HOJA BINAFSI YA NDUGU JANUARY MAKAMBA (CCM – BUMBULI) KUHUSU SHERIA YA UDHIBITI WA SHUGHULI ZA UPANGAJI NYUMBA ZA MAKAZI (RENTAL HOUSING ACT)
9 Februari, 2012
Mheshimiwa Spika,
Nakushukuru kwa kunipa fursa na heshima ya kuwasilisha hoja hii katika Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Hoja yangu ina madhumuni ya kuliomba Bunge lako tukufu liazimie, kwa kauli moja, kuitaka Serikali, katika Mkutano ujao wa Saba wa Bunge, kuleta Muswada wa Sheria ya Kudhibiti Upangaji wa Nyumba za Makazi (Rental Housing Act):
1. Itakayoweka utaratibu na udhibiti wa sekta ya upangaji wa nyumba nchini kwa ujumla;
2. Itakayowezesha kuanzishwa kwa Wakala wa Udhibiti wa Sekta ya Nyumba – Real Estate Regulatory Authority (RERA).
3. Itakayoainisha wazi haki na wajibu wa wapangaji na wenye nyumba;
4. Itakayoweka utaratibu wa haraka na rahisi zaidi kwa wapangaji na wenye nyumba kupata haki zao;
5. Itakayodhibiti na kuweka adhabu kwa vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wapangaji;
6. Itakayoweka utaratibu wa ukaguzi wa viwango na hali za makazi ya kupanga;
7. Itakayozuia na kuweka adhabu kwa utaratibu wa kutoza kodi ya nyumba kwa miezi sita au mwaka mzima;
8. Itakayodhibiti wenye nyumba kuwalazimisha wapangaji kulipa kodi ya nyumba kwa fedha za kigeni, hasa dola za kimarekani;
9. Itakayodhibiti upandishaji holela wa kodi za nyumba;
10. Itakayowezesha mikataba ya upangaji wa nyumba kusajiliwa;
11. Itakayoweka utaratibu wa kuwatambua na kuwasajili madalali wa nyumba ili kudhibiti vitendo vyao.
12. Itakayoiwezesha Serikali kupata mapato kutokana na biashara ya upangaji nyumba kwa kuwalazimisha wenye nyumba kujisajili kwenye Mamlaka husika na kutoa risiti kwa wapangaji;
13. Itakayoweka taratibu nyingine mbalimbali zitakazolinda haki za wapangaji na wenye nyumba na zitakazowezesha sekta ya makazi kukua na kushamiri na kupunguza tatizo la makazi nchini.
Mheshimiwa Spika,
Msingi wa hoja hii ni malalamiko mengi ambayo mimi na ninyi viongozi wenzangu mmekuwa mkiyapata kutoka wananchi wengi hasa waishio mijini kutokana na adha wanazopata katika kutafuta nyumba za kupanga au kuishi kwenye nyumba za kupanga.
Mheshimiwa Spika,
Naomba uniruhusu nitoe mifano hai ya baadhi ya watu walionifuata na kunielezea masaibu yao.
Dora, ni binti wa miaka 30, ni mwandishi wa habari. Alipomaliza Chuo Kikuu alibahatika kupata kazi kwenye gazeti moja pale Dar es Salaam. Kwa kuwa alipata kazi, na kwa kuwa wazazi wake hawakai Dar es Salaam, aliamua kutafuta chumba cha kupanga ili aanze maisha yake. Alihangaika kwa miezi nane bila kupata nyumba. Kila alipoenda, kwanza aliambiwa lazima awe na fedha ya kodi ya miezi sita na sehemu nyingine aliambiwa mwaka mzima. Hili lilikuwa gumu kwake kwasababu ndio alikuwa amepata kazi na anaanza maisha, pesa ya kodi kwa mwaka mzima hakuwa nayo.
Pili, sehemu nyingi wenye nyumba walimwambia kwamba hawakodishi nyumba kwa mtu ambaye hajaoa wala kuolewa. Kimsingi, hii sio haki. Lakini Dora hakuwa na pa kwenda.
