale ambao bado hawajapiga hatua ni mambo gani hawajafanya. Nitatumia elimu hii na uzoefu huu kushirikiana na watu wa kwetu Bumbuli kusukuma maendeleo mbele.

Sasa, kutamani Ubunge ni jambo moja, lakini kudhamiria kuwa Mbunge mzuri ni jambo jingine. Nimedhamiria kuwa mtumishi mzuri wa wananchi. Na nimeamua kuufanya mchakato huu wa kuwania Ubunge uwe tofauti kidogo.

Nimefanya utafiti wa kina kuhusu jimbo la Bumbuli. Nimezunguka na kuzungumza na watu wa makundi mbalimbali, vijana , wazee, kina-mama, viongizi, watendaji na wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya, walimu, viongozi wa vijiji na vitongoji. Nilitaka kujua matumaini yao, kero zao, karaha zao, na mambo yapi wanayatarajia kwa viongozi wao. Nilifanya semina ya siku mbili wa wana-Bumbuli karibu ishirini wanaowakilisha makundi mbalimbali, na tukazungumza kwa kina sana kuhusu masuala ya Bumbuli. Nilipata fursa ya kutazama kwa kina takwimu na taarifa mbalimbali zinazohusu maendeleo ya Jimbo. Nikafanya utafiti wa kina kuhusu dhana nzima ya maendeleo ya maeneo ya milimani. Matokeo ya yote haya ni hiki kitabu. Nimekiita Bumbuli: Jana, Leo na Kesho.

Nilidhani kwamba, kama mtu unaamua kugombea uongozi wa eneo fulani, na kama kweli una dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko kwenye eneo hilo, lazima ujiridhishe kama kweli unayajua mambo ya hapo mahali. Sio kuyajua tu juu juu kwa kuambiwa au kusikia. Uyajue kwa kina, kwa takwimu, na vielelezo na kwa kina. Huwezi kuzungumzia mabadiliko kama huna tarifa zote za kina kuhusu Jimbo lako. Hiki ndicho nilichofanya.

Kitabu nimekimegawanya katika sehemu tatu: Sehemu ya kwanza nimeiita Jana, ambapo tunaangalia historia ya Wasambaa na Usambara kwa ujumla. Historia na utamaduni vina nafasi kubwa kwenye mchakato wa maendeleo. Lazima tuyazingatie haya. Sehemu ya Pili, nimeiita Leo. Yaani Bumbuli ya leo ikoje? Changamoto ni zipi na fursa ni zipi. Na kwa kuzingatia hayo tunaanzaje. Sehemu ya tatu, nimeiita Kesho, ambapo sasa naelezea Bumbuli mpya inaweza kufananaje. Kitabu hiki kitakuwa na matoleo mawili: moja kwa lugha ya Kiswahili na jingine kwa lugha ya Kiingereza. Toleo la Kiswahili litatoka baada ya mwezi mmoja. Nimeamua kuandika kwa lugha ya Kiingereza pia kwasababu nadhani moja ya majukumu ya Mbunge ni kupanua wigo wa washirika wa maendeleo wa jimbo lako. Ningependa watu wengi muhimu na mashuhuri niliokutana nao wakati nasafiri na Rais nje ya nchi nao wapate kukisoma, na kutazama ni kwa namna gani wanaweza kusaidia.

Kwakuwa sasa sio wakati wa kampeni, sio vyema kutumia fursa hii kutoa ahadi ambazo zinaweza kutafsiriwa kama sehemu ya kampeni. Na kitabu hiki hakiongelei chochote kuhusu Ubunge wala Mbunge wala dhamira yangu ya kugombea. Kinatoa fursa kwa mtu yoyote - mwekezaji, mtalii, mtafiti na wengineo – kuifahamu vizuri Bumbuli.

Lakini kwa kuwa mimi nina dhamira ya kugombea Ubunge, nimetumia fursa ya kukiandika ili kujifunza, lakini pia nitakitumia kama mwongozo wangu.

