Friday, April 27, 2018

Muungano Wetu na Kisa Cha Nyimbo Mbili

Muungano Wetu na Kisa Cha Nyimbo Mbili.

Na January Makamba

Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, ambazo nilishiriki kama Msaidizi wa Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Ndugu Jakaya Kikwete, hoja ya uzalendo na urithi wa Mwalimu Nyerere kwa taifa letu ilichukua nafasi kubwa. Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwenye uchaguzi ule, Ndugu Freeman Mbowe, katika mikutano yake  ya kampeni, alimtaja sana Mwalimu Nyerere, alitumia sana bendera ya taifa na  alikuwa akiwaimbisha wananchi wimbo wa taifa. Hata hivyo, katika kuimbisha wananchi wimbo wa taifa, aliwaeleza kwamba wimbo huo umekosewa kwenye mpangilio wa beti: kwamba ubeti wa pili ulipaswa kuwa ndio ubeti wa kwanza. Kama mnavyofahamu, kwenye mstari wa kwanza kabisa wa wimbo wetu wa taifa, tunamuomba Mungu aibariki Afrika. Ubeti mzima wa kwanza wa wimbo wetu wa taifa unahusu Afrika. Tanzania tunaikumbuka kwenye ubeti wa pili. Afrika imetajwa mara tano kwenye wimbo wetu.

Hoja ya Ndugu Mbowe ilikuwa ni kwamba lazima tuwe wazalendo kwa kuiweka Tanzania mbele. Kwahiyo, lazima ubeti wa pili unaoanza na “Mungu Ibariki Tanzania” uwe ndio ubeti wa kwanza. Watu wengi, hasa vijana, wakawa wanaona mantiki katika hoja yake.

Hata hivyo, baadhi yetu katika timu ya kampeni ya CCM tukaona kwamba Ndugu Mbowe amekosa uelewa wa msingi muhimu wa kutafuta uhuru wetu na kujenga taifa letu. Tukaamua kumjibu tukieleza kwamba haelewi historia ya Tanzania wala urithi wake. Tukatoa sababu. Na mjadala wa mpangilio wa beti za wimbo wetu wa taifa ukafa. Hata hivyo, wakati tunaadhimisha miaka 54 ya Muungano wetu, ambao ni utambulisho wa nchi yetu, kielelezo cha utaifa wetu, na kilele cha umoja wetu, ni muhimu kukumbushana kidogo.

Wimbo wa taifa hutungwa kwa umakini na hupitishwa baada ya tafakari kubwa na muafaka mpana. Wimbo wa taifa hubeba utambulisho, utashi na ndoto za taifa husika.

Wimbo wetu wa taifa umeitanguliza Afrika kabla ya Tanzania na umeutaja umoja kama moja ya ngao zetu kuu. Hili halikutokea kwa ajali. Wakati wa harakati za kutafuta uhuru wetu, moja ya shabaha yetu ilikuwa ni kupata uwezo wa kuharakisha maendeleo yetu lakini pia kutimiza azma yetu ya kuungana kama Waafrika. Kuanzia miaka ya 1930, kulikuwa na mwamko mkubwa wa Umajumui wa Afrika ambao ulijidhihirisha pia kupitia ushirikiano kwenye harakati za kutafuta ukombozi wa bara la Afrika. Kama Tanganyika, tulikuwa tayari kuchelewesha uhuru wetu ili tuupate siku moja na majirani zetu na siku hiyo hiyo tutangaze Jamhuri moja. Hata tulipopata uhuru wetu, tulitangaza kwamba uhuru huo haujakamilika hadi pale Afrika nzima itakapokuwa huru. Na tukaimba kwamba tunataka kuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro ili pia ukamulike na kutoa matumaini hadi nje ya mipaka yetu. Na tukaikwangua hazina yetu, na kumwaga damu ya vijana wetu, kwa ajili ya ukombozi wa Afrika. Heshima ya nchi yetu ikapaa.