Mheshimiwa Spika,
Huko nyumba, ilikuwepo Sheria ya Udhibiti wa Pango ya Mwaka 1984 (Rental Restriction Act of 1984), ambayo ilikuwa inamlinda Dora asitozwe kodi ya mwaka. Hata hivyo, Sheria hiyo ilifutwa mwaka 2005 na baadhi ya vipengele kuingizwa kama marekebisho ya Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 na Sheria ya Mahakama ya Ardhi ya Mwaka 2005. Hata hivyo, vipengele madhubuti vya kumlinda mpangaji vilitupwa kabisa.
Mheshimiwa Spika,
Yupo pia Bwana Saidi Bakari Shemweta, mzaliwa wa jimbo langu la Bumbuli anayeishi Mbagala. Ana familia ya watu wa sita: mke na watoto watatu na ndugu wengine wawili. Anafanya biashara ndogo ndogo na kipato chake ni cha siku kwa siku. Alikuwa na mkataba wa pango wa mwaka mzima. Lakini mkataba huo ulikuwa wa kuandikishiana kwenye kipande cha karatasi. Mkataba huo ulitengenezwa na mwenye nyumba na ulisheheni zaidi maslahi ya mwenye nyumba kuliko haki zake kama mpangaji. Alikuwa analipa kodi bila kupewa risiti. Na wapangaji wenzake nao wanalipa kodi bila risiti. Lakini yeye kwenye biashara zake, ambazo zina kipato kidogo kuliko cha mwenye nyumba, analipa kodi. Hali ya makazi anayoishi, kwa maana ya idadi vya watu kulinganisha na vyoo, hali ya upatikanaji maji, ilikuwa hailingani na kiwango cha kodi anayolipa. Na hata pale ambapo mwenye nyumba alipaswa kufanya matengenezo, hakuwa anafanya hivyo.
Pamoja na yote hayo, ghafla mwenye nyumba aliamua kupandisha kodi katikati ya mkataba kwa kuwa tu alipata mpangaji aliyekuwa tayari kulipa kodi kubwa kuliko Bwana Shemweta. Bwana Shemweta alitafutiwa kosa, akapewa notisi ya ghafla. Kwa kuwa hakuweza kupata nyumba ndani ya kipindi kifupi, kwa tatizo lilelile la kukosa kodi ya mwaka mzima, akalazimika kuondolewa kwa nguvu kwa vitu vyake kutolewa nje pamoja na watoto na ndugu zake. Hakujua pa kwenda kudai haki yake. Hakujua analindwa na Sheria gani na hakujua pa kuanzia.
Mheshimiwa Spika,
Naamini masaibu kama haya ya Dora na Shemweta yapo mengi na mengine ukisikia yanasikitisha zaidi. Sisi Wabunge tumekuja hapa Bungeni kama wawakilishi wa watu ili tutunge Sheria kwa manufaa ya walio wengi. Lakini tupo hapa tukitambua kwamba jamii yetu ina matabaka. Ina wanyonge na ina wenye mabavu. Ina watu wanaokunywa mvinyo wa dola 2,000 kwa chupa, na ina watu ambao hawajui mchana watakula nini. Lakini wote hawa wanahitaji makazi. Lakini kuna waliojaliwa kujenga nyumba zao, ambao makazi sio jambo lililo katika mawazo yao, lakini kuna wengi zaidi ambao hawakujaliwa ambao makazi ndio shaka yao kubwa. Katika kutunga Sheria lazima tuendeshwe na msingi wa kusaidia wanyonge, pamoja na kwamba tunalinda haki za raia wote wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2005, Bunge lilifuta Sheria ya Udhibiti wa Pango ya Mwaka 1984 (Rental Restriction Act of 1984) ambayo ilikuwa inatoa ulinzi kwa wanyonge ambao ni wapangaji. Sababu ya kuifuta Sheria hii ilikuwa ni kwamba eti Sheria za kudhibiti bei ni sheria za enzi za kijamaa na kwamba pango liachwe liwe kazi ya soko. Huu sio ukweli. Sheria hii ilitungwa mwaka 1962 wakati nchi yetu ilikuwa bado haijaingia kwenye siasa ya ujamaa. Lakini pia nchi nyingi za kibepari zina Sheria ya Kudhibiti Pango, ikiwemo Kenya, ambapo chini ya Sheria yao Namba 296, ni kosa kudai pango la zaidi ya miezi miwili, na Uganda, chini ya Sheria yao Namba 231. Vilevile, katika mageuzi ya uchumi wa nchi yetu tumeunda taasisi nyingi na tumetunga Sheria kadhaa zinazodhibiti bei za bidhaa mbalimbali – mfano: SUMATRA, bei za usafiri; EWURA, bei ya nishati; TCRA, bei za kupiga simu.