Kwenye kitabu tunaona kwamba asilimia 90 ya wakati wa Bumbuli wanategemea kilimo. Hata hivyo, wakati Tanzania nzima wastani wa wakati kwa eneo ni watu 49 kwa kilomita moja ya mraba, Jimbo la Bumbuli wastani ni watu 309 kwa kilomita moja ya mraba, na wastani wa watu wanne wanalima katika hekta moja ya ardhi. Maana ya takwimu hizi ni kwamba watu wana vishamba vidogo sana, na uzalishaji ni mdogo na tija ni ndogo. Kwahiyo, ni muhimu kubadilisha hali hii. Nitashirikiana na wananchi kuhakikisha tunaongeza tija kwenye kilimo lakini vilevile tunajikita kwenye kuzalisha mazao yenye thamani kubwa zaidi, na kutafuta soko la maana la mazao ya wakulima.

Katika Wilaya ya Lushoto yenye majimbo matatu, zao la chai linalimwa kwenye Jimbo la Bumbuli pekee. Lakini ukiwatazama wakazi wa Bumbuli huwezi kujua kwamba wanalima zao lenye soko la dunia. Ukitazama kwenye kitabu nimejaribu kulinganisha kati ya mkulima wa chai Rungwe na yule wa Mponde, kule kwetu. Inasikitisha. Wastani wa bei ya majani mabichi ya chai kule Bumbuli ni shilingi 130 kwa kilo, wakati Rungwe ni karibu mara tano ya hiyo. Chai ni ile ile na mnada wa chai ni huo huo kule Mombasa. Wakulima wa chai Bumbuli wanatumia eneo kubwa zaidi kwa asilimia 40 kuliko wale wa Rungwe lakini tunazalisha kidogo zaidi – kwa tofauti ya kati ya kilo 200 hadi 330 za majani yaliyosindikwa kwa hekta. Utafiti wa mwaka 2008 unaonyesha kwamba asilimia karibu 20 ya mashamba ya chai yametelekezwa kwasababu wakulima hawaoni tena faida ya kulima chai. Nimeazimia kushirikiana na wananchi kupata ufumbuzi wa matatizo ya wakulima wa chai.

Tunaona kwamba huduma bado ni tatizo. Wakati wa mvua barabara nyingi hazipitiki na shughuli zinasimama. Watu wanashindwa kwenye kupekeka maiti kwa mazishi au kwenye kuhudhuria harusi au maulidi kwasababu barabara muhimu, kwa mfano ya Soni-Bumbuli, hazipitiki. Mbaya zaidi ni kwamba kule kwetu mvua ni karibu kila siku. Katika jimbo zima la Bumbuli hakuna hata tawi moja la Benki. Inawezekanaje mahali watu wanalima zao kubwa kama chai, wana biashara kubwa za mboga na matunda lakini hawana hata tawi moja la Benki. Matokeo yake ni kwamba hakuna mikopo, na hakuna huduma ya kuweka fedha. Hali hii lazima ibadilike. Lushoto nzima lipo tawi moja tu la Benki. Lakini ukiangalia mahesabu ya lile tawi, pesa zinazowekwa ni maradufu ya pesa zinazokopeshwa. Maana yake ni kwamba ile Benki iko pale kukomba pesa za eneo lile, eneo la watu ambao ni masikini, bila kutoa huduma za mikopo. Hili na lenyewe nitalitazama.

Kwenye elimu, bado ziko changamoto nyingi. Watoto wengi hawamalizi shule ya msingi. Mwaka huu, 2010, wanafunzi 1,286 hawakuingia darasa la saba kutokea darasa la sita, na kati hao, tofauti na sehemu nyingine nchini, wengi wao, karibu asilimia 71, ni wavulana. Lazima tumalize tatizo hili.

Serikali imejitajidi kujenga shule nyingi za Sekondari. Lakini bado mahitaji yapo. Hadi sasa, wanafunzi waliopo darasa la saba ni takriban 5,548. Kama wote wataingia kidato cha kwanza, yatatakiwa madarasa mapya karibu 160 na walimu wengi zaidi, jambo ambalo haliwezekani kwa muda uliopo. Lakini tukienda na mwenendo wa hali halisi, labda asilimia 8-10 ya wanafunzi hawa, yaani wanafunzi kati ya 450 hadi 550, ndio wataingia kidato cha kwanza, na nusu ya hawa ndio watamaliza sekondari. Je, hawa wengine wanaenda wapi? Nitakaa na wananchi wa Bumbuli na kuzungumza kwa kina kuhusu yote haya. Tunapaswa kuongeza shule za Sekondari na hata zile zilizopo zinapaswa kuimarishwa ili kuwa na hadhi na uwezo wa kutoa elimu bora. Katika Jimbo la Bumbuli hatuna shule hata moja ya kidato cha tano na sita. Hili tutalirekebisha.