Kwahiyo, umoja wa Afrika na baina ya Waafrika, ni sehemu ya urithi wetu kama taifa na ni ngao yetu, kama tunavyoimba kwenye wimbo wetu wa taifa. Kwahiyo, msingi wa kwanza wa Muungano wetu ni huu. Dhamira ya Waafrika kujumuisha nguvu zao ili kujilinda kwa uhakika zaidi na kupata maendeleo na ustawi wao kwa kasi zaidi.  

Muungano wetu ni kielelezo pekee kilicho hai kinachoonyesha ujasiri na uthubutu wa Watanzania kutimiza kwa vitendo dhamira ambayo Afrika nzima imekuwa inailezea kwa maneno. Katika mambo yanayopaswa kutupa fahari na kutufanya Watanzania tutembee kifua mbele ni Muungano wetu. Ndio maana wimbo wetu upo na umebaki kama ulivyo kwasababu umoja ni urithi na ngao yetu, na umoja wetu umedhihirishwa na kuthibitishwa na Muungano wetu.

Nitaongelea wimbo wa pili. Unaitwa “Tazama ramani”. Ni kweli ukitazama ramani utaona nchi nzuri inayoitwa Tanzania. Lakini uzuri wa nchi yetu sio tu wa milima, mito na mabonde kama tunavyoimba. Bali pia ni wa mipaka yake. Sote tunajua kwamba mipaka ya nchi za Afrika haikutengenezwa na Waafrika wenyewe. Wakoloni walikaa kikao huko Berlin, Ujerumani kuanzia mwezi Novemba 1884 hadi Februari 1885 ili kumegeana vipande vya ardhi ya Afrika na kuchora mipaka kwenye vipande hivyo. Hivyo vipande leo ndio vinaitwa nchi huru za Afrika. Kama Mtanzania, faraja unayoipata, au unayopaswa kuipata, ukitazama ramani, ni kwamba, kwa Tanganyika na Zanzibar kuungana, mipaka ya Tanzania tumeitengeneza wenyewe. Ni jeuri kubwa tumefanya. Tumenajisi yatokanayo na mkutano dhalimu wa Berlin. Moja ya sababu kubwa ya Tanzania kuheshimika duniani ni jeuri hii kubwa. Na moja ya njia za haraka na za uhakika za kujivua nguo na kujiondolea heshima yetu ni kuufanya Muungano uzorote, ulegee na uvunjike.

Hata hivyo, nikiri kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukuwa mgumu kutokea kwasababu ya maingiliano ya kibiashara na kijamii ya karne kadhaa baina ya watu wa pande hizi mbili. Hata kabla ya watawala wa kigeni kuingia katika maeneo yetu, tayari kulikuwa na muungano, tena wa damu kabisa, wa watu wa pande zetu mbili. Kwa kifupi, Muungano wetu tunaodhimisha miaka 54 ya kuundwa kwake, ulirasimisha tu udugu uliokuwepo. Kwahiyo, msingi mwingine mkuu wa Muungano wetu ni udugu na ujamaa wa karne nyingi baina ya watu wa pande mbili. Huu ni msingi imara, inawezekana hata zaidi ya mifumo na miundo ya kitaasisi iliyowezesha Muungano wetu kudumu kwa miaka 54 sasa.