Mheshimiwa Spika,
Kama tumeona ni sahihi kuweka udhibiti kwamba makampuni ya simu za mikononi yasipandishe bei ya kupiga simu holela, kwanini tusiweke udhibiti kwenye hitaji muhimu la maisha ya mwanadamu, yaani makazi, kwamba mwenye nyumba asipandishe kodi holela, kwa kiwango na wakati wowote anaotaka?
Inawezekana kukawa na wasiwasi kwamba tukiweka udhibiti wa shughuli za pango, biashara ya upangishaji nyumba itaharibika na uwekezaji utazorota. Hiyo inawekana tu kama hakuna udhibiti wa Serikali. Ndio maana napendekeza kwamba katika Sheria ambayo Serikali basi kuanzishwe Mamlaka ya Udhibiti wa Biashara ya Nyumba (Real Estate Regulatory Agency – RERA) ambayo itadhibiti miendeno ya wadau wote katika sekta ya nyumba. Nchi nyingi zilizofanya vizuri katika sekta ya makazi zina mamlaka hizi.
Vilevile, tumeona kwamba, hata baada ya kuifuta Sheria ya Rental Restriction Act ya 1984, bado mahitaji ya nyumba yameongezeka na uwekezaji haujakidhi mahitaji.
Mheshimiwa Spika,
Sheria ninayopendekeza itungwe sio ya kudhibiti bei ya pango pekee. Ni sheria ya kudhibiti mwenendo mzima wa biashara ya upangaji ili wadau na washiriki wote kwenye biashara hii – yaani wenye nyumba, wapangaji, madalali, Serikali – wapate haki zao za msingi, na mashauri na migogoro ya nyumba ipate kushughulikiwa kwa haraka, kwa haki na kwa ukamilifu.
Vilevile, ni muhimu nikaweka wazi kwamba Sheria ninayopendekeza sio Sheria ya kuwakandamiza wenye nyumba. Ni sheria itakayolinda maslahi ya wote, kwani ni dhahiri kabisa kwamba wapo wapangaji ambao nao hawatimizi wajibu wao na ambao ni wasumbufu katika kulipa pango na wazembe katika kutunza mali za wenye nyumba.
Mheshimiwa Spika,
Ni dhahiri kwamba liko tatizo la nyumba na makazi nchini. Takwimu zinaonyesha kwamba kuna upungufu wa nyumba takriban milioni tatu nchini kwa sasa, na kwamba kila mwaka kunahitajika nyumba mpya 200,000. Kasi ya ujenzi wa nyumba haiendani na mahitaji haya licha ya uamuzi wetu wa kuweka uhuru mkubwa wa soko katika biashara hii. Lakini hatuwezi kukaa, kama Serikali na kama viongozi, na kukubali kwamba kwa kuwa kuna upungufu wa nyumba, na kwa kuwa soko la nyumba linawapa nguvu zaidi wenye nyumba, basi haki za wanyonge, ambao ni wapangaji, zisilindwe.