Huduma ya afya na yenyewe bado haijawafikia wananchi wale kwa kiwango cha kuridhisha ingawa jitihada zimefanyika. Kwa kweli yapo mengi ambayo siwezi kuyamaliza kuyazungumzia yote. Lakini nimejiandaa vizuri. Nimefanya utafiti wa kina kuyajua matatizo ya Bumbuli, nimezungumza sana na watu wa Bumbuli, wazee kwa vijana, kina mama kwa watoto, wanyabiashara, viongozi wa dini, na viongozi wa vijiji na vitongoji, na wamenieleza mambo gani wanayatarajia, na mimi nimejiandaa kushirikiana nao kuyafanikisha.

Nawashukuru kwa kunisikiliza

January Makamba
5 Julai 2010

28 comments:

Faustine said...

January,
Safi sana! Nimependezwa na taarifa yako ya kutia nia kugombea nafasi ya ubunge huko Bumbuli.Taarifa hii ni nzuri iliyo na takwimu na ahadi zinazopimika.
Nimependezwa pia na staili yako ya kuja na kitabu ulichoandika.
Nakutakia kila la heri katika mchakato wako huko Bumbuli. Kaza buti!

Faustine

Anonymous said...

Go January Go, tumechoka na wazee wasio leta maendeleo,tunataka Viongozi wa kusaidia wananchi sio kwa kupata mkate bali kwa kuwafundisha namna ya kutafuta mkate, tunataka viongozi waona watatizo ya watoto wetu, tunataka viongozi kwenye muono namna ya kuwasaidia hawa watoto wetu tunaowabakiza nyuma(wasiochanguliwa kuendelea na masomo) na wao wanasaidiwa katika kujiletea maendeleo taifa haliwezi kuendelea kama tutakuwa tunaacha 40% ya watoto wote nyuma kila mwaka!

Anonymous said...

ila na wewe using'ang'anie huko na ukumbuke hiyo ni kazi ya mungu kwa hiyo huna hisa za kudum,,,i.e. uwe mfano kwamba 10 years itakutosha kama ni kuleta mabadiliko utakua umeshaleta hivyo uachie wengine wayaendeleze

Anonymous said...

January,
Nimekuwa nikifuatilia siasa za Bongo kwa muda mrefu. Mie sijawahi kukusikia, lakini baada ya kusoma muhtahsari wa habari hii, Nimeridhika kwamba vijana kama wewe ndio tunahitaji kuleta mageuzi ya msingi Tanzania. Umepambanua matatizo ya sehemu (Bumbuli) na umetumia takwimu kuorodhesha tatizo na kuidhinisha njia ambazo unadhani zinaweza kutatua matatizo. Very well put. Nakupigia saluti, tukipata vijana kama wewe 10 katika bunge we will see the positive change in no time. Tafadhali sana sana sana Usipoteze msisimko wa kusaidia jamii (Public service). Usiingie katika mitego ya rushwa zisizo na mpango bungeni. Kila la Heri!
--e,
Saint Louis, USA

Donny said...

Januari nakupongeza kwa hatua hii kubwa. Mungu atakuwa nawe. Lakini ujiandae maana yake wako watu wenye wivu, chuki, fitna, vinyongo ambao jambo hili litawauma moyoni kwa kuona unavyofanikia. Umaarufu vilevile unakuja na chuki. Utatukanwa na kuandamwa lakini usiogope kwani hao ni wachache wenye wivu na roho za kwanini na wivu wao unawatafuna mioyoni mwao watu wengi tupo nyuma yako. Jitahidi utimize ahadi zako/

Anonymous said...

Hongera sana January. Najua wananchi wa Bumbuli hawatafanya kosa, watakuchagua wewe. Mungu akutangulie katika mchakato huo.

Chambi Chachage said...

Hongera kwa kuzindua kitabu cha namna hiyo, je, kinapatikana wapi hapo Dar es Salaam?