Je, Muungano wetu unaweza kuwa imara zaidi? Bila shaka. Ndio maana kila uchao jitihada zinafanywa na Serikali za pande zote mbili kurekebisha mambo yatakayosaidia kuuimarisha zaidi. Bahati mbaya mjadala kuhusu Muungano mara nyingi umekuwa kwenye yale mambo yanayoitwa “Kero za Muungano”, ambayo jina sahihi ni Changamoto za Masuala ya Muungano. Kwa upande mmoja hili ni jambo jema kwasababu linaonyesha hamu na dhamira ya kukabiliana na masuala yanayoweza kudhoofisha Muungano wetu. Kwa upande mwingine, msisitizo kwenye kero unaondoa uwezo wa kuona fursa za ustawi zilizopo katika Muungano na unaondoa uwezo wetu wa kujivunia mambo mengi mazuri na mafanikio makubwa yaliyotokana na uwepo wa Muungano wetu. Kuimarisha Muungano ni sehemu ya ujenzi wa taifa letu. Ujenzi wa taifa haukumalizwa siku Muungano umeundwa. Kimsingi siku hiyo ilikuwa ni siku ya kusimika msingi. Kazi ya ujenzi wa taifa letu ni endelevu. Na kuondoa changamoto za Muungano ni sehemu ya kazi adhimu kabisa ya ujenzi wa taifa letu.  

Muungano wetu umeleta ustawi mkubwa wa watu wa pande mbili. Tanzania ya leo sio ya mwaka 1964. Usalama wa nchi yetu umeimarika. Fursa zimefunguka. Kwa mfano, wapo watu wengi kutoka Tanzania Bara walioajiriwa kwenye mahoteli mengi ya kitalii Zanzibar. Pia, Wazanzibari wanaoishi na kufanya kazi au biashara Tanzania Bara ni wengi kuliko Wazanzibari wote wanaoishi kwenye kisiwa cha Pemba. Hili ni jambo jema. Na mwenendo na takwimu za kidemografia zinaonyesha kwamba katika miongo miwili au mitatu, Wazanzibari wengi zaidi watakuwa wanaishi Tanzania Bara kuliko walioko Zanzibar. Hili pia ni jambo jema kwasababu moja ya  shabaha za Muungano ni uwezo wa watu wa pande zote mbili kuishi na kushamiri kwenye upande wowote wa Muungano.  Naamini kabisa kwamba Muungano wetu unayo nafasi kubwa zaidi ya kuleta ustawi mpana zaidi wa watu wa pande zote mbili.

Naamini kabisa yapo mambo ya kurekebisha ili kuongeza uwezekano huo. Katika mambo Serikali ya Awamu ya Tano tunayoendelea kuyashughulikia ni pamoja na uwezo wa magari yaliyosajiliwa Zanzibar kutembea Bara, na magari yaliyosajiliwa Bara kutembea Zanzibar, bila bughudha. Siamini kabisa kwamba ni sahihi kwamba mtu mwenye gari lenye namba za nchi ya jirani atembee nalo bila bughudha lakini gari lenye namba za Zanzibar likionekana Bara likamatwe na kushindwa kutembea.  Pia tunajua na tunafuatilia masuala ya kuhuisha mifumo ya ukadiriaji kodi na utendaji wa baadhi ya watumishi kwenye bandari zetu ili kuondosha kabisa usumbufu wanaopata wananchi wa kawaida wanaposafiri na kusafirisha mizigo yao kati ya pande hizi mbili.

Naamini kwamba moja ya mantiki ya kuwa ni Muungano ni kwamba ni lazima iwe rahisi, haraka na nafuu kufanya biashara, kupata masoko na kusafirisha bidhaa kati ya pande mbili za Muungano. Kwa uhalisia, maendeleo ya viwanda na uchumi ya Zanzibar yatafikiwa iwapo Zanzibar itakuwa na uwezo wa kulifikia soko la Bara kwa bidhaa haswa zinazozalishwa Zanzibar. Tunafanyia kazi kwa bidii kubwa masuala yanayoonekana kama ni vikwazo vya biashara kati ya pande mbili za Muungano. Binafsi nimewafuata na kuzungumza mara kadhaa na wafanyabiashara wa Zanzibar chini ya umoja wao na taasisi zao. Nimemfuata na kukaa vikao virefu na Waziri wa Biashara wa Zanzibar kuzungumzia masuala ya biashara. Nimemfuata na kukaa na Waziri wa Fedha wa Zanzibar. Waziri wa Biashara wa Serikali ya Muungano amekaa na Waziri wa Biashara wa Zanzibar na wataalam wao. Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameitisha na kuongoza vikao vya kisekta vya sekta za Biashara, Fedha na Uchukuzi wa pande zote mbili.