Mheshimiwa Spika,
Inawezekana ikaja hoja kwamba Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999, na Sheria ya Mahakama ya Ardhi ya Mwaka 2005, zinatoa kinga kwa wapangaji. Baada ya utafiti wangu, na kwa msaada wa wataalamu wa Sheria zinazohusiana na makazi, ukweli ni kwamba Sheria hizo hazitoshelezi. Kwa mfano, kwa Sheria za sasa, mwenye nyumba hana haja ya kwenda mahakamani kupata haki yake ya kimkataba - anaweza kuuza kitu chochote cha mpangaji, lakini mpangaji, ili kupata haki yake, ni lazima aende mahakamani ambako kuna mlolongo mrefu.
Kwa kweli hatuna haja kufanya utafiti wa kina kubaini tatizo kwenye shughuli za upangaji, matatizo kwenye sekta ya upangaji tunayona kila siku na tunayajua. Inahitajika Sheria mpya, mahsusi kabisa kwa masuala ya makazi ili Sheria hizi mbili zibaki katika masuala ya ardhi ambayo nayo pia yana mambo mengi.
Naamini katika azma ya Serikali kuboresha hali ya makazi nchini. Naamini katika uongozi thabiti wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ambaye anafanya kazi nzuri. Naamini kabisa kwamba tukitunga Sheria hii na ikasimamiwa vizuri tutakuwa tumewasaidia Watanzania zaidi ya milioni 14 wanaoathirika na udhibiti mdogo katika shughuli za upangaji.
Naamini pia kwamba, katika mchakato wa kutunga Sheria hii, wadau wote watashirikishwa kutoa mawazo na maoni yao.
Mheshimiwa Spika,
Kabla sijatoa hoja yenyewe napenda kuwashukuru viongozi wa Chama cha Wapangaji Tanzania walionisaidia na kunihimiza kuleta hoja hii. Nawashukuru pia waandishi wa habari walioandika habari na makala kuunga mkono kusudio la hoja hii. Nawashukuru marafiki zangu wote kwenye mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook kwa kunipa maoni na ushauri na kuunga mkono hoja hii. Nawashukuru wote, ikiwemo Wabunge walionipa moyo kuleta hoja hii.
Baada ya maelezo hayo, naomba sasa niwasilishe hoja yenyewe. Hoja hii inawasilishwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007, Kanuni ya 54 (i).
Mheshimiwa Spika,
KWA KUWA, asilimia kubwa ya Watanzania, hasa waishio mijini, wanaishi kwenye nyumba za kupanga, na karibu asilimia 40 ya kipato chao wanakitumia kwa ajili ya kulipia pango;
KWA KUWA, kumekuwa na udhibiti mdogo wa biashara ya upangaji, na kupelekea kuongezeka kwa vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wapangaji, ikiwemo kudaiwa pango la miezi sita hadi mwaka mzima, tena kwa fedha za kigeni;
KWA KUWA, kumekuwa na tatizo la makazi mijini na hivyo kuwalazimisha wapangaji kukubali masharti ya upangaji yanayoenda kinyume na haki, na kwa kuwa vitendo hivi vimekuwa vinaendelea kwa muda mrefu bila udhibiti;
KWA KUWA, hakuna Sheria mama inayodhibiti upangaji na inayolinda haki za mpangaji, na kwa kuwa Sheria ya Ardhi ya 1999 na Sheria ya Mahakama ya Ardhi ya 2005 hazitoa udhibiti kamilifu wa sekta ya upangaji nyumba,
HIVYO BASI, Bunge liazimie kuitaka Serikali, kwa haraka inavyowezekana, ilete Muswada wa Sheria ya Kudhibiti Shughuli za Upangaji wa Nyumba (Rental Housing Act) ambayo, pamoja na mambo mengine, itakaweka utaratibu na udhibiti wa sekta ya upangaji wa nyumba ikiwemo kuweka haki na wajibu wa wapangaji na wenye nyumba, kuweka mazingira ya ukuaji wa sekta ya makazi, na kuanzishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Sekta ya Nyumba (Real Estate Regulatory Authority).
Mheshimiwa Spika,
Naomba kutoa Hoja.
January Makamba
10 Februari 2012
Why are English majors disappearing?
5 months ago