Anonymous said...

Hongea mghoshi.
Nimefurahi kuona taarifa yako ya kutia nia ya kuchuikua lile jimbo la Bumbuli.
Naomba kabla hata ya kuwa mbunge ni kupe changamoto tatu ambazo zinanitatiza. Kwanza hawa vijana wa kiume wanaokimbilia mjini mara tu baada ya kumaliza darasa la saba,kwani wakati nipo class 6 watu walikuwa darasani hawaongelei suala lolote zaidi ya kukimbilia Dar baada tu ya mtihani wa kumaliza Darasa la saba na bado hili ni tatizo wilayani Lushoto ,sijui nyie kama mkiwa viongozi pamoja na wabunge wa majimbo ya Lushoto na Mlalo mtalichukuliaje hili.
La pili ni suala akina dada nao kwani wengi wanaolewa wakiwa wadogo sana 15-18/19 mbali na hapo wanasema watakuwa wamepitwa na wakati kwa kule Mtae/Sunga wanawaita "KANDO" hii inapelekea kila binti kutaka kuolewa kabla ya Kufikisha miaka 20.Hili ni Bonge la Tatizo.
La mwisho ni jinsi gani mtawasaidia hao wakulima hasa ukilinganisha na population yao na vijishamba wanavyomiliki hasa katika wakati huu wa mabadiliko ya hali ya hewa.

Vinginevyo nakutakia kila la Kheri kumuondosha Mh. Shelukinda

Emma said...

Hongera ndugu yetu. Mungu akutangulie akuepushe na mabaya na wabaya. Akupe uvumilivu na hekima. Emma, Sweden

chego said...

Hongera Bro! kwa kutangaza nia, Naomba uwe mwanamapinduzi wa kweli kama Che-guevara na si kuendekeza ufisadi na kuididimiza nchi yetu.

Emmanuel Tayari said...

Hizo Ndizo tunaita Siasa Pembuzi, Uwezo wa kutambua kwa kina Mizizi ya matatizo ya watu unaotaka kuwawakilisha.

Siasa zetu, zilijaa ahadi hewa kwa mda mwingi kwasababu watu wengi waliogombea nafasi za kisiasa hawakujali kufanya utafiti wa mizizi ya matatizo ya sehemu wanazoomba uwakilishi.

This is a step ahead in tearm of politics , which aim to tackle Mizizi ya Umaskini wa Mtanzania, ninakupongeza

Anonymous said...

hope you will make the change that is badly needed by the people of bumbuli and Tanzanian at large.

Hope you will make us proud of having "Mbunge Kijan"as we are proud of Zitto Kabwe

As politicians are all about whats left and whats right, I guess you will be more of whats wrongs and whats right

Mike Loe said...

all the best
tunatumai you will be able to walk the talk after wananchi give you their votes

Remigius said...

hongera bwana,
nilikuwa nasikia kuhusu ww kwa muda mrefu lakini nikadhani huna jipya ukizingatia kuwa ww ni mtoto wa makamba LAKINI niliposoma interview yako kwenye michuzi nafikiri ilikuwa mwisho wa mwaka jana NILISTAAJABU sana...tangu hapo nimekuwa na interest kubwa sana na kila unachokifanya. nimefuatilia articles zako zote unazopost kwenye blog yako na niseme ukweli ZIMESHIBA. kwa bahati mbaya tuu baadhi ya watu wanaweza kukupuuza kama nilivofanya hapo awali kwa kufikiri huyu yuko hapo kwa mgongo wa baba yake, LAKINI pole pole kila atakayepata kusikia hata sentence yako moja atakukubali.
binafsi nimekuwa na hamu ya kuwaona viongozi wenye vision awe kijana au mzee maana ndiyo maana ya kuongoza...na bahati mbaya tunao wengi viongozi vipofu na wanatupotosha kweli kweli lakini kwa judgement yangu inayokuja baada ya kukufatilia saana UNASTAHILI KUWA HATA WAZIRI
ninasikitika pia kuwa unagombania ktk jimbo ambalo mbunge wake nilimuona kama mtu makini pia LAKINI utafiti unaouelezea kwenye kitabu kama ni kweli basi UNAMSUTA.

mwisho ningeomba kitabu chako kiwe available kwenye amazon ili sisi tulio nje ya nchi tukipate pia ktk muda kabla ya uchaguzi

sala yangu ni kwako ni kwamba baada ya ubunge wako miaka mitano wana bumbuli na watz wote waseme kama kuna kitu KIKUBWA mzee makamba aliwahi kulifanyia taifa hili ni kumzaa JANUARY

Anonymous said...