Tunaamini kabisa kwamba masuala ya muda mrefu, yakiwemo utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha, ambayo yatatatua changamoto nyingi za masuala ya kifedha, yanastahili kupatiwa ufumbuzi na bahati nzuri hatua nzuri imefikiwa kwenye masuala hayo.

Ni muhimu kutambua kwamba hakuna kero au changamoto yoyote ya Muungano inayoweza kuondosha uhalali wala umuhimu wa Muungano. Na ni muhimu kutambua haitakuja kutokea siku kwamba hatuna la kufanya katika kuboresha na kuimarisha Muungano wetu. Kazi ya kujenga nchi na kuimarisha Muungano wetu ni ya kudumu. Faraja tunayopata ni kwamba, kwa sasa, kwa watu wa itikadi mbalimbali za kisiasa, na kwa watu wa pande mbili za Muungano, mjadala na hoja sio tena uhalali wa Muungano bali mjadala upo kwenye namna bora zaidi ya kuuimarisha. Wapo wachache ambao watabaki kujadili jinsi ulivyoafikiwa. Katika mambo makubwa ya kihistoria duniani, watu wa kuhoji yalivyotokea na kama kweli yalitokea hawawezi kukosekana.

Muungano wetu utaimarishwa kama tutauongelea tukiwa na vichwa na nyoyo tulivu huku tukitambua kwamba ni urithi adhimu kabisa. Kunyoosheana vidole au kuitana majina au kushambuliana hakuna msaada wala manufaa. Nasikitishwa na baadhi ya kauli za kushambuliana, wakati mwingine zinazotolewa Bungeni kuhusu upande mmoja au mwingine wa Muungano. Hakuna sababu ya kudharauliana na kupuuzana. Kila upande wa Muungano na umuhimu wake. Falsafa yangu mimi niliyeaminiwa katika dawati hili la Muungano, ni kusikiliza kila mtu bila kumhukumu wala kumshambulia wala kuhoji uzalendo wake na mapenzi yake kwa Muungano wetu na nchi yetu. Ninaamini, ukiondoa watu wachache sana, kila anayesimama kuongelea Muungano anataka uwe bora zaidi na imara zaidi. Wajibu wetu ni kusikiliza. Aliyeshika dawati hili kabla yangu, ambaye sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Rais, amenifunda vizuri kuhusu namna ya kushughulikia masuala haya. Napata pia miongozo na maelekezo murua na fasaha kutoka kwa viongozi wakuu akiwemo Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Raisi wa Zanzibar Mheshimiwa Ali Mohammed Shein; na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa; Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idi. Nafanya kazi vizuri na Mawaziri wenzangu wa Zanzibar, hasa Waziri Mohammed Aboud Mohammed.  Nafarijika kwamba michango mingi ya Wajumbe kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar mingi ni ya kujenga na kuimarisha Muungano.

Kuna siku sitakuwa na kazi hii ninayoifanya sasa. Kuna siku watu wote tuliopo tutaondoka hapa duniani. Wajibu wetu ni kuwaachia watoto wetu na wajukuu wa wajukuu zao Muungano ukiwa imara zaidi kuliko ulivyo sasa. Nchi hii hatukuirithi kutoka kwa waliotangulia, bali tumeiazima kutoka kwa wanaokuja baada yetu. Ukiazima kitu kanuni ni kukirejesha kikiwa salama. Muhimu tukairejesha nchi yetu na Muungano wetu kwa wanaokuja ukiwa salama.


January Makamba, mwandishi wa makala hii, ni Mbunge wa Bumbuli na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)