Thursday, July 17, 2014

Asanteni sana!


Naomba kurudia kutoa shukrani zangu za dhati kwa wale wote miongoni mwenu, wake kwa waume, wazee kwa vijana, walionitumia ujumbe na salamu kutoka pande zote za nchi - kwa kupiga simu, kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu na kupitia mitandao ya kijamii - kueleza kufurahishwa kwao na uamuzi wangu wa asilimia 90 kutaka kujitokeza kugombea Urais wa Taifa letu pale muda utakapowadia, na kwa mujibu wa taratibu za Chama chetu cha CCM..

Nimepokea salamu nyingi sana za kunitia moyo katika kipindi hiki ninapoendelea kujitathmini na kupata nasaha, baraka na ushauri kutoka kwa wazee wetu, viongozi wetu wa zamani na wa sasa, na viongozi wetu wa dini. Nafarijika sana kwamba wengi wenu mmeupokea uamuzi wangu kwa furaha sana. Tueendelee kuwa pamoja na naahidi sitawaangusha. Tukifanikiwa, na wakati utakapofika, tutaendesha kampeni ya kihistoria itakayotoa matumaini mapya kwa Tanzania mpya. Tutawashangaza wale wanaoamini kwamba hatuwezi au tunajaribu tu.

Pia nimesoma na kuyapokea kwa moyo mkunjufu maoni ya baadhi yenu, ambao kwa namna moja au nyingine hamkupendezwa na uamuzi wangu. Hata nyie, kama ilivyo kwa Watanzania wote, mnayo haki na uhuru wa kutoa maoni yenu. Naahidi kuyazingatia na kuyafanyia kazi maoni na mawazo yenu, hasa yale yenye kujenga na kuimarisha mjadala juu ya Tanzania tuipendayo.

Najua wengi mna shauku kubwa ya kufahamu kwa mapana na marefu mawazo yangu juu ya namna gani tunaweza kuibadili nchi yetu kuwa bora zaidi. Kwa sasa naomba subira kidogo kutoka kwenu. Wakati muafaka ukiwadia, nitaeleza kwa mapana na marefu fikra zangu kuhusu Tanzania mpya tuitakayo. Mjadala wa kuhusu aina ya uongozi tunaoutaka na sifa za Rais atakayefuata, pamoja na mahitaji ya nchi yetu ni mjadala bora zaidi kuliko mjadala unaendelea sasa wa majina ya wagombea Urais au ule mjadala wa "vijana dhidi ya wazee". Nchi yetu hii ni nchi yetu wote bila kujali umri. Tunapoongelea kuhusu nia na haja ya kuwa na uongozi wa kizazi kipya hatumaanishi kwamba hiyo ndiyo sifa pekee ya Urais kama baadhi wanavyotaka ieleweke.

Nchi yetu ina changamoto nyingi lakini bado ni nchi nzuri na mfano wa kuigwa hapa Afrika. Wapo viongozi waliotangulia ambao wamefanya tuwe na sifa hii. Wazee wetu ni hazina katika Taifa letu na wataendelea kushirikishwa katika ujenzi wa nchi yetu. Ili kuleta fikra mpya, maarifa mapya na majawabu mapya kwa changamoto mahsusi za zama hizi, wengi wetu tunaamini wakati umewadia sasa wa kupokezana kijiti kutoka kizazi kimoja hadi kingine cha uongozi, na siyo kizazi hicho hicho kimoja kupokezana kijiti. Na wala hili sio jambo la ajabu kwasababu huu ndio umekuwa utamaduni wetu katika awamu zote. Kila kizazi kina changamoto zake na kina wajibu wake. Wakati umewadia kwa kizazi cha sasa kushika usukani ili nacho kitengeneze mustakabali wake mpya badala ya kuendelea kutumiwa na wanasiasa kama daraja tu wakati wa kuomba kura na baadaye kuwekwa kando katika maamuzi makubwa yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.

Pia, wakati tukitumia haki yetu ya kujadili kuhusu Rais ajaye, ni muhimu kutambua kwamba nchi yetu inaye Rais sasa hivi mwenye mamlaka kamili na ridhaa kubwa ya wananchi – na lazima aheshimiwe na apewe nafasi ya kufanya kazi yake. Ningependa kurudia shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dr. Jakaya Kikwete kwa ziara yake aliyoifanya wiki iliyopita jimboni kwetu Bumbuli kukagua shughuli za maendeleo na kuhimiza utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM. Namshukuru sana kwa maneno yake ya busara, yaliyojaa hekima na yenye kutia moyo aliyoyasema juu yangu.

Mwisho, nawasihi sana wapenzi na mashabiki wangu kujiepusha na malumbano yasiyo na msingi, hasa hasa wale wanaotumia jina langu kufanya hiyo. Tuwe wavumilivu wa mawazo yaliyo tofauti na yetu. Hiyo ndiyo njia pekee ya kupanua demokrasia yetu. Tujenge hoja zaidi badala ya kulipiza dhihaka juu yangu kwa kutoa dhihaka juu ya wagombea wengine au kutoa dhihaka kwa wazee wetu kwa ujumla. Hata hivyo msiache kunisemea pale mnapoona kuna njama za makusudi za kupindisha ukweli juu yangu na juu ya makusudio yangu. Kuomba uongozi ni kuomba utumishi. Sio mapambano. Sio suala la kufa na kupona. Unaomba kibali kwa Mungu kuwaongoza watu wake kupitia ridhaa yao. Tusisahau kumuomba Mungu atupatie kiongozi mzuri mwenye hekima na atakayetenda haki kwa watu wote.
Asanteni sana.
Pamoja tunaweza.
January Makamba (MB),
17-7-2014