Copies za hiki kitabu ‘BUMBULI’ zisije zikawa ‘sold out’, maana huko Beijing wa-chinese na wanafunzi wao walivyo wacheshi watamsoma ‘BUMBULI’ mapema mapema tu - ‘sold out’

ISACK said...

Januaari nimefurahi sana na uamuzi wako kuchukua hatua ya kushiriki kattika siasa ya Tz. Kinachonifurahisha zaidi ni staili ya kuandika kitabu kwani siku usipotimiza uliyoyandika ni rahisi sana kufanyiwa refence. Pamoja na kwamba mimi si mshabiki wa siasa za CCM lakini umenivutia kwa staili ya kisasa uliyotumia. Naomba usinaswe katika siasa chafu ya chama chako. Hakikisha unashirikiana na vijana wote wa Tz bila kujali itikadi ya za vyama vyao.

Nikupongeze sana kwa mwanzo huu mzuri.

salama said...

J,
It is indeed time for some savvy and fresh ideas, with people like you in political podium. There's no doubt that our country's political thermometer is going to increase and give people some sort of life and hope. Congrats on the book too, I'd love to have a copy.

All the best man!

Anonymous said...

Hongera sana January, tunahitaji vijana wenzetu kama wewe mtuongoze na kutupa moyo wa kulitumikia taifa. Nakutakia kila la kheri.

-S.R.

Anonymous said...

Januari hongera, ujio wako ni kama wa OBAMA, tunasubiri hiyo CHANGE.

Majaliwa said...

Januari hongera sana kwa kuzindua kitabu na kwa kujitosa kugombania Ubunge Bumbuli.

Kwa kweli - ukishinda au ukishindwa - ni baraka kubwa kwa nchi yetu pale vijana wenye uwezo wanapotamani kushika nafasi za uongozi:it speaks volumes for us as Tanzanians. Na ingawaje mimi ni mpenzi wa vyama vya upinzani (CHADEMA) nimefurahi na kuguswa sana kwa jambo hili,our country will be all the better if both sides of parliaments are able to produce quality candidates.Naamini utatoa mchango mkubwa katika ushindani wa sera za kuing'oa nchi kutoka kwa umasikini huu ambao bado unatukera after 49 years of CCM governance.

Mwishi ni kukusihii ukazane usinase kwenye mtego wa ufisadi kama ukifanikiwa kufika Dodoma.Daima: "9Upendo wako (kwa wana-Bumbuli na Watanzania pamoja na binadamu wote) uwe wa kweli. Chukia uovu, shikilia yaliyo mema. 10Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa kindugu. Waheshimuni wengine kuliko mnavyojiheshimu wenyewe".Warumi 12:9-10.

Majaliwa

January Makamba said...

Kuanzia Dr. Faustine, na wengineo wote, nawashukuru sana kwa ushauri, mawazo, changamoto na sapoti. Nitayazingatia yote. Nawaahidi kwamba sitawaangusha.

Foundation For Environmental Management and Campaign Against Poverty(FEMAPO) said...

January sikufahamu personally lakini, nimekufahamu kwa mawazo yako ya kina kuhusu MBUMBULI ni wabunge wangapi wanayafahamu majimbo yao kwa kina kiasi hiki? Wewe ni kijana makini, tunaomba vijana wote na wezako wote mtakaoingia bungeni mwaka huu, mkaanzishe kampeni kabambe ya kuhakikisha bunge la mwaka 2015 linakuwa na histoiria ya kuwa na vijana wengi kwa ajili ya kutengezena Tanzania mpya, maana kila kijana akilifanya jimbo lake jipya ndo kuifanya tanzania kuwa mpya!

All the best nategemea kukutana na wewe ukiwa mbunge!

Habib Mbwana Ali said...

January,
Mimi ni mzaliwa wa Tanzania lakini nilichukua uraia wa nchi jirani ya Kenya.Ningependa kukupongeza sana kwa ujasiri uliotuonyesha sisi kama vijana.Hata huku kwetu Kenya, vijana wameanza kujitosa katika ulingo wa siasa.Ningependa kuwahusia wakaazi wote wa Bumbuli mumpe Janury kura zenu.
Nakutakia kila la heri January.......

Anonymous said...

Hongera January kwa uamuzi wako thabiti wa kuwania ubunge jimbo la Bumbuli.tambua kuwa umekuwa mfano wa kuigwa na vijana wengi,kwani tunahitaji mabadiliko makubwa ya kutokuwa na hofu katika kuwania ngazi hizi kubwa za uongozi katika taifa letu.HONGERA SANA.Alphonce A.K kutoka MWANZA.

Anonymous said...

Hongera January uamuzi mzuri wa kuwania ubunge jimbo la Bumbuli.

Steve said...

January,
You are born to do this. Bumbuli should be so happy to have someone like you as their representative.
It's about time for the Bunge of Tanzania to have fresh blood with new ideas.
I support you 100%, just keep up the good work and the spirit of helping others.
I wish you all the best, will be here if you need some campaign managers for free.

Steve,
NH.

Anonymous said...

I think it is about TIME, for the young, energetic, ambitious leaders to take our country foward.

and to be honest with you January, given the current climate, and you as individual who is fortunate enough to walk through houses of power at such a young age, these two factors make you a perfect candidate, in RESETTING the button on how politics should BE DONE!

And it is our hope that, this country will emerge as cruddle of Democracy in Eastern and Central Africa, if we(vijana) are given a chance and listened to!

You need to realize that, people of Bumbuli na wananchi wote kwa ujumla, watakuangalia how you model yourself as a politician, au Biashara ndio ile ile, kwa maneno ya mtaani. I am sure you had time to reflect on that. Ni kazi ngumu kwa kweli.

Wish you all the best!

Anonymous said...

Good Vision.. lakini wasiwasi wangu ni ule ule tu kua.. kila mtu anapoingia katika kinyang'anyiro cha kutafuta nafasi ya uongozi hasa wa kisiasa ari huwa ya juu sana na hivyo kumsababisha atoe matumaini makubwa amboyo pengine ni vigumu kutekelezeka wakati akiingia kwenye uhalisia ( Uongozi wenyewe)...pengine wananchi wa bamburi wanaweza wasijue rangi yako halisi kwa kipindi hiki ...labda january huyu anayezungumza maneno matamu na yenye matumaini mapya siye yule ambaye watamuona baada ya kuyapata hayo madaraka ( kama viongozi wengi wa hii nchi walivyo) ..mimi na kuasa tu kijana mwezangu..onyesha mfano ambao umekosekana kuonyeshwa kwa miaka nenda rudi katika hii nchi...wewe ni kijana na ur too ambitious and i know u can do all you have planned to do in your area...please na nakusisitizia hili Please WALK THE TALK...and you will be a new icon for the youth leaders na vijana wote kwa ujumla pamoja na wananchi and in you utaleta mtazamo mpya wa uongozi...mimi si wa bumbuli but for now na after umetoa hiki kitabu..all eyes will be on you hasa kwa sisi vijana..hatutapenda na nafikiri utaharibu sana (njia nzuri ambayo sasa unakwenda kuianza kuijenga ya mtazamo mpya wa uongozi mpya wa vijana wanaosimamia maneno wanayoyaongea kwa vitendo) kama utaishia kwenye mitego ya ufisadi na kusahau maendeleo ya jimbo lako na taifa lako kwa ujumla...utatuangusha na vijana tutapoteza trust tena kwa wananchi..hatutaki kufika huko..tumekwisha anza ku win mioyo ya wananchi na wewe pamoja na vijana wengine ( mnaoelekea katika michakato ya kuelekea kwenye UONGOZI hasa wa kisiasa) ndio kama makamanda wetu wakutuzidishia waumini katika hili watakaokua na imani zaidi ya uongozi wa vijana..na hapo ndipo Tanzania itakapo anza kubadilika...Usituangushe.!

Mdau ..Ken

sidevok@gmail